Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Barnaba ameibuka gumzo kwenye tamasha la Asante Tanzania la Christian Bella baada ya kuwasha moto jukwaani kwa kuimba nyimbo mbalimbali za wasanii wengine, huku wimbo wa Kinyaunyau wa bendi ya Njenje ukiwa kivutio kikubwa kwa mashabiki waliojaa ukumbini.

Barnaba aliimba nyimbo zake tatu pekee kabla ya kuanza kuchanganya na’copy’ za nyimbo maarufu zilizowafanya mashabiki kuimba naye mwanzo hadi mwisho.

Miongoni mwa nyimbo zilizotikisa zaidi ni Kinyanyau ya bendi ya Njenje na mashabiki wengi waliinuka kwenye viti vyao wakicheza na kuimba kwa nguvu huku Barnaba akiendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa kuimba live.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kushuka jukwaani, Barnaba amesema hupendelea zaidi kuimba live kuliko kutumia flash au CD kwa sababu humfanya awe huru kubadilika kadri anavyoona mwitikio wa mashabiki.

“Mimi napenda sana kuimba live kuliko kutumia flash au CD jukwaani kwa sababu inanipa morali ya kuimba nyimbo nyingi kwa wakati mmoja,” amesema Barnaba.

Msanii huyo amesema mara nyingi hupenda kuchanganya nyimbo tofauti ili kuwapa mashabıki ladha ya aina mbalimbali za muziki na kuongeza burudani zaidi jukwaani.

“Unaweza kuimba wimbo wako mashabiki wasivutike sana, lakini ukichanganya na nyimbo nyingine au hata za kwako mwenyewe, lazima kuna chaguo lao watakalolikubali,” amesema.

Tamasha hilo la Asante Tanzania limeendelea kuacha gumzo kwa mashabiki wa muziki jijini Dar es Salaam kutokana na wasanii mbalimbali waliopanda jukwaani na kutoa burudani zilizoonyesha utofauti mkubwa wa muziki wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *