
Jaji wa mahakama ya shirikisho katika Wilaya ya Columbia nchini Marekani amesitisha vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Marekani dhidi ya Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maeneo ya Palestina.
Albanese alithibitisha uamuzi huo kupitia mtandao wa X akisema: “Mahakama ya Marekani imesitisha vikwazo vya Marekani dhidi yangu! Nawashukuru binti yangu na mume wangu kwa kusimama kunitetea, pamoja na kila aliyetoa msaada hadi sasa.”
Vikwazo hivyo vilikuwa vimewekwa na utawala wa Donald Trump na baadaye kutetewa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio. Albanese alilengwa kutokana na kuelezea vita vya Israel dhidi ya Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari na kuitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuanzisha uchunguzi dhidi ya maafisa wa Israel na Marekani.
Katika uamuzi wake, Jaji Richard Leon alisema hatua hizo zilikiuka haki za Albanese za uhuru wa kujieleza chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, akibainisha kuwa vikwazo hivyo vilitokana moja kwa moja na wito wake wa kuitaka ICC iwajibishe wahusika.
Jaji huyo amesema: “Albanese hajafanya chochote zaidi ya kuzungumza.”
Kwa muda mrefu Albanese amekuwa akiitaka mahakama ya ICC kuwafungulia mashitaka watu wanaohusishwa na mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Wito wake wa kutaka uwajibikaji kuhusu mauaji ya kimbari ulipata uzito zaidi baada ya ICC kutoa hati za kukamatwa mwezi Novemba 2024 dhidi ya Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita wa Israel Yoav Gallant kutokana na jinai zao huko Gaza.
Licha ya uamuzi huo wa mahakama katika kesi ya Albanese, vikwazo vya Marekani bado vinaendelea dhidi ya baadhi ya maafisa wa ICC ambao Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inawashutumu kwa kuendesha uchunguzi kuhusu jinai za Israel za mauaji ya kimbari huko Gaza pamoja na operesheni za kijeshi za Marekani ambazo zimesababisha maafa makubwa.