
Jumatatu, Mei 4, 2026, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliidhinisha bajeti ya Sh525 bilioni ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Hii ni bajeti kubwa zaidi ya fedha kuwahi kutengwa kwa wizara hiyo ikizidi ile ya mwaka uliopita kwa zaidi ya Sh6 bilioni.
Ikumbukwe kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wizara hiyo ilitengengewa bajeti ya Sh519.66 ambayo ilikuwa ongezeko la Sh234.36 bilioni kutoka bajeti ya mwaka mmoja nyuma yake kwa maana ya 2024/2025.
Tofauti na hapo nyuma, kwa miaka hii miwili ya fedha, kiasi kikubwa cha fedha kwenye bajeti zilizotengwa kitaenda moja kwa moja katika shughuli za maendeleo na kidogo kitaenda katika shughuli za kawaida za wizara.
Hapo mwanzo, shughuli za maendeleo ya michezo zilizokuwa zikitengewa kiasi kidogo cha fedha huku fungu kubwa likienda katika shughuli za kawaitrhda kama mishahara ya watumishi wa wizara.
Na hapana shaka kitendo cha Tanzania kuwa miongoni mwa wenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na nchi za Uganda na Kenya kimechangia kwa kiasi kikubwa wizara hii inayohusika na michezo kutengewa fedha nyingi kwa mwaka unaoisha wa fedha na huo unaokuja.
Hii ni kwa sababu uandaaji wa Fainali za AFCON unahusisha miradi mbalimbali ambayo inagharimu kiasi kikubwa cha fedha hivyo kama wizara itatengewa fungu dogo la fedha kwa shughuli za maendeleo, haitoweza kuitimiza na hivyo nchi itapoteza haki na sifa za kuandaa mashindano hayo yenye thamani na mvuto mkubwa zaidi katika soka barani Afrika.
Baafhi ya miradi hiyo ni ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya kutumika kwa mechi na mazoezi katika mashindano hayo, miundombinu ya usafiri na pia ya hamasa na matangazo kabla, wakati na baada ya mashindano hayo.
Lakini pia ukiondoa AFCON, kuna suala la ujenzi wa ukumbi mkubwa (arena) wa michezo ya ndani isiyo ya soka na matamasha, uendeshaji na uboreshaji wa Chuo cha Michezo cha Malya, ujenzi wa vituo vya michezo pamoja na uendeshaji wa michezo ya shule za msingi (mitashumta) na Sekondari (Umisseta).
Tunaamini bajeti hiyo ikitekelezwa vyema, kuna hatua kubwa ambayo nchi yetu itapiga katika michezo kama ambavyo mwanga umeanza kuonekana katika miaka ya hivi karibuni.
Nchi itakuwa na uhakika wa kuwa na viwanja bora zaidi vya soka na vilivyo na vigezo vya kimataifa vya kuandaa mechi za daraja la juu za soka hivyo wachezaji wetu watapaa jukwaa la kuonyesha vipaji vyao lakini hata kuvutia wawekezaji zaidi.
Uwekezaji mkubwa katika Chuo cha Michezo cha Malya utasaidia kuzalisha idadi kubwa ya wataalam wa uongozi, uufundishaji na uamuzi wa michezob wa viwango vya kimataifa ambao hivi sasa idadi yao ni ndogo hapa nchini.
Ujenzi wa vituo vya michezo utakuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha vijana wenye vipaji vikubwa vya michezo ambao watakuwa na msaada wa kiwango cha juu kwa timu zetu za taifa miaka ya usoni.
Lakini kama tukishindwa kuitekeleza vyema bajeti, hayo yaliyotajwa hapo juu hayawezi kutimia hivyo ni lazima kuwe na usimamizi mzuri wa fedha hizo zilizotengwa ili ziweze kuleta matokeo chanya.