
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeeleza katika ripoti yake kuwa waasi wa kundi la M23 na wanajeshi wa Rwanda waliukalia kwa mabavu na kwa ukatili mji wa Uvira kwa muda wa mwezi mmoja unaopatikana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; hatua iliyoambatana na mauaji ya kiholela, ubakaji na kuwateka nyara raia.
HRW imesema katika ripoti yake ya siku ya Alhamisi kwamba mji wa Uvira ulivamiwa na kukaliwa kwa mabavu kuanzia Disemba 10 mwaka jana hadi Januari 17 mwaka huu.
HRW imesema kuwa imesajili mauaji ya kiholela zaidi ya 50, vitendo vya ubakaji visivyopungua 8 na watu 12 hawajulikani walipo hadi sasa. Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeongeza kusema: Raia wa mji wa Uvira walilengwa na ufyatuaji risasi wakati wakijaribu kukimbia.
Ripoti hii ya HRW imetolewa kwa kutegemea mahojiano zaidi ya 120 yaliyofanyika mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
Kundi hilo limebainisha kuwa kuwa waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda walikuwa wakienda nyumba hadi nyumba, wakiwalenga wanaume na wavulana wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na wanamgambo kwa jina la Wazalendo wenye mfungamano na serikali ya Kinshasa.
Mwananchi wa Kongo aliyenukuliwa na HRW katika ripoti hiyo ameeleza kuwa, watu wanne wa familia yake walipigwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka katika mji wa Uvira.