
Katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu, uchafuzi wa mazingira na ushindani wa kiuchumi, Tanzania haiwezi kufikia Dira ya Taifa ya 2050 bila kuwaandaa na kuwawezesha vijana wataalamu wa mazingira kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa. Leo hii, taaluma ya mazingira si jambo la pembeni tena, bali ni mhimili muhimu wa uchumi, afya, uwekezaji na maendeleo endelevu.
Tanzania ina hazina kubwa ya vijana. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, nchi ina zaidi ya watu milioni 61, zaidi ya asilimia 60 ni vijana wenye umri chini ya miaka 35. Hii ni fursa muhimu kwa taifa kuwa na nguvu kazi yenye maarifa mapya, matumizi ya teknolojia za kisasa na uwezo wa kuleta ubunifu katika kutatua changamoto za mazingira zinazoongezeka kila siku.
Kadri Tanzania inavyoendelea kuelekea uchumi wa viwanda na ukuaji wa miji, changamoto za mazingira nazo zinaongezeka kwa kasi. Takribani asilimia 38 ya Watanzania sasa wanaishi mijini kutokana na kasi ya ukuaji wa miji. Hali hii imeongeza mahitaji ya nishati, maji, makazi, usafiri na huduma nyingine za msingi.
Bila wataalamu wa mazingira wenye uwezo wa kupanga na kusimamia maendeleo haya kwa misingi ya uendelevu, taifa linaweza kujikuta likibeba gharama kubwa za kiuchumi na kijamii katika miaka ijayo.
Ripoti za taasisi mbalimbali za kimataifa zinaonyesha kuwa nchi nyingi za Afrika hupoteza kati ya asilimia 3 hadi 5 ya pato la taifa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Tanzania imeendelea kushuhudia athari za ukame, mafuriko, mmomonyoko wa ardhi, kupungua kwa vyanzo vya maji na ukataji wa misitu. Benki ya Dunia imeeleza kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya hekta 480,000 za misitu kila mwaka, jambo linaloathiri sekta za kilimo, utalii, nishati na afya za wananchi.
Katika mazingira hayo, vijana wataalamu wa mazingira wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si watazamaji. Kupitia elimu ya kisasa katika maeneo kama ukaguzi wa mazingira, tathmini za athari za mazingira na kijamii, nishati jadidifu, uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, miundombinu ya kijani na uhifadhi wa bioanuwai, vijana wanaweza kubadili changamoto kuwa fursa za maendeleo. Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya kazi za ushauri katika miradi mikubwa ya mazingira na miundombinu hutolewa kwa kampuni za kigeni. Hali hii husababisha fedha nyingi kutoka Afrika kwenda nje wakati vijana wenye uwezo wakikosa nafasi za kujifunza na kufanya kazi.
Tatizo hili halitokani na ukosefu wa vipaji vya ndani, bali linachangiwa na uwekezaji mdogo katika kukuza wataalamu vijana, mifumo dhaifu ya kuwaunganisha na miradi mikubwa, pamoja na sera zisizotoa kipaumbele kwa wataalamu wazawa.
Tanzania tayari ina wataalamu wengi wa mazingira wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi, jambo linalothibitisha kuwa vijana wa Kitanzania wana uwezo wa kushindana kimataifa wakipewa mazingira sahihi.
Uchumi wa kijani ni eneo lenye nafasi kubwa kwa vijana wataalamu wa mazingira. Dunia sasa inaelekea katika uwekezaji wa miradi inayozingatia matumizi bora ya rasilimali, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kulinda mazingira. Majengo ya kisasa yanayotumia viwango vya EDGE, kwa mfano, hupunguza matumizi ya maji, nishati na hewa chafu kwa kiwango kikubwa. Miradi kama hiyo inahitaji wataalamu wa mazingira, wahandisi, wabunifu na wasimamizi wa mifumo endelevu.
Mbali na kutoa ajira, miradi ya kijani huwapa vijana nafasi ya kupata uzoefu wa vitendo, kuongeza ubunifu na kujenga ushindani katika soko la kimataifa. Tanzania ikiwekeza zaidi katika nishati jadidifu, usimamizi wa taka, majengo ya kijani na kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, inaweza kuzalisha maelfu ya ajira mpya huku ikilinda mazingira.
Aidha, ushirikiano wa kikanda ni muhimu kwa sababu changamoto za mazingira haziheshimu mipaka ya nchi. Kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, vijana wataalamu wa mazingira wanaweza kushiriki miradi ya kikanda, kubadilishana maarifa na kuongeza ushindani wao kimataifa.
Diplomasia ya mazingira nayo inapaswa kupewa uzito zaidi. Mataifa yanayotumia wataalamu wao vizuri katika majadiliano ya kimataifa kuhusu tabianchi, nishati na mazingira hupata ushawishi mkubwa pamoja na fursa za ufadhili na uwekezaji.
Tanzania inapaswa kuhakikisha vijana wataalamu wanashirikishwa katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Ili kufanikisha Dira ya Tanzania 2050, hatua madhubuti zinahitajika sasa. Serikali inapaswa kuimarisha sera za local content ili kuhakikisha wataalamu wazawa wanapata nafasi katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Sekta binafsi nayo ina jukumu muhimu la kutoa nafasi za mafunzo, ushauri wa kitaaluma na ajira kwa vijana. Vyama vya kitaaluma vinaweza kusaidia kuwaunganisha vijana, kuwajengea uwezo na kuhakikisha taaluma ya mazingira inakuwa na viwango vinavyotambulika kimataifa.
Mwandishi ni Mwanzilishi Mfawadhi, Umoja Conservation Trust (UCT)