
Dodoma/Dar. Serikali imesema inakamilisha maboresho ya mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ambao awamu ya pili ya uandikishaji wa wananchi, itahusisha kifurushi cha Sh150,000 kwa mwaka kwa kaya yenye watu wasiozidi sita.
Maboresho hayo yanalenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa huduma, kudhibiti gharama za matibabu na kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa mpango huo.
Wakati jana, Wizara ya Afya ikiomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh1.8 trilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27, imeeleza kuwa awamu ya pili itakayohusisha kaya 589,000 inalenga kusajili kaya zisizo na uwezo na wananchi wenye uwezo wa kujigharamia.
Bima ya Afya kwa Wote imetajwa kuwa miongoni mwa vipaumbele sita vya mpango na bajeti, mapato na matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo vya Wizara ya Afya, kwa mwaka 2026/27.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni Dodoma jana, Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa amesema awamu hiyo mpya inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wengi zaidi kupitia mfumo wa bima ya afya unaozingatia kaya.
“Kwa sasa tunakamilisha maboresho ya mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza ufanisi wa usimamizi, kudhibiti gharama za huduma na kuwezesha kuanza kwa awamu ya pili ya uandikishaji wa wananchi kwa kitita cha Sh150,000 kwa mwaka kwa kaya yenye watu wasiozidi sita,” amesema.
Amesema chini ya mpango huo, kaya zitalipa Sh150,000 kwa mwaka kwa huduma za afya kwa familia yenye watu wasiozidi sita, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama za matibabu na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bila vikwazo vya kifedha.
“Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote iliyopitishwa mwaka 2023, inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa uhakika bila kubanwa na gharama,” amesema Mchengerwa.
Waziri huyo amesema awamu ya pili inalenga kusajili kaya 589,000, zikiwamo zisizo na uwezo pamoja na wananchi wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya usajili na usimamizi wa bima hiyo ili kuongeza ufanisi, kudhibiti udanganyifu na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika vituo vya afya.
Amesema katika awamu ya kwanza, tayari kaya 172,297 zimefikiwa, sawa na asilimia 62 ya lengo la awali, huku wananchi 463,000 wakinufaika na huduma kupitia mfumo huo.
Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu ameishauri Serikali kuwekeza kwenye Bima ya Afya kwa Wote kupitia uchangiaji wa miamala ya simu, lakini akashauri kusiwe na uanzishwaji wa tozo mpya.
Kingu amesema katika utafiti alioufanya, amegundua ndani ya mwaka kuna Sh158.4 trilioni zinasambazwa kupitia mitandao ya simu, akashauri ikiwa kutakuwa na makato ya walau Sh10 kwenye kila muamala, Tanzania inaweza kukusanya Sh4 trilioni kwa mwaka.
“Sisemi mkaanzishe tozo mpya ili mlete mzigo kwa Watanzania, tumieni utaratibu mkae na vijana, wako tayari kuwapeni mbinu, kukata kidogo walau Sh10 hata shilingi tano, mtakusanya pesa na mtaanza kutoa huduma bora, anzeni kesho na siyo lini,” amesema Kingu.
Mbunge huyo amesema hakuna Mtanzania anayeweza kukataa kukatwa fedha kidogo wakati anajua akienda hospitali atakutana na madaktari wazuri, dawa za kutosha na miundombinu mizuri, hivyo hakutakuwa na malalamiko.
Bajeti ya Sh1.8 trilioni
Katika bajeti hiyo, Mchengerwa amesema wizara imeomba Sh1.8 trilioni, kati ya hizo, Sh1.148 trilioni sawa na asilimia 64 zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo, huku Sh652 bilioni zikitumika kwa matumizi ya kawaida.
Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Sh516 bilioni zitatumika kwa mishahara ya watumishi wa afya na Sh135 bilioni kwa matumizi mengine ya uendeshaji.
Amesema fedha hizo zitalenga kuimarisha miundombinu ya afya, vifaa tiba, huduma za kibingwa pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Ongezeko la magonjwa
Mchengerwa amesema watu milioni 39.9 walipata huduma za matibabu nchini katika mwaka wa fedha 2025/26 huku magonjwa ya mfumo wa hewa, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), malaria na kuharisha yakiongoza kwa idadi ya wagonjwa waliofika hospitalini.
Amesema kati ya wagonjwa 36,996,862 waliopatiwa huduma, wagonjwa 35,260,883 walitibiwa nje na wengine 1,735,979 walilazwa hospitalini.
Mbali na magonjwa hayo, maradhi ya ngozi, shinikizo la damu na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) nayo yameendelea kuwa changamoto kubwa kwa wananchi.
Aidha, wagonjwa 55,300 walihudumiwa kupitia mpango wa Madaktari Bingwa wa Samia katika halmashauri 184 nchini.
Waziri Mchengerwa pia ameeleza hali ya magonjwa nchini, akibainisha kuwa pamoja na mafanikio ya upatikanaji wa huduma, Tanzania inakabiliwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema magonjwa ya mfumo wa hewa, malaria, kuharisha na maambukizi ya njia ya mkojo bado yanaongoza, lakini pia magonjwa kama shinikizo la juu la damu, kisukari na magonjwa ya viungo yameingia kwenye orodha ya magonjwa 10 yanayoongoza kuwapeleka wananchi hospitalini.
Ameonya kuwa hali hiyo inachangiwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha kama ulaji usiofaa, matumizi ya pombe kupita kiasi, uvutaji sigara na kutofanya mazoezi.
Kamati ya Bunge yatoa tahadhari ya miradi
Wakati Waziri akieleza mafanikio na mipango ya Serikali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Dk Zeyana Abdallah Hamid imeeleza wasiwasi kuhusu kasi ya utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo.
Dk Zeyana amesema uchambuzi wa kamati umebaini kuwa, katika mwaka wa fedha 2025/26, ni asilimia 46 tu ya fedha za ndani za miradi ya maendeleo zilizokuwa zimetolewa hadi Februari 2026.
Ameeleza kuwa, kuna miradi 41, sawa na asilimia 71 ya miradi yote ambayo haikupokea hata senti moja ya fedha za ndani licha ya kuidhinishwa na Bunge.
“Ucheleweshaji wa fedha hizi unaweka hatarini utekelezaji wa miradi mikubwa ya afya nchini,” amesema Dk Zeyana.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto Dodoma, ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa pamoja na vituo vya huduma za kibingwa.
Kamati hiyo pia imeeleza changamoto ya kifedha inayokabili Bohari ya Dawa (MSD) huku Serikali ikidaiwa Sh302.2 bilioni.
Dk Zeyana amesema hali hiyo inakwamisha uwezo wa MSD kununua na kusambaza dawa kwa ufanisi na kuitaka Serikali kutoa mtaji wa haraka ili kuimarisha shughuli zake.
Dk Zeyana ameishauri Serikali kuhakikisha utekelezaji wa bajeti unafanyika kwa wakati na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kuondoa changamoto za kifedha katika sekta ya afya.
Akichangia bajeti hiyo, mbunge wa viti maalumu Neema Mgaya amesema Dira ya Taifa inaelekeza kuwa, ifikapo 2050 Tanzania inatakiwa kuwa kitovu cha tiba utalii hivyo akaomba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iendane na hospitali nyingine za kimataifa.
Neema amesema tangu mwaka 2022 hadi sasa Tanzania imepata wagonjwa 23,000.
Mbunge wa viti maalumu, Jacquline Kainja aliyezungumzia maboresho ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya huduma za wajawazito ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, ameishauri Serikali kuwa na uhusiano mzuri na sekta binafsi ili kusaidia utoaji huduma bora.
Mbunge wa Singida Mjini (CCM) Yagi Kiaratu ameitaka Serikali ikomeshe udanganyifu kwa watu wanaotumia bima za afya za watu wengine kupata matibabu.
Bunge linatarajiwa kuendelea na majadiliano ya bajeti hiyo kabla ya kuidhinisha Sh1.8 trilioni zilizoombwa na Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27.