
Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa umesitisha operesheni za kuwaokoa mabaharia waliokwama katika Mlango-Bahari wa Hormuz kufuatia shambulio dhidi ya meli ya mizigo lililotokea Alhamisi, hatua inayozidisha hofu ya kurejea kwa mkwamo wa usafirishaji katika njia hiyo muhimu zaidi za biashara ya dunia na kutishia tena soko la mafuta.
Deutsche Welle (DW) imeripoti kuwa uamuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Bahari la Umoja wa Mataifa (IMO), Arsenio Dominguez, aliyesema mazingira ya sasa hayaruhusu kuendelea kwa operesheni za uokoaji hadi tathmini mpya ya usalama itakapokamilika.
“Usalama wa mabaharia unabaki kuwa jambo la msingi. Ili kuhakikisha urambazaji unafanyika kwa usalama na kwa utaratibu, mpango wa uokoaji wa IMO utasitishwa hadi hapo ufafanuzi zaidi utakapopatikana,” amesema Dominguez.
Kwa mujibu wa DW, The New York Times, Reuters na vyombo vingine vya habari vya kimataifa kutoka nchini humo, shambulio hilo lilihusisha meli ya kubeba makontena iliyokuwa ikipita katika Mlango-Bahari wa Hormuz, eneo linalobeba sehemu kubwa ya mafuta yanayosafirishwa duniani kwa njia ya bahari.
Baada ya tukio hilo, shirika la Iran linalodai kusimamia usafiri wa baharini katika eneo hilo, PGSA, limetoa onyo kwa kampuni za usafirishaji likisema meli zote zinapaswa kutumia njia zilizoidhinishwa na mamlaka zake.
“Taarifa hii ni onyo kwa meli zote kwamba safari zitakazofanyika kupitia njia ambazo hazijaidhinishwa na PGSA hazitakuwa chini ya dhamana ya usalama,” imesema taarifa ya shirika hilo.
Rais wa Marekani, Donald Trump amelielezea shambulio hilo kuwa ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kusitisha mapigano na kusisitiza kuwa Marekani itaendelea kulinda usalama wa njia za kimataifa za usafiri wa baharini.
“Hili ni tukio la kipumbavu na ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Hatutakubali usalama wa usafiri wa baharini kuhatarishwa,” Reuters limemnukuu Trump.
Naye Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema serikali ya Marekani haitasita kujibu mashambulizi yoyote yatakayolenga meli au maslahi ya Marekani.
“Yeyote atakayetumia nguvu dhidi yetu atakutana na jibu la nguvu kutoka kwetu,” amesema Vance.
Kwa upande wa Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema litajibu kwa nguvu endapo mashambulizi dhidi ya Iran yataendelea, huku likisisitiza kuwa usalama wa Hormuz lazima uzingatie taratibu zilizowekwa na mamlaka za Iran.
“Tutatoa jibu kali kwa shambulio lolote litakalolenga Iran au maslahi yake,” imesema IRGC.
Haya yanajiri ikiwa ni siku chache tangu mwafaka wa amani katika eneo hilo kufikiwa na kurejesha matumaini ya kushuka kwa gharama za maisha zikizokuwa zimeathiriwa na vita hivyo.
Kutokana na hali hiyo, kampuni kadhaa za usafirishaji zinaripotiwa kuwa zimeanza kusitisha safari zikisubiri hali ya usalama kutengemaa.
Wachambuzi wa uchumi wanaonya kuwa iwapo tahadhari hizi zitaendelea, gharama za bima ya meli, usafirishaji wa mafuta na bidhaa nyingine zinaweza kuongezeka na hivyo kuathiri tena bei za mafuta na gharama za maisha duniani.
Hii ni kwasababu Hormuz ni njia muhimu inayopitisha karibu theluthi moja ya mafuta yote yanayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani.
Kwa sababu hiyo, tukio lolote la kiusalama katika eneo hilo hufuatiliwa kwa karibu na masoko ya kimataifa kutokana na uwezo wake wa kuathiri biashara, uchumi na mnyororo wa usambazaji wa bidhaa duniani.