Video iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO inaanzia katika wilaya ya Comoé nchini Côte d’Ivoire unaonekana msitu mkubwa na katika mstu huo mkulima mwanamke Nicole Kambou, mwenye umri wa miaka 36 akiwa na mumewe Ouattara Seydou wakifanya kazi katika shamba lao la kakao.

Baada ya miaka mingi ya ukataji miti kiholelaholela na ukame kuathiri ardhi na uzalishaji, sasa wakulima hawa wanashuhudia mabadiliko chanya kupitia upanzi wa miti unaosaidia kurejesha rutuba ya udongo na kuhifadhi unyevunyevu. 

Nicole Kambou, ambaye ni mama wa watoto wanne, akiwa amesimama mbele ya shamba lake la kakao kwa furaha anasema,

“Hali ya hewa na mazingira yamebadilika baada ya kupanda miti. Sasa jua si kali sana na udongo una rutuba, tofauti na hapo awali ulikuwa mkavu. Shukrani kwa miti ambayo tumepanda, udongo una rutuba nyingi sasa.”

© Unsplash/Etty Fidele Kukausha maharage ya kakao kabla ya kusagwa nchini Côte d’Ivoire.

Takribani kilomita 100 kutoka hapo, katika eneo la Agboville, kusini mashariki mwa nchi, mkulima Landry Ohomon anaokota na kukata matunda ya kakao ya rangi ya njano ishara kuwa yako tayari kuvunwa. Bwana Landry anasema ameshuhudia mafanikio baada ya kuhamia katika kilimo mseto cha misituni. Anasema uzalishaji wake umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Uzalishaji umeongezeka. Nimekuwa na mavuno mazuri sana baada ya kutekelezwa kwa kilimo hiki mseto. Hapo awali, nilikuwa nikizalisha takriban kilo 400 hadi 900 za kakao kwa mwaka. Mwaka jana, nilizalisha zaidi ya kilo 2,500, hivyo ninakumbatia kilimo mseto katika shamba langu.”

Afisa wa kiufundi wa FAO, Zana Ouattara, akionesha aina ya miti mpya iliyopandwa katika shamba la mkulima mmoja, anaeleza kuwa mbinu hii inasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi huku ikiimarisha uzalishaji.

“Miti hii miwili ambayo ni mti huu wa kakao na mti huu wa kivuli, unajumuisha maono yetu kwa mustakabali wa uzalishaji wa kakao nchini Côte d’Ivoire. Kabla ya FAO kuingilia kati, mti huu wa kakao ulikuwa kwenye jua. Lakini kwa kupanda mti huu wa kivuli, chini ya miaka mitatu tunaweza kuona kwamba unatoa kivuli kwa kakao, tunaona kwamba mavuno ya mti wa kakao yameongezeka. kuna maganda zaidi kwenye mti huu wa kakao, ambayo hufaidika kutokana na kivuli kinachotolewa na mti mpya uliopandwa. Hii ina maana kwamba upanzi wa miti ni suluhisho kwa wakulima wetu wa kakao katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi..”

Kupitia miradi hii ya FAO inayofadhiliwa na wadau kama Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF), zaidi ya wakulima 200,000 sasa wanafaidika na mbinu hizi endelevu. Mwakilishi wa FAO nchini humo, Joseph Nyemah, anasisitiza umuhimu wa misitu katika uzalishaji wa kakao.

“Kila mtu sasa anajua kwamba kama unataka kuendeleza uzalishaji wa kakao, kama unataka kuvuna mazao mengi ya kakao yenye ubora, unahitaji kuwa na misitu katika mazingira, na mashambani.”

Katika video hii ya FAO wakulima wanaonekana wakichakata na kukausha kakao na kusindika kwenye magunia, huku lori zikihamisha magunia mengi yaliyojaa kakao ghafi na kuzipanga kwenye chumba cha kuhifadhi. Licha ya ongezeko la uzalishaji, changamoto inasalia kuwa wakulima wanakabiliwa na tatizo la kushuka kwa bei ya kakao, jambo linaloweza kupunguza hamasa ya uzalishaji. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *