
Dar es Salaam. Upatikanaji wa mitaji umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) nchini, jambo ambalo ni kikwazo kwa biashara nyingi zenye uwezo wa kukua licha ya kuwa na mawazo mazuri na wateja wanaoongezeka.
Kutokana na changamoto hiyo, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kuimarisha msaada kwa SMEs kupitia DSE Enterprise Acceleration Program (DEAP) pamoja na Endeleza Portal ambayo ni jukwaa la kidijitali linalounganisha biashara na watoa mitaji mbalimbali.
Mjadala kuhusu DEAP na Endeleza ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ukiongozwa na mtaalamu wa maendeleo ya biashara na uendelevu kutoka DSE, Innocent John Mbele, huku ukihusisha wataalamu wa masoko ya mitaji na maendeleo ya biashara.
Wazungumzaji walisisitiza kuwa kupata mtaji si suala la fedha pekee, bali pia biashara kuwa na mifumo bora, uwazi, utawala mzuri na maandalizi ya kuvutia wawekezaji.
Akizungumza katika mjadala huo, Mbele alisema DEAP na Endeleza zimeundwa kusaidia biashara ambazo bado hazijafikia hatua ya kuorodheshwa kwenye soko la hisa lakini zina uwezo wa kukua.
“Kupitia DEAP na Endeleza Portal, DSE inajenga daraja lenye mfumo rasmi kati ya SMEs na watoa mitaji. Lengo ni kuzisaidia biashara kujiandaa, kuonekana, na kupata aina sahihi ya mtaji kulingana na safari yao ya ukuaji,” alisema.
Alieleza kuwa kupitia DEAP, biashara hupatiwa mafunzo ya kujenga uwezo katika maeneo muhimu ikiwemo utawala bora, uandaaji wa taarifa za fedha, mkakati wa biashara, uzingatiaji wa kanuni na namna ya kupata mitaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi wa Maarifa wa FSD Tanzania, Bernie Mshana, alisema SMEs zinahitaji zaidi ya ndoto ili kuvutia mitaji.
“Ili SMEs zivutie mitaji, zinahitaji zaidi ya kuwa na ndoto au malengo. Zinahitaji kumbukumbu sahihi, mipango wazi ya ukuaji, utawala bora, na upatikanaji wa taarifa za kuaminika za soko. Majukwaa kama Endeleza yanaweza kusaidia kupunguza pengo la taarifa kati ya SMEs na watoa mitaji,” alisema.
Endeleza Portal imeelezwa kuwa jukwaa salama linaloruhusu SMEs kujisajili na kuweka taarifa zao ili kuonekana kwa wawekezaji mbalimbali wakiwemo kampuni za private equity, venture capital, taasisi za maendeleo ya fedha na watoa mitaji mbadala.
Kupitia mfumo huo, SMEs zinapata nafasi ya kuonyesha uwezo wa biashara zao huku wawekezaji wakipata urahisi wa kutambua biashara zilizo tayari kwa uwekezaji.
Katika mjadala huo Meneja Mwandamizi wa Huduma za Udalali wa Dhamana wa CRDB Bank Plc, Imani Muhingo, alisema biashara nyingi bado hazina uelewa wa kutosha kuhusu njia mbalimbali za kupata mitaji.
“Biashara nyingi hazijafahamu kikamilifu aina mbalimbali za nyenzo za ufadhili zilizopo sokoni. Zaidi ya mikopo ya kawaida ya benki, SMEs zinaweza kuchunguza ufadhili wenye muundo maalum, mitaji binafsi, hati fungani, na hatimaye fursa za masoko ya umma kulingana na hatua ya ukuaji wa biashara husika,” alisema.
Aidha, kundi la DEAP la mwaka 2026 linatarajiwa kutumia mfumo wa sekta maalumu likijikita katika madini, kilimo, fintech na mali isiyohamishika.
Katika sekta ya madini, programu hiyo itasaidia biashara kuelewa namna ya kujiandaa kwa uwekezaji na kuboresha taarifa za kifedha na kijiolojia. Kwa upande wa kilimo, msisitizo utawekwa kwenye biashara zinazohitaji mtaji wa uendeshaji na upanuzi wa shughuli zake.
Kwa sekta ya fintech, kampuni bunifu zitapatiwa msaada kuhusu utayari wa kikanuni na upanuzi wa biashara, huku sekta ya mali isiyohamishika ikisaidiwa kuelewa fursa za ufadhili kupitia masoko ya mitaji na ubia wa uwekezaji.
Mshauri Mkuu wa Africapital, Adam Mayingu, yeye alisema wawekezaji huangalia zaidi ya wazo la biashara. “Wawekezaji wanatafuta biashara zenye uwezo wa kukua, zilizopangwa vizuri, na zinazoweza kuonyesha uwezo wa ukuaji pamoja na uwajibikaji. Kwa hiyo, SMEs zinapaswa kujiandaa kabla ya kuwafuata watoa mitaji,” alisema.
Kwa mujibu wa wadau hao, mipango ya DEAP na Endeleza inaweza kusaidia kufungua mitaji kwa biashara zinazokua, kuongeza ajira na kuimarisha ushiriki wa SMEs katika uchumi huku msisitizo unaotolewa ukiwa ni kwamba kupata mtaji hakuhusu kutafuta fedha pekee, bali pia kuandaa biashara kuwa tayari kupokea uwekezaji.