
TAARIFA za ndani zinaeleza makubaliano ya uongozi wa Mtibwa Sugar ya kuachana na Kocha Yusuf Chipo, yapo hatua ya mwisho na ni suala la muda kutangaza rasmi, huku klabu hiyo ikisaka mbadala wake akitajwa beki wa zamani wa kikosi hicho ambaye pia amewahi kuinoa, Mecky Maxime.
Mtibwa ambayo imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya uliyopita wa 2024-2025 kucheza Ligi ya Championship, ipo nafasi ya 11 katika msimamo, imecheza mechi 22, imeshinda tano, sare nane, imefungwa tisa, inamiliki mabao 16, imetikiswa kwenye nyavu mara 29, ikikusanya alama 23, inatajwa ndiyo sababu ya kutaka kuachana na Chipo.
Chanzo kilisema wakati wanaandaa mazingira ya kupeana mkono wa kwa heri na Chipo, mazungumzo na kocha Maxime yanaendelea na endapo mambo yakienda vizuri atapokea kijiti.
“Tunazungumza na Maxime, kabla hatujafikia hatua ambayo timu hatuwezi kuinusuru, tumeamua kufanya maamuzi magumu ili tusije tukarejea Ligi ya Championship tulikotokea,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “Maxime anaifahamu vizuri Mtibwa kwani ameichezea na kuifundisha, tunaamini mchango wake unaweza ukatutoa tulipo na kwenda sehemu nyingine salama.”
Huduma ya Maxime inahitajika Mtibwa baada ya kocha huyo kuachana na Mbeya City Aprili 26, 2026 na alijiunga nayo Desemba 7, 2025 alipochukua mikoba ya Malale Hamsini.