
Njombe. Maofisa habari nchini wametakiwa kuitangaza miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ili wananchi waifahamu na kujivunia nayo.
Hatua hiyo inatajwa kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi na kujua shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali yao na walinde miradi kwa maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa jana Mei 10, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati akifunga kikao kazi cha 21 cha maofisa habari nchini kilichofanyika mkoani Njombe.
Amesema ukisoma Dira ya Taifa, uchumi mpya unaotajwa kwenye dira hiyo ni uchumi wa Liganga na Mchuchuma na uwekezaji wake kwenye miradi hiyo ni Sh7 trilioni lakini wengi hawafahamu kuhusu mradi huo.
Amesema kwenye ilani ya uchaguzi imeainisha miradi mikubwa ambayo imepewa kipaumbele katika utekelezaji wa dira ya miaka mitano upo wa Liganga na Mchuchuma, Maganga Matitu na Kate.
“Kwa hiyo hapa utaona tunajenga reli ya kutoka Ludewa, Njombe, Makambako kujenga viwanda vya kuongeza thamani kwenye chuma, kwa hiyo hivyo vitu vingi watu hawavifahamu kwa sababu idara yetu ya habari inaandika vitu vilivyozoeleka,” amesema Mtaka.
Mtaka kwa upande mwingine amewataka maofisa hao kutumia fursa zilizopo mkoani humo kuwekeza ili wanapomaliza utumishi wao serikalini wajimudu kimaisha kama wanavyoishi sasa wakiwa kazini.
Amesema pamoja na maofisa hao kupata nafasi ya kukutana na kubadilishana uzoefu, wanapaswa pia kuziona fursa zilizopo na kuzitumia kukuza uchumi wao binafsi na Taifa kwa jumla.
Amesema taasisi inapopata mafanikio, yanapaswa kwenda sambamba na mtumishi kwa kuhakikisha mshahara anaoupata anautumia vizuri kwa kuwekeza katika maeneo tofauti.
Ametoa wito kwa wananchi na wawekezaji nchini kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo mbalimbali katika sekta za kilimo, ufugaji na biashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Kelvin Kanji ameushukuru uongozi wa mkoa kwa kuwapokea vizuri na kuwapa ushirikiano katika kipindi chote ambacho vikao vilikuwa vikiendelea mkoani humo.
“Tunakushukuru wewe na timu yako ya mkoa tumepata ushirikiano mkubwa kwa hakika mkuu wa mkoa una watu wakarimu,” amesema Kanji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Mawasiliano serikalini, Zamaradi Kawawa amesema kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanikiwa kutoa huduma kwa wananchi wapatao 839.
“Wakati wa mafunzo haya ya maofisa habari tumeweza kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Njombe 839,” amesema Kawawa.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Rebeka Lwitiko amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwao kwa kuwa, yanaenda kuboresha utendaji wa kazi zao.
“Tumepata mafunzo ambayo tunaenda kuyafanyia kazi lakini pia tumeona fursa mbalimbali zilizopo Njombe,” amesema Lwitiko.