USHINDI wa mabao 4-1 ambao TRA United iliupata dhidi ya Azam FC wiki iliyopita katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ndio stori kubwa hapa kijiweni leo.
Ni kipigo kikubwa sana ambacho wengi kiukweli hatukukitegemea kwa vile Azam FC ni timu kubwa kuliko TRA United na inanolewa na kocha mkubwa Florent Ibenge.
Hakuna anayeweza kubisha hoja ya kwamba Ibenge ni kocha mwenye jina kubwa na ukizingatia ana benchi pana la ufundi lenye watu wenye wasifu mzuri kulinganisha na TRA United.
Hata hivyo, baada ya kukumbuka kitu kimoja, hapa kwenye kijiwe tukakubaliana kwamba inawezekana kile kipigo kilistahili kwa Azam FC japo kilikuwa kikubwa.
Na sababu ya kukubaliana huko ni mtu mmoja tu pale TRA United anayeitwa Etienne Ndayiragije ambaye ni kocha mkuu wa hiyo timu.
Huyu ni masta hasa katika kufanya upembuzi na tathmini yakinifu juu ya ubora na udhaifu wa timu pinzani kisha akaenda katika ubao wa kuchorea na kuandaa mpango mzuri wa kukabiliana na mpinzani aliye mbele yake.
Kwa Ndayiragije huwa ni rahisi kwake kuzikabili timu kubwa kwa sababu huwa zinacheza kwa staili iliyo endelevu kulinganisha na nyingine ambazo zimekuwa zikibadilika kiuchezaji mara kwa mara.
Ndio maana katika historia yake hapa nchini, Etienne amekuwa akizisumbua timu kubwa pengine hata pale anapokutana na timu za daraja la kati au la chini.
Mfano tu ni ile fainali ya Kombe la FA pale Jamhuri Dodoma mwaka 2017 dhidi ya Simba. Kile kiwango bora cha Mbao FC katika fainali kiliwapa presha kubwa vigogo siku ile.