
Msemaji huyo La Niece Collins ametangaza kuwa Ofisi ya Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imepokea ombi jingine la kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Na mgombea huyo wa hivi karibuni kujiunga katika kinyang’anyiro hicho ni aliyekuwa rais wa mkutano wa 73 wa Baraza hilo na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Ecuador, María Fernanda Espinosa.
Mwanamke wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na Karibea
Collins amesema kuwa ombi la María Fernanda Espinosa lilipokelewa alasiri ya tarehe 11 mwezi Mei jijini New York, Marekani, pamoja na tamko la maono kuhusu mpango wa kazi, wasifu wa mgombea na tamko kuhusu ufadhili wa kampeni.
Pamoja na kuwa Waziri wa zamani wa Ulinzi wa nchi yake, pia aliwahi kushika Wizara ya Utamaduni na Urithi. Mwaka 2018, María Fernanda Espinosa alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na Karibea, na wa nne katika historia ya Umoja wa Mataifa kushika nafasi ya rais wa Baraza Kuu, ambapo alihudumu kwa mwaka mmoja ambacho ndicho kipindi kinachotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Hadi mwezi uliopita, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la GWL, Global Women Leaders, ambalo linawakutanisha marais wa zamani wa nchi na serikali pamoja na viongozi wengine wa kimataifa kwa ajili ya kuhamasisha wanawake zaidi kushika nyadhifa za kisiasa na maamuzi.
Wagombea watatu wanawake na wawili wanaume
Jina la Espinosa liliwasilishwa na Antigua na Barbuda.
Hadi sasa, orodha ya wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inajumuisha wanawake watatu, kwa mpangilio wa kuwasilisha maombi yao: Michelle Bachelet, akiungwa mkono na Brazil na Mexico; Rebeca Grynspan, aliyependekezwa na Costa Rica; na María Fernanda Espinosa, akiungwa mkono na Antigua na Barbuda.
Wagombea wawili wanaume ni Rafael Mariano Grossi, aliyependekezwa na Argentina, na Macky Sall, akiungwa mkono na Burundi.
Soma hapa kufahamu kwa kina waliokuwa wameshatangaza nia zao.
Uchaguzi wa Katibu Mkuu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huchaguliwa na Baraza Kuu baada ya kupendekezwa na Baraza la Usalama kwa muhula wa miaka mitano wenye uwezekano wa kuchaguliwa tena.
Kiongozi wa sasa, António Guterres, ataondoka madarakani tarehe 31 Desemba mwaka huu baada ya kuhudumu mihula miwili mfululizo.