Geita. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita, limefikia uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi 11 wa Serikali waliotenda makosa mbalimbali, ikiwamo utoro kazini, kushindwa kutekeleza majukumu yao, ulevi na ubadhirifu wa fedha za umma.
Hali hiyo imeelezwa kuwa ilikuwa ikikwamisha utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo kwa wananchi.
Uamuzi huo umetangazwa Ijumaa Mei 8, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Enock John alipokuwa akisoma taarifa ya uamuzi wa kamati maalumu ya uchunguzi katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26.
“Kwa mujibu wa Kanuni ya 57(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma ya 2022, imethibitika kuwa watumishi hao wameshukiwa na utoro na makosa mengine, hivyo baraza kwa kauli moja limekubaliana wafukuzwe kazi,” amesema John.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Enock John wakati akisoma maazimio ya baraza la madiwani kuwafukuza kazi watumishi 11 kwa kukiuka kanuni za utumishi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed, akizungumza na Mwananchi amesema baadhi ya watumishi wanatekeleza shughuli zao binafsi muda wa kazi, jambo linalosababisha miradi ya kimaendeleo kukwama.
“Baadhi ya watumishi wanatumia muda wa kazi kutengeneza fursa zao binafsi badala ya kuzingatia majukumu ya ofisi. Tunatoa onyo kwa watumishi wenzangu kutii maadili ya kazi,” amesema mkuu huyo.
Aprili 30, 2026, Halmashauri ya Wilaya ya Chato ilitangaza kuwafukuza kazi watumishi saba kwa makosa mbalimbali, ikiwamo utoro kazini, katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26.