Katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na misukosuko ya kisiasa na kiusalama, hasa kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, nchi nyingi zimeanza kutafakari upya namna ya kujilinda dhidi ya athari za kupanda kwa bei ya mafuta na changamoto za upatikanaji wa nishati muhimu kama gesi ya kupikia (LPG).

Tanzania nayo tayari imeathiriwa na kinachoendelea Mashariki ya kati bei ya mafuta na LPG vimepanda na kwa sasa hatuna budi kufanya maamuzi ya kimkakati hasa kwa kuhamia kwenye kuhamasisha miradi midogo ya gesi asilia iliyofanya kuwa kimiminika (Mini LNG) na kuongeza matumizi ya CNG ili kujenga uchumi imara na unaojitegemea.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitegemea mafuta kutoka nje ya nchi. Hali hiyo imekuwa ikiweka shinikizo kubwa kwenye matumizi ya fedha za kigeni na kuifanya Shilingi ya Tanzania kuendelea kupoteza thamani kila mara bei za mafuta duniani zinapopanda.

Vita vya Mashariki ya Kati vinaendelea kuongeza taharuki kwenye soko la mafuta duniani, jambo ambalo linaweza kusababisha gharama za usafirishaji, uzalishaji na maisha ya wananchi kuongezeka kwa kasi.

Lakini Tanzania ina bahati kubwa ya kuwa na rasilimali ya gesi asilia ambayo bado haijatumika kwa kiwango kinachostahili kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Hapa ndipo umuhimu wa miradi Mini LNG unapokuja.

Mini LNG ni mfumo wa kuchakata na kusambaza gesi asilia kwa kiwango kidogo ukilinganisha na miradi mikubwa ya LNG inayohitaji mabilioni ya dola na muda mrefu kujengwa. Miradi hii inaweza kujengwa karibu na maeneo yenye mahitaji ya nishati, viwanda au hata mikoa ambayo bado haijaunganishwa na miundombinu mikubwa ya gesi.

Faida yake kubwa ni kwamba uwekezaji wake ni mdogo na unaweza kuanza kuleta matokeo kwa haraka. Kwa wastani, mradi wa Mini LNG unaweza kuhitaji uwekezaji wa kati ya dola milioni 20 hadi dola milioni 200 kutegemea ukubwa wake, tofauti na miradi mikubwa ya LNG inayoweza kugharimu zaidi ya dola bilioni 10. Hii ina maana kuwa hata sekta binafsi ya ndani inaweza kushiriki kwa urahisi zaidi.

Nchi kadhaa tayari zimeonyesha mafanikio kupitia mtindo huu. China ni moja ya nchi zilizofanikiwa sana katika matumizi ya Mini LNG, ambapo mfumo huo umetumika kusambaza gesi kwenye maeneo ya viwanda na usafiri wa magari makubwa. Matokeo yake yamekuwa kupungua kwa utegemezi wa mafuta ya dizeli na kuboresha usalama wa nishati.

India nayo imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye LNG ndogo kwa ajili ya viwanda, usafiri wa malori na matumizi ya kupikia. Serikali ya India imeweza kuongeza matumizi ya gesi kwenye uchumi wake kwa kasi kupitia miradi inayoweza kujengwa kwa gharama nafuu na kusambazwa katika maeneo mengi.

Indonesia, ambayo ni nchi yenye mazingira yanayofanana kwa kiasi fulani na Tanzania kutokana na visiwa na umbali wa maeneo yake, imefanikiwa kutumia Mini LNG kupeleka nishati kwenye maeneo ambayo hayakuwa na umeme wa uhakika. Mfumo huo umesaidia kupunguza gharama za mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme.

Tanzania inaweza kujifunza mengi kutoka kwa mifano hiyo. Badala ya kusubiri kwa miaka mingi utekelezaji wa miradi mikubwa pekee, nchi inaweza kuanza sasa kuwekeza kwenye vituo vidogo vya LNG katika maeneo ya kimkakati kama Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza na Dodoma.

Hatua hiyo inaweza kwenda sambamba na kuongeza matumizi ya CNG kwenye magari binafsi, mabasi ya abiria na malori. Tayari Tanzania imeanza kuona mwitikio mzuri wa matumizi ya CNG, hasa Dar es Salaam, lakini bado kasi yake ni ndogo ukilinganisha na mahitaji yaliyopo.

Faida zake ni nyingi. Kwanza, CNG ni nafuu zaidi kuliko petroli na dizeli. Hii inasaidia kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi na wafanyabiashara. Pili, inapunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa kuagiza mafuta kutoka nje. Kadri nchi inavyopunguza uagizaji wa mafuta, ndivyo inavyopunguza presha kwenye dola na kusaidia kulinda thamani ya Shilingi yetu.

Lakini pia matumizi makubwa ya gesi yanaweza kufungua fursa mpya za uwekezaji na ajira. Viwanda vya vifaa vya gesi, huduma za usafirishaji, vituo vya kujazia CNG na miundombinu ya LNG vinaweza kuzalisha maelfu ya ajira mpya kwa vijana.

Kama Tanzania tutaamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Mini LNG na CNG, tunaweza kujenga uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi, kupunguza gharama za maisha, kulinda thamani ya fedha yake na kuongeza uwezo wa kujitegemea.

Ukweli unabaki kuwa Tanzania hatuwezi kuendelea kutegemea mafuta kutoka nje wakati tuna utajiri mkubwa wa gesi asilia. Dunia ya sasa inaonyesha wazi kuwa uhakika wa nishati ni sehemu ya uchumi wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *