
J.D Vance, Makamu wa Rais Donald Trump wa Marekani, amedai kuwa malengo yote yaliyotangazwa na utawala wa nchi hiyo na hasa ya kijeshi na ya nyuklia katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran yamefikiwa. Vance amedai kuwa Marekani imefanikiwa kufikia yale yote iliyokuwa imepanga kuyafikia kwa kutumia uwezo wake wa kiuchumi, kidiplomasia na kijeshi.
Kuhusiana na madai hayo ni wazi kuwa makamu wa rais wa Marekani amejaribu kupunguza makali ya mashinikizo ya ukosoaji mkubwa wa ndani unaofanywa na pande mbalimbali na hata zinazouunga mkono utawala wa Trump kutokana kushindwa kwake kufikia malengo yaliyotangazwa rasmi ya kushambuliwa Iran.
Kuanzia saa za mwanzo za operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, utawala wa Trump ulifanya juhudi kubwa kubuni na kueneza simulizi bandia ya ushindi wa kihistoria dhidi ya Iran. Katika mfululizo wa hotuba zake za kitaifa na kimataifa, Trump alidai kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ulikuwa umeharibiwa kabisa, kamandi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC kulemazwa, jeshi la wanamaji la Iran kuangamizwa, jeshi lake la anga kutoweka na makombora yake ya balistiki yalikuwa yamekaribia kuharibiwa na kufutwa kabisa.
Miezi mitatu baadaye, tathmini za kijasusi za ndani ya Marekani, tathmini huru za satelaiti, data ya uchumi wa kimataifa, na tafiti za uchunguzi wa maoni ndani ya Marekani yenyewe zilitoa picha tofauti kabisa. Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya Magharibi na kimataifa, kuna sehemu sita ambapo malengo yaliyotajwa ya vita hayakufikiwa kabisa, na katika sehemu nyingine mashambulizi yalikuwa na matokeo ya kinyume yaliyohatarisha maslahi ya Marekani.
1. Kuhusu suala la nyuklia, lengo la vita lilikuwa ni eti kuizuia Iran kupata uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Trump alidai kwamba vituo vya nyuklia vya Natanz, Fordow na Isfahan viliharibiwa kabisa katika mashambulizi ya awali. Lakini tathmini za mashirika ya ujasusi ya Marekani na ripoti za setilaiti ziligundua kuwa uharibifu ulikuwa mdogo mno na kuwa ulifanyika kimsingi katika sehemu za kuingia kwenye vituo hivyo. Sehemu muhimu za chini ya ardhi na mitambo ya kisasa ya kusukuma maji haikuharibika kwa kiasi kikubwa. JD Vance mwenyewe alikiri hadharani wakati huo kwamba Washington haijui eneo sahihi ilikofichwa akiba ya urani iliyorutubishwa.
2. Hormuz: Silaha ya Kiuchumi Iliyokabidhiwa Iran kwa mikono miwili
Makosa makubwa zaidi ya kimkakati yaliyofanywa na Marekani katika vita hivi, kwa mujibu wa Ali Vaez, Mkurugenzi wa Mradi wa Iran katika Kundi la Kimataifa la Migogoro, ni kuikabidhi Tehran kile alichokielezea kama “silaha ya kiuchumi ya maangamizi ya umati.” Tangu vilipoanza vita, Iran imekuwa ikidhibiti kikamilifu Lango-Bahari la Hormuz na kusimamia safari za meli katika lango hilo kwa masharti yake. Hata baada ya kusitishwa mapigano, usafiri wa meli unaendelea chini ya masharti makali ya Iran na kwa gharama za ziada kwa mashirika ya meli. Tumeshuhudia sote namna kufungwa lango hilo kumekuwa na taathira za moja kwa moja kwa bei ya nishati ya ulimwenguni.
3. Mshtuko wa Kiuchumi kwa Marekani na Dunia
Vita vilikuwa na taathira hasi za moja kwa moja na za haraka kwa familia za Marekani. Bei ya mafuta yasiyosafishwa ilipanda kutoka karibu dola 67 hadi zaidi ya dola 120, ongezeko la hadi asilimia 80. Bei ya tiketi za ndege ilipanda kwa karibu asilimia 20. Mfumuko wa bei katika mnyororo wa usambazaji wa nishati ulizidisha mashinikizo dhidi ya familia nyingi katika pembe tofauti za dunia.
Suala hili bila shaka lilikuwa na taathira mbaya sana za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa Trump, ambaye awali alijigamba kwamba alikuwa amefanikiwa kurejesha bei ya mafuta chini ya dola tatu kama mafanikio ya kiuchumi kabla ya vita.
4. Mvutano wa Kisiasa
Vita haraka vikawa mgogoro wa kisiasa wa ndani. Kura ya maoni ya Reuters/Ipsos kuanzia Aprili 2026 iliweka ukadiriaji wa uungwaji mkono kwa Trump kuwa asilimia 34 hadi 36. Ni asilimia 34 pekee ya Wamarekani ndio waliunga mkono uamuzi wa kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Uungaji mkono wa kiuchumi wa Trump uliporomoka hadi takriban asilimia 23 hadi 25. Wengi wa wapiga kura, walitathmini vita hivyo kama “uamuzi mbaya” ambao haungefikia malengo ya vita.
5. Mgongano wa Simulizi
Al Jazeera na vyombo vingine vya habari viliakisi pakubwa pengo kubwa lililokuwepo kati ya madai ya ushindi ya Trump na ukweli wa mambo katika uwanja wa vita. Wakati Trump anazungumzia “ushindi kamili” na “mapatano yanayokaribia,” muundo wa mamlaka ya Iran ulibakia madhubuti, urutubishaji urani uliendelea, utaratibu mpya ulibuniwa katika Lango Bahari la Hormuz, na hifadhi ya urani haikuwa imekabidhiwa. Mkanganyiko huo uliharibu sana itibari ya Trump kuhusu vita.
6. Sauti za Ndani
Wachambuzi wa Marekani waliashiria moja kwa moja kushindwa Trump katika medani ya vita. New York Times na waandishi wa habari wa CNN waliripoti kuwa tangu mwanzo, utawala wa Trump haukuwa na mkakati wa wazi wa kujinasua kwenye vita au kudhibiti taathira zake za kiuchumi. Wataalamu wa kijeshi walitathmini uthabiti wa Iran, uendeshaji wake mzuri wa vita visivyo wa uwiano, na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa mfumo wa Kiislamu kuwa jambo ambalo halikutarajiwa na utawala wa Trump na hasa Pentagon.
Hitimisho
Sababu tatu kuu zilizotumika kuhalalisha vita, yaani kuharibu mpango wa nyuklia wa Iran, kuharibu makombora yake ya masafa marefu na kubadilisha mfumo unaotawala nchini, zote hazijafikiwa au zimekuwa na matokeo kinyume na ilivyokusudiwa. Iran, licha ya kupata hasara, lakini ilionyesha mapambano ya kijasiri, ikazalisha nyenzo mpya, na kuikatisha tamaa Marekani katika takriban kila uwanja. Wakati huo huo Marekani ililipa hasara kubwa za kijeshi, kiuchumi na kisiasa, huku washindani wake wakuu kimataifa Russia na China wakitumia mgogoro huo kujimarisha zaidi.