
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, ameikosoa vikali Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuwa mshirika wa moja kwa moja katika uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran. Ametoa kauli hiyo akijibu madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na mwakilishi wa UAE.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa BRICS mjini New Delhi siku ya Alhamisi, Araghchi amelaani kauli za mwakilishi wa Imarati zilizotolewa katika mkutano huo huo.
Araghchi amesema alikuwa ameamua kutolitaja jina la UAE katika hotuba yake kwa nia ya kulinda umoja na mshikamano wa BRICS lakini baadaye akaona kuna ulazima wa kuweka mambo wazi mbele ya hadhara.
Katika vita vya uchokozi vilivyoanzishwa na muungano wa kijeshi wa Marekani na Israel tarehe 28 Februari, Iran ilisema ilijibu kwa kujilinda kupitia mashambulizi mengi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maslahi ya Marekani na Israel katika eneo, hasa ndani ya nchi za Ghuba ya Uajemi ikiwemo UAE.
Waziri huyo wa Iran amesema kuwa uchokozi huo ulipoanza, UAE ilikataa hata kulaani mashambulizi hayo.
Araghchi amesema: “Hawakukemea shambulio la kikatili dhidi ya shule katika siku ya kwanza kabisa ya uchokozi huo , shambulio lililosababisha kuuawa kwa zaidi ya wanafunzi 170 wasio na hatia.”
Aliongeza kuwa mbali na kushindwa kulaani uchokozi huo, UAE baadaye ilishiriki kikamilifu kwa kuruhusu kambi za kijeshi, anga, ardhi na miundombinu yake kutumiwa na Marekani pamoja na Israel katika hujuma dhidi ya watu wa Iran.
Akimhutubu moja kwa moja mwakilishi wa UAE katika kikao hicho, aliuliza:
“Mwakilishi wa UAE anazungumzia sheria za kimataifa , basi na atuambie ni sehemu gani ya sheria za kimataifa inayoruhusu kuunga mkono uchokozi usio na sababu wala uhalali?”
Hata hivyo, Araghchi alisisitiza kuwa Iran haikuilenga UAE yenyewe kwa kufafanua kuwa Iran ililenga tu vituo vya kijeshi vya Marekani na miundombinu ya kijeshi ya Marekani ndani ya UAE.”
Araghchi amesema alitaka kutoa “ushauri wa kindugu kwa marafiki wa Imarati”, akisema kuwa uwepo wa majeshi na vituo vya Marekani katika ardhi yao haukuwaletea usalama walioutarajia.
Akizungumza tena moja kwa moja na afisa wa UAE, alisema:
“Kama mnataka Israel iwape usalama, haya ndiyo matokeo yake. Kama mnataka Marekani iwape usalama, haya ndiyo matokeo mnayoyalalamikia leo.”
Araghchi amesema pia kuwa hivi karibuni imefichuliwa kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa ametembelea UAE na Abu Dhabi wakati wa vita hivyo.
Amesisitiza kuwa kuna ushahidi mkubwa unaoonyesha UAE iliruhusu vituo vyake vya kijeshi kutumiwa na Marekani kushambulia Iran.
Mwisho, Araghchi alizitaka nchi nyingine wanachama wa BRICS kwamba ikiwa wanataka kuchukua msimamo wa haki na usawa, basi uchokozi wa Marekani, Israel na UAE dhidi ya Iran unapaswa kulaaniwa waziwazi.