
Unguja. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema nchi za Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika lazima ziwekeze kwenye mifumo ili kila operesheni inayofanyika iwe kwenye mfumo.
Mwenda ametoa kauli hiyo leo Mei 11, 2026, wakati akifungua kikao cha 43 cha Kamati ya Uongozi ya Mkutano wa Shirika la Forodha Duniani, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA), kinachofanyika Zanzibar na kuzishirikisha nchi wanachama 24 za ukanda huo.
“Nchi lazima ziwekeze zaidi kwenye mifumo ili kila operesheni inayofanyika iwe kwenye mfumo, kwani inategemea nchi hizi kubadilishana taarifa na takwimu.
“Kama ilivyo Tanzania, mfumo wa TANSIS tangu mtu anapoanza kuagiza mzigo mpaka anapotolewa mzigo, mchakato wote unafanyika kwenye mfumo. Ila watu wakifanya mfumo usifanye kazi, maana yake biashara zitakwama na mapato ya Serikali yanaweza kuwa hatarini,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwenda, lazima zichukuliwe hatua za makusudi kuzuia vihatarishi kwenye biashara, kwa sababu jambo hilo halikwepeki kutokana na mifumo hiyo.
Kamishna Mwenda amesema kazi kubwa ya forodha ni kulinda usalama wa nchi, kwani ipo mipakani kuhakikisha hakuna magendo yanayoingia kupitia mipaka hiyo.
“Tunafanya hivyo kwa kuzuia magendo na bidhaa zisizoruhusiwa. Kwa hiyo ni kazi kubwa, lakini bado kuna changamoto ya kuchelewesha mizigo. Watajadili na kuja na mikakati maalumu kuhakikisha changamoto zinatatuliwa,” amesema.
Amesema katika utendaji kazi wa kuzuia magendo lazima kuwapo na umakini ili kutochelewesha biashara, jambo ambalo linaweza kuwa na athari katika mapato ya nchi.
“Wakati tunazuia watu wasiingie na bidhaa zisizoruhusiwa, tunachelewesha biashara. Watu wasicheleweshwe wakafanye biashara zao na uchumi ukue. Kwa hiyo kuna mambo watafanya na mikakati ya kuzuia vihatarishi vya usalama wa nchi bila kuathiri biashara,” amesema Mwenda.
Amesema nchi zinataka kuendelea na zinahitaji mapato, kwani kuna watu wanapunguza mizigo na wengine wanashirikiana na watendaji kutoa mizigo bila kufuata utaratibu.
Naye Mkurugenzi wa WCO ESA, Josephine Manyasi, amesema kazi yao ni kujenga uwezo kwa maofisa wa forodha katika ukanda huo wenye nchi 24, hivyo wamekutana kwa ajili ya kujengeana uwezo.
“Mikakati tuliyoweka ni kusaidia maofisa wa forodha. Kwa hiyo tumeungana kama kanda. Kuna mataifa yamekwenda mbele katika kujengeana uwezo, hivyo tunaunganisha uzoefu kuja pamoja kufundisha watendaji wao,” amesema.
Amesema wanataka kukuza mtalaa wa maofisa wa forodha katika mazingira ya pamoja ili watambue michakato inayoweza kutumika katika mataifa yote na wawe na mpango mmoja.
“Tusiwe nchi moja inafundisha watendaji wao hivi na nyingine inafundisha hivi, jambo ambalo litasababisha kukwamisha biashara,” amesema.
Naye mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Forodha Kenya, Dk Emmau Omwenga, amesema wanataka kuona namna watakavyoinua maofisa wanaofanya kazi katika forodha ili kupatikana ushuru mzuri.
Amesema mkutano huo ukiisha anaona utasaidia sana nchi katika kujengea uwezo, hivyo nchi husika zitakuwa zimeimarika katika uwezo wao.