Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amekemea mahubiri chonganishi, akieleza kwamba yanachangia wananchi kuacha kwenda hospitali kupata huduma na badala yake wanategemea maombi ili kupona maradhi yanayowasumbua.

Amesema kumekuwepo na ramli chonganishi kwenye maeneo ya waganga wa kienyeji katika jamii na sasa kumeanza kuwepo kwa mahubiri chonganishi miongoni mwa watu wa Mungu.

Mtaka amesema hayo leo Mei 11, 2026 wakati akizindua kambi ya afya bure itakayotoa huduma za kibingwa na madaktari katika Kanisa la Waadventist Wasabato lililopo mkoani Njombe.

Amesema imefikia hatua mtu anaumwa haambiwi akafanye vipimo wala matibabu badala yake anaambiwa kuwa amerushiwa jini au kurogwa na ndugu wa karibu na matokeo yake anapoteza maisha.

“Mtu anaumwa haambiwi akafanye vipimo wala matibabu, anaambiwa wewe umerushiwa kipande, umerogwa na jirani yako unatengenezewa wachawi kwenye kaya unayotokea, unaambiwa una mapepo, unakemewa, unaanguka unakuja kuzungumza na kutoa ushuhuda wa uongo,” amesema Mtaka.

Amesema mambo hayo ambayo wakati wa giza yalifanyika kwenye nyumba za watu ambao hawakuwa na ufahamu wa kwenda kwa waganga wa kienyeji kupata tiba, yanaanza kufanyika.

“Leo kuna mahubiri ukiyasikiliza huwezi kujua tofauti ya yale mahubiri na kazi za mganga wa kienyeji , kama ambavyo ukiangalia kwenye TV siku hizi huwezi kujua hii ni Twanga Pepeta au muziki wa injili,” amesema.

Amesema wakati Serikali inakemea ramli chonganishi ambayo mkoani Njombe hakuna kuna kila sababu pia ya kukemea mahubiri chonganishi ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu.

Amelipongeza Kanisa la Waadventist Wasabato kwa kuandaa kambi hiyo na kutoa huduma kwa wananchi akisema itasaidia kubaini changamoto zao na kupatiwa matibabu.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kwenye kambi hiyo kupatiwa vipimo kulingana na changamoto zao ili baadaye waweze kupatiwa matibabu ya kibingwa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Juma Mfanga amesema moja ya changamoto iliyopo mkoani humo ni upatikanaji wa huduma ya macho ambayo bado haijaimarika.

Amesema kwenye kambi hiyo ya afya kuna dawa nyingi ambazo zinatolewa bure tofauti na vituo vya afya vya Serikali ambavyo havitoi dawa labda kwa kundi maalumu la watu.

“Mimi naomba wenzetu waliopo majumbani wafike hapa kwa ajili ya kupata huduma hapa hawatibiwi Wasabato, wanatibiwa watu wote,” amesema Mfanga.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda amesema kwa upande wake hajawahi kuona mikusanyiko mingine ya kidini kama pia huwa wanatoa huduma za kitabibu kama ilivyo kwa kanisa hilo la Wadventisti Wasabato.

“Kwasababu kuna watu wengine hawaamini ya kwamba mwanadamu anaweza kuugua na kupata maradhi, lakini kuna watu tu wanaamini kwamba mtu akiugua anatakiwa atibiwe kiroho tu na hapaswi kunywa dawa wala kupata huduma za kitabibu,” amesema Sweda.

Mkuu wa Idara ya Afya Chama cha Wajasiriamali Waadventist Wasabato Tanzania (ATAPE), Dk Samwel Kikaro amesema kwa Mkoa wa Njombe wamepanga kuwapatia huduma za afya zaidi ya wananchi 3,000.

“Huduma ambazo tutazitoa ni huduma za macho, uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, afya ya wanawake na Utra Sound, magonjwa ya watoto, huduma za mfumo wa mkojo, tezi dume, huduma za meno, magonjwa ya moyo na huduma za maabara,” amesema.

Askofu Kanisa la Wadventisti Wasabato Jimbo la Kusini, Joseph Mgwabi amesema kanisa hilo linataka neno la Mungu liendane na huduma kwa jamii na ndiyo sababu ya kuweka kambi ya afya ili wananchi waweze kupatiwa huduma hiyo muhimu.

“Siku ya leo tunafungua kambi rasmi ya afya ambayo ni sehemu ya mahubiri haya yanayoendelea hapa ili kuliweka neno katika vitendo,” amesema Mtaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *