
Ripoti ya kwanza ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, kuhusu mwelekeo wa elimu ya juu duniani inaonesha kuwa idadi ya wanafunzi waliojiandikisha imeongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, kutoka takriban wanafunzi milioni 100 mwaka 2000 hadi kufikia wanafunzi milioni 269 mwaka 2024.
Ripoti hiyo iliyotolewa leo Mei 12, 2026, inaeleza kuwa idadi ya wanafunzi wanaosoma nje ya nchi zao pia imeongezeka mara tatu, huku kukiwa na wanafunzi milioni 7.3 wanaosoma ughaibuni, ambapo nusu yao wapo katika nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Khaled El-Enany amesema,“Ripoti hii mpya inaonesha ongezeko la mahitaji ya elimu ya juu, ambayo ina jukumu lisiloweza kubadilishwa katika kujenga jamii endelevu.”
El-Enany ameongeza kuwa, licha ya ongezeko kubwa, fursa hizo bado hazijawa sawa kwa wote. “Si kila wakati upanuzi huu humaanisha uwepo wa fursa sawa kwa wote, jambo linalodhihirisha uhitaji wa mifumo mipya ya ufadhili ili kutoa elimu ya juu yenye ubora na inayojumuisha kila mtu.”
Tofauti kubwa za kikanda na changamoto ya gharama
Takwimu kutoka nchi 146 zinaonesha kuwa ingawa asilimia 43 ya watu wenye umri wa kwenda chuo (miaka 18-24) wamejiandikisha duniani kote, kuna tofauti kubwa sana kati ya kanda na kanda. Katika nchi za Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini, asilimia 80 ya vijana wamejiandikisha kwenye elimu ya juu, ikilinganishwa na asilimia 9 tu katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Aidha, taasisi binafsi bado zinachukua theluthi moja ya wanafunzi wote duniani, huku nchi kama Brazil, Japan, na Korea Kusini zikiwa na wanafunzi wanne kati ya kila watano wanaosoma kwenye vyuo binafsi.
“Kuhitimu masomo hakujaongezeka kwa kasi sawa na kujiandikisha, huku uwiano wa kimataifa wa wanaohitimu ukiongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2013 hadi asilimia 27 pekee mwaka 2024,” inafafanua ripoti hiyo. Hali kadhalika, ni theluthi moja tu ya nchi duniani ambazo zimeweka sheria ya kutotoza ada katika vyuo vikuu vya umma.
Usawa wa kijinsia na fursa kwa wakimbizi
Kwa upande wa usawa wa kijinsia, wanawake sasa wamewazidi wanaume katika elimu ya juu, ambapo kwa kila wanaume 100 kuna wanawake 114 waliojiandikisha mwaka 2024. Hata hivyo, wanawake bado wako nyuma katika ngazi ya udaktari (PhD) na wanashikilia robo moja tu ya nafasi za uongozi wa juu katika taaluma. UNESCO pia imepiga hatua katika kuwasaidia wakimbizi, ambapo idadi ya wakimbizi waliojiandikisha imeongezeka kutoka asilimia 1 mwaka 2019 hadi asilimia 9 mwaka 2025 kupitia mfumo wa “Pasi ya Sifa” (Qualifications Passport).
Kupitia mpango huo ambao sasa unatekelezwa katika nchi za Kenya, Uganda, na Zambia, UNESCO inawasaidia watu walioyahama makazi yao kutambuliwa sifa zao za kitaaluma hata kama hawana nyaraka.
Kuhusu ufadhili, uwekezaji wa serikali katika elimu ya juu unafikia wastani wa asilimia 0.8 tu ya Pato la Taifa (GDP) duniani kote, jambo ambalo linaweka shinikizo kubwa kwa vyuo vikuu huku teknolojia ya akili mnemba (AI) ikianza kubadilisha ufundishaji, ingawa ni chuo 1 tu kati ya 5 kilichokuwa na sera rasmi ya AI kufikia mwaka 2025.