
Timu mbili zimefanikiwa kupanda daraja na kuingia Ligi ya Championship baada ya kufanya vyema katika daraja la First League.
Kufuatia kila moja kuongoza kundi lake katika First League, Maafande wa Rhino Rangers wa Tabora wamepanda na msimu ujao watakuwa miongoni mwa timu 16 za Championship kama ilivyo kwa Bandari Tanzania ya Dar es Salaam.
Upo uwezekano wa timu nyingine mbili kati ya nne za First League kwenda Championship kupitia mchujo (play off) ambao kwanza utazihusisha zenyewe kisha zile za ligi ya Championship.
Timu nne za First League ambazo zinanukia kucheza mchujo ni Endurment, IAA SC, Nyumbu na Cosmopolitan.
Kwa upande mwingine, timu mbili zimefanikiwa kufuzu daraja la First League baada ya kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mikoa iliyofikia tamati mkoani Kigoma, Mei 2, 2026.
Timu hizo ni Kajuna FC ya Kigoma na Madini Kahama ya Shinyanga huku timu za Mount Hanang ya Manyara na Stand Masasi ya Mtwara zenyewe zikifanikiwa kupata tiketi ya kucheza mechi za mchujo kuwania nafasi nyingine mbili za kucheza First League msimu ujao.
Wahenga walisema ukishindwa kujipanga basi umepanga kushindwa. Tunaweza kuitumia kauli hii kuzikumbusha timu hizo ambazo zimefanikiwa kupanda katika madaraja ya juu zaidi ya yale ambayo zilikuwepo msimu huu.
Wakati huu ambao timu nyingine zinaendelea na ligi zao, hatutegemei kuona Rhino Rangers, Bandari Tanzania, Kajuna FC na Kahama Madini wakaiga kufanya jambo hilo hasa upande wa utawala kwa vile wanakabiliwa na vibarua vigumu msimu ujao katika ligi wanazokwenda kushiriki.
Nyakati kama hizi wanaopaswa kupumzika ni wachezaji tu wa timu zao lakini kwa viongozi, hiki ni kipindi ambacho wanapaswa kufanya kazi ya ziada kutengeneza mpango mzuri wa maandalizi ya klabu zao ili ziweze kutamba katika msimu ujao na kutimiza malengo ya msingi.
Hapana shaka, kwa kupanda Championship, lengo la mama la Bandari Tanzania na Rhino Rangers katika Ligi ya Championship msimu ujao ni kupanda Ligi Kuu ya NBC.
Kwa upande wa Kahama Madini na Kajuna, lengo lao kuu msimu ujao ni lazima liwe kupanda daraja la Championship.
Na jambo kubwa ambalo viongozi wa timu hizo nne wanapaswa kulifanya katika nyakati hizi ni kushirikiana na mabenchi yao ya ufundi kufanya sajili za wachezaji ambao watakwenda kuongeza nguvu na ubora katika vikosi vyao kuendana na malengo yao.
Usajili huo unapaswa kufanyika kwa kuzingatia mahitaji ya kikosi kulingana na udhaifu ambao umeonekana katika msimu huu na sio kujaza tu namba ya wachezaji kikosini.
Zikumbuke kwamba mashindano ambayo zinakwenda kushiriki sio mepesi na zitakutana na timu bora zilizoandaliwa vizuri kimbinu na kiufundi.
Zinapaswa kusajili wachezaji kadhaa wa kuziongezea uzoefu ambao utaziwezesha kuhimili ushindani ambao uko mbele yao na sio kuamini wale ambao wako katika vikosi vyao hivi sasa.
Ikumbukwe kuanzia First League na kuendelea hakuna zuio la kikanuni juu ya umri wa wachezaji kama ilivyo kwa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa ambayo kanuni inalazimisha timu iwatumie wachezaji walio na umri chini ya miaka 20 tu.
Katika madaraja hayo ya juu huwezi kuwatumia wachezaji wote wenye umri chini ya miaka 20 kwa vile watakutana na wazoefu na waliopevuka zaidi jambo litakaloigharimu timu.
Eneo lingine ambalo timu hizo zinatakiwa kujiimarisha ni la kiuchumi.
Uzoefu unaonyesha kuwa kadri timu inavyopanda daraja, ndivyo gharama za uendeshaji na usimamizi wa timu zinavyozidi kuongezeka.
Kwa mfano, katika mabingwa wa mikoa timu inatumia gharama kidogo kulinganisha na First League kwa vile hatua ya mwanzoni mechi zote inacheza mkoani kwake na hatua inayofuata ya makundi inaenda katika kituo kimoja.
Lakini katika First League italazimika kucheza mechi saba za ugenini ambazo baadhi au zote zinaweza kuwa nje ya mkoa wake.
Hata suala la kuimarisha vikosi vyao pia litahitaji bajeti kubwa ya fedha tofauti na sajili zao za awali. Mahitaji ya wachezaji wa kucheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa hayawezi kuwa sawa na ya daraja la juu yake kama ilivyo yale ya First League ni madogo kulinganisha na Championship.