Unguja. Wakati bei mpya za tiketi za boti zilizotangazwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) zikianza kutumia leo, wananchi wameendelea kuiangukia Serikali kuwapunguzia gharama hizo ili kuwapa ahueni.

Mamlaka hiyo ilitoa taarifa kwa umma kuhusu ongezeko la bei ya tiketi kwa vyombo vya usafiri baharini vinavyobeba abiria Mei 6, 2026 na kuanza kutumika leo.

ZMA imetangaza ongezeko la bei ya tiketi ya boti kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam itakuwa Sh40,000 kutoka Sh35,000 kwa daraja la chini na nusu tiketi itauzwa kwa Sh20,000 na bei ya Flying Horse itakuwa Sh22,000 kutoka Sh20,000.

Wakizungumza na Mwananchi, wakazi kutoka maeneo mbalimbali kisiwani hapa wamesema kutokana na kipato chao hawawezi kumudu gharama za bei hiyo.

Saumu Juma, mkazi wa Kisauni, amesema licha ya Serikali kueleza sababu za kupanda, kwa gharama hizo bado wananchi wa kipato cha chini ndio wanaobeba mzigo mkubwa kutokana na hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha.

“Hii haitamuathiri mtu mwenye uwezo wa kifedha ni sisi wananchi wa kipato cha chini ndio tunaoubeba mzigo huu unatuumiza, ongezeko la Sh5,000 kwetu ni kubwa sana,” amesema.

Amesema Serikali inapaswa kutafuta njia bora za kupunguza nauli hizo za boti kwa kuwa, hilo ndio tegemeo lao hakuna mwingine.

Mwananchi Haji Massoud Ahmed ametoa rai kwa wamiliki wa majahazi kuboresha vyombo vyao ili wananchi watumie kwa sababu hakuna namna nyingine ya kufanya.

“Tunaamini wamiliki wa majahazi wakiboresha wanyonge tutakuwa ndio kimbilio letu kwa sababu hatuna msaada wowote hadi kufikia hapa,” amesema.

Imrani Hassan Hasuni amesema uamuzi huo ni kuonea abiria Zanzibar, kwa sababu hizo boti zina uwezo wa kununua mafuta na nauli ikabaki ya Sh35,000 na sio Sh40,0000.

Amesema kawaida za vyombo usafiri vinakimbilia kupandisha nauli za boti kupata faida za juu lakini kwenye jambo lakushusha hawataki kulielewa.

Pia, amesema wananchi wanaweza kukubaliana na hilo kwa wakati ila wanaiomba Serikali mafuta yakishuka na bei zishuke kwa sababu kila mwaka nauli za boti zinapanda.

Naye, Salim Hussein amesema wananchi wengi wanakufa kwa sababu ya msongo wa mawazo ya maisha, mafuta hayapanda Tanzania pekee.

Amesema gharama za maisha zimekuwa kubwa huku kipato wanachopata hakikidhi mahitaji yao ya kila siku kutokana na nauli kadiri siku zinavyoendelea nauli zinapanda.

Salim ameiomba Serikali iwafikirie wananchi katika hilo kwani hali inazidi kuwa mbaya upande wao na Serikali ndio tegemeo la wananchi.

Kampuni ya Zan Fast Ferries imetangaza mabadiko ya nauli jana ambapo daraja la chini itakuwa Sh40,000 na daraja la juu (VIP) ni Sh80,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *