KAMA kuna furaha ndani ya kikosi cha TRA United kwa sasa basi ni hatua ya kuangusha mbuyu kwa kuichapa Azam mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, lakini matajiri hao wa Chamazi wasilie peke yao kwani vigogo wengine wamekwama uwanjani hapo.
Ushindi huo wa TRA United uliopatikana Mei 8, 2026, sio tu umeiumiza Azam kwa kupoteza, bali pia umeikatisha rekodi ya matajiri hao ya kutopoteza kwenye ligi baada ya kucheza mechi 21, huku Yanga ikibaki pekee na rekodi hiyo msimu huu.
TRA United ikiwa nyumbani msimu huu, imezigomea timu zote zilizomaliza nafasi nne za juu msimu uliopita kwenye ligi zilipokwenda Sheikh Amri Abeid ambapo mbili imetoka 0-0 dhidi ya Yanga na Simba, huku ikizifunga Azam 4-1 na Singida Black Stars 2-0.
Yanga ilikuwa ya kwanza kufika kwenye uwanja huo Machi 18, 2026 na kukutana na mshtuko wa kulazimishwa sare tasa dhidi ya TRA iliyokuwa nyumbani. Bingwa huyo mtetezi alinusurika kufungwa dakika za mwisho kutokana na uimara wa kipa wake Djigui Diarra aliyeokoa hatari.
Baada ya mchezo huo kuonekana kama TRA imebahatisha, Aprili 5, 2026 ikafuata Singida Black Stars na kukutana na kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao. Mabao hayo yalitokana na beki Abdallah Kheri ‘Sebo’ kujifunga huku lingine likifungwa na Christopher Tebandeke kwa penalti.
Simba ilifuata baada ya Singida kuacha pointi tatu, ambapo Wekundu hao waliokuwa wakiicheka Yanga kwa kupata sare tasa, nao wakajikuta wakipata matokeo hayo hayo Aprili 9, 2026. Simba ilinusurika kupoteza baada ya bao la wakusanya kodi hao kukataliwa.
Azam ilifunga dimba ilipokubali kipigo hicho cha mabao 4-1 kilichowashtua matajiri hao wa Chamazi. Azam ilianza mchezo vizuri kwa kutangulia kufunga bao moja kabla ya kugeuziwa kibao kwa kishindo kwenye uwanja huo.
Hatua hiyo inaifanya TRA United kukusanya jumla ya pointi tano dhidi ya timu hizo zilizoshiriki mashindano ya Afrika msimu huu, huku ikilinda heshima yake nyumbani mbele ya vigogo hao wa soka nchini.
Hata hivyo, TRA imekuwa haina matokeo mazuri ilipozifuata timu hizo ugenini na Simba iliichapa mabao 3-0, Azam ikaitandika mabao 2-0, lakini ikaichapa Singida mabao 3-1. Sasa itasubiri kuvaana na Yanga Juni 27, 2026.