Kibaha. Siku sita baada ya kutokea kwa vurugu katika eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani zilizosababisha vifo vya watu wanne, Serikali imeanza kufanya tathimini ya uharibifu huku wananchi walioathirika wakisema bado hawajui hatima yao.

Vurugu hizo zilizotokea alfajiri ya Mei 6, 2026 zilitokana na mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wakazi wa eneo hilo na familia ya Juma Ngololo inayodaiwa kuwa mmiliki halali wa maeneo hayo.

Mapigano hayo yaliwahusisha wananchi na watu waliotajwa kuwa mabaunsa waliodaiwa kupelekwa na Ngololo ili kubomoa nyumba zilizojengwa eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 12, 2026 Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Vikawe, Shaban Ally Shaban amesema tangu kutokea kwa vurugu hizo Mei 6, 2026 wananchi wake bado wapo kwenye njia panda juu ya hatima ya mgogoro huo.

“Leo (Mei 12, 2026) wamekuja maofisa wa Halmashauri na kufanya tathimini ya uharibifu uliotokana na vurugu, baada ya hapo wananchi hawajapewa taarifa yoyote kuhusu hatua zinazofuata.

“Wananchi wapo njia panda, watu walikuja wakafanya tathimini na kuondoka, lakini hadi sasa hakuna anayejua nini kinaendelea kuhusu mgogoro huu wala hatima ya waliopoteza makazi yao,” amesema.

Katika vurugu hizo, watu wanne waliotajwa kuwa mabaunsa walifariki dunia, watatu wakipoteza maisha eneo la tukio huku mmoja akifariki hospitalini baada ya kujeruhiwa.

Mbali na vifo, wananchi walijeruhiwa, nyumba ziliharibiwa, huku eneo hilo likiendelea kuzungukwa na polisi wenye silaha na mabomu ya machozi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John (Niki wa Pili) aliiambia Mwananchi kwamba Serikali ya wilaya ilijaribu kusuluhisha mgogoro huo uliokuwepo baada ya kutokea uvamizi, ambapo wenye maeneo 121 waliridhia wavamizi wawalipe isipokuwa familia ya Ngololo.

Alisema kabla ya vurugu hizo kulikuwa na mchakato wa maridhiano kati ya wananchi waliokuwa wamejenga eneo hilo (wavamizi) na baadhi ya wamiliki halali, ambapo walikubali kuwa waliuziwa maeneo hayo kwa utapeli na wapo tayari kuyalipia upya kwa gharama ya Sh3,000 hadi Sh3,500 kwa kila mita ya mraba.

“Familia ya Ngololo haikukubaliana na maridhiano hayo na badala yake ilitaka suala hilo liamuliwe mahakamani, hivyo mgogoro wa ardhi uliopo eneo hilo utamalizwa na mahakama, kuhusu vurugu zilizotokea tayari mtuhumiwa amekamatwa kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Akizungumzia hali ya waathirika, Mwenyekiti Shaban amesema familia 10 zilizopoteza makazi zimehifadhiwa kwenye mapagale huku zikisaidiwa chakula kupitia michango ya wadau mbalimbali akibainisha kwamba katika mgogoro huo, hakuna mkazi wa Vikawe aliyepoteza maisha.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 12, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema majeruhi wanaendelea na matibabu.

Kuhusu mtuhumiwa amesema uchunguzi bado unaendelea ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *