Dar es Salaam. Wakati huduma ya uzazi pandikizi (IVF) ikiendelea kuwa tegemeo kwa wanandoa wengi wanaokabiliwa na changamoto ya kupata mtoto, mjadala umeendelea kuibuka kuhusu gharama za huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambako mzunguko mmoja wa matibabu hugharimu kati ya Sh14 milioni na Sh18 milioni.
Kwa watu wengi, kiwango hicho cha gharama huonekana kuwa kikubwa.
Hata hivyo, nyuma ya huduma hiyo kuna mfumo wa kisasa wa kitabibu unaohusisha matumizi ya teknolojia ya hali ya juu, wataalamu waliobobea wanaofanya kazi muda wote, vifaa vya gharama kubwa pamoja na mazingira maalumu yanayohitaji uangalizi wa saa 24.
Kwa mujibu wa Muhimbili, mgonjwa anayelipia Sh14 milioni na kufanikiwa kuhifadhi viinitete maabara, endapo mimba haitashika katika jaribio la kwanza, atalazimika kulipa Sh1 milioni kwa ajili ya kupandikizwa tena.
Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, anaweza kurudia huduma hiyo hadi mara nne, huku kila jaribio la ziada likihusisha gharama ya Sh1 milioni kwa ajili ya uhifadhi wa viinitete pekee.
Mkuu wa Kitengo cha Upandikizaji Mimba katika hospitali hiyo, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi pamoja na mtaalamu wa uzazi pandikizi, Matilda Ngarina anasema watu wengi hudhani gharama za IVF zinahusisha sindano na dawa pekee.
Anasema huduma hiyo hutegemea mfumo mpana wa kitabibu na maabara nyeti zinazohitaji uangalizi wa hali ya juu wakati wote.
“Watu wengi hudhani ni gharama za sindano na dawa tu, lakini ndani yake kuna mambo mengi. Kuna matumizi ya nitrojeni ya kimiminika, gesi, umeme wa jenereta la akiba, walinzi wanaokesha usiku kucha, matengenezo ya vifaa, pamoja na upimaji na urekebishaji wa usahihi wa vifaa vinavyotunza viinitete katika viwango maalumu vya joto. Haya yote ni sehemu ya gharama za huduma hiyo,” anasema Dk Ngarina.
Maabara ya uhai saa 24
Dk Ngarina anasema maabara ya IVF ni mazingira maalumu yanayofanya kazi kama kiwanda cha uhai, hitilafu ndogo tu inaweza kuharibu mchakato mzima wa matibabu.
Anasema vifaa vinavyotumika kuhifadhi viinitete, mayai na mbegu za uzazi hulazimika kufanya kazi katika viwango maalumu vya joto, hewa na unyevunyevu bila mabadiliko yoyote.
“Mashine za kutunzia viinitete katika joto maalumu zinahitaji matengenezo ya mara kwa mara, urekebishaji pamoja na upimaji wa usahihi wake. Wakati mwingine vifaa hivyo hupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati na kupimwa kisha hurudishwa. Haya yote yana gharama,” anasema Dk Ngarina.
Aidha, anasema mfumo wa umeme wa kituo hicho unahitaji uangalizi mkubwa zaidi ikilinganishwa na maabara za kawaida.
“Huwezi kuruhusu umeme kukatika hata kwa sekunde chache. Kuna jenereta la akiba na wataalamu wanaohakikisha mfumo wote unaendelea kufanya kazi ipasavyo. Hitilafu ndogo tu inaweza kuathiri mfumo mzima,” anasema.
Dk Ngarina anasema gharama za huduma hiyo zinajumuisha pia matumizi ya gesi maalumu za maabara, nitrojeni ya kimiminika inayotumika kuhifadhi viinitete, vifaa vya matumizi ya kila siku pamoja na mishahara ya wafanyakazi wa zamu za usiku.
“Hata vifaa vya usafi kama karatasi laini, maji, huduma za usafi pamoja na watu wanaokesha usiku kucha kuhakikisha kila kitu kiko sawa, hulipwa. Hii ni huduma inayotolewa saa 24,” anasisitiza.
Anasema gharama ya kati ya Sh14 milioni na Sh18 milioni huhusisha mchakato mzima kuanzia hatua ya kuanza matibabu hadi mgonjwa anapopata ujauzito, lakini haijumuishi gharama za kujifungua wala huduma nyingine za baadaye.
Dawa na changamoto ya ununuzi
Mbali na gharama za vifaa na uendeshaji wa maabara, dawa zinazotumika katika huduma ya uzazi pandikizi (IVF) nazo ni changamoto kubwa kutokana na gharama zake na upatikanaji wake.
Dk Ngarina anasema dawa nyingi zinazotumika katika matibabu hayo huagizwa kutoka nje ya nchi, huku zikiwa na gharama kubwa pamoja na muda mfupi wa matumizi.
“Huwezi kununua dawa nyingi na kuzihifadhi kwa muda mrefu, kwa sababu baadhi yake huisha muda wa matumizi ndani ya miezi miwili au mitatu,” anasema Dk Ngarina.
Anasema awali Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilikumbana na changamoto ya kupata wasambazaji wa dawa hizo kupitia mfumo wa ununuzi wa Serikali.
“Mwanzoni tulidhani tunaweza kuwasiliana moja kwa moja na watengenezaji wa dawa, lakini baadaye tukagundua kuwa wanafanya kazi kupitia wasambazaji wao maalumu,” anasema.
Kwa sasa, hospitali inaendelea kufanya mazungumzo ya muda mrefu na wasambazaji ili kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa urahisi zaidi.
Safari ya IVF si sindano pekee
Dk Ngarina anasema watu wengi hawaelewi mchakato mzima wa IVF, ambao huanza kwa mama kupewa dawa za homoni ili kuchochea uzalishaji wa mayai mengi.
Anasema sindano hizo hutolewa kwa takribani siku 14 kabla ya hatua ya kuvuna mayai kufanyika kwa njia maalumu ya kitabibu.
Baada ya hapo, mayai hupelekwa maabara ambako huunganishwa na mbegu za mwanamume ili kutengeneza viinitete ambavyo baadaye hupandikizwa kwenye kizazi cha mwanamke.
“Kuna kipindi cha matumizi ya sindano za homoni kinachoweza kufikia siku 14. Baada ya hapo tunachukua mayai, tunatengeneza viinitete, kisha tunavipandikiza kwenye kizazi,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa IVF si huduma yenye uhakika wa mafanikio kwa asilimia 100.
“Watu wengi hudhani IVF ina mafanikio ya uhakika, lakini kwa wastani kiwango cha mafanikio ni takribani asilimia 40. Kuna wakati mnawafanyia wagonjwa wote matibabu lakini hakuna anayepata ujauzito, bila sababu ya moja kwa moja kueleweka,” anasema Dk Ngarina.
Anasema kuna nyakati hata wataalamu hushindwa kueleza kwa nini baadhi ya viinitete vinavyoonekana kuwa bora havifanikiwi kushika mimba, huku vingine vilivyoonekana dhaifu vikifanikiwa.
“Unaweza kupandikiza viinitete viwili vizuri kabisa lakini visifanikiwe kushika mimba. Wakati mwingine kile kilichoonekana dhaifu ndicho kinachofanikiwa. Kuna mambo ambayo bado hatujayaelewa kikamilifu kama binadamu,” anasema.
Aidha, anasema huduma ya IVF haiendeshwi na daktari mmoja pekee, bali huhusisha wataalamu wa kada mbalimbali wanaofanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.
“Tunao wataalamu wa biolojia ya maabara wanaoshughulikia mayai na mbegu za uzazi, madaktari wanaowahudumia wagonjwa, wataalamu wa upasuaji wa matundu (laparoscopy), pamoja na washauri nasaha wanaosaidia wagonjwa upande wa kisaikolojia,” anasema Dk Ngarina.
Kwa sasa, huduma hiyo inatolewa na wataalamu wa Kitanzania waliopata mafunzo ndani na nje ya nchi, huku baadhi ya wataalamu wa kimataifa wakishiriki katika hatua za awali za kuimarisha mfumo huo.
Siku 14 za hofu na matumaini
Kwa wagonjwa wengi, kipindi kigumu zaidi huanza baada ya viinitete kupandikizwa na kusubiri majibu ya matokeo.
Dk Ngarina anasema siku 14 za kusubiri majibu huwa na msongo mkubwa wa mawazo kwa wanandoa wengi.
“Hii ni presha kubwa sana. Wengine hupima nyumbani hata kabla ya siku waliopangiwa hospitalini. Mwingine akianza kuona dalili za hedhi hupiga simu akisema, ‘daktari, nimeanza hedhi nifanye nini?’” anasema.
Anasema wagonjwa hupokea matokeo kwa namna tofauti kulingana na hali zao za kihisia.
“Wengine hukubali matokeo kirahisi, wengine hulia na wengine hutaka kuelewa kila hatua iliyofanyika. Kila mtu ana namna yake ya kukabiliana na hali hiyo,” anasema Dk Ngarina.
Kutokana na changamoto hizo za kihisia, anasema huduma ya ushauri nasaha imewekwa kuwa sehemu muhimu ya matibabu ya IVF.
Kwa nini mafanikio hushuka?
Kwa mujibu wake, hata uzazi wa kawaida wa binadamu una kiwango kidogo cha mafanikio kwa kila mwezi.
“Kati ya wanandoa 10 wenye afya njema, ni wawili au watatu tu wanaweza kupata ujauzito kila mwezi bila msaada wa kitabibu. Hiyo ndiyo asili ya mwanadamu,” anasema.
Dk Ngarina anafafanua kuwa mafanikio ya IVF hutegemea mambo mengi, ikiwamo ubora wa mayai, mbegu za mwanamume, afya ya kizazi pamoja na mwitikio wa mwili wa mwanamke.
“Unaweza kufanya kila kitu kwa usahihi lakini mwili ukakataa. Hapo ndipo tunasema bado kuna mambo ambayo hatuyafahamu kikamilifu,” anasema.
Surrogacy na uhifadhi wa mayai
Dk Ngarina anasema huduma ya ubebeshaji wa mimba kwa mama mwingine (surrogacy) bado haijaanza rasmi nchini kutokana na ukosefu wa sheria maalumu zinazosimamia huduma hiyo.
Kuhusu huduma ya kuhifadhi mayai kwa wanawake, anasema pia haijaanza rasmi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na gharama kubwa pamoja na changamoto za kiteknolojia.
Hata hivyo, hospitali tayari inatoa huduma ya kuhifadhi mbegu za kiume pamoja na viinitete kwa baadhi ya wagonjwa.