Uwanja Majengo Moshi kujengwa kwa Sh2.1 bilioniUwanja Majengo Moshi kujengwa kwa Sh2.1 bilioni

Moshi. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imesaini mkataba na Kampuni ya Sibstone Limited wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Majengo utakaogharimu Sh2.1 bilioni.

Mradi huo wa ujenzi unaotarajiwa kubadili taswira ya soka Kilimanjaro, ulisainiwa jana Ijumaa, Mei 15, 2026 na Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo na m Mkandarasi wa kampuni ya Sibstone Company Limited, Joseph Mrema.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika ofisi za manispaa hiyo, Moshi Mjini, Kidumo amesema serikali ya manispaa imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kabla ya kuanza kwa mashindano ya AFCON 2026.

“Hatujawahi kukwama tangu tuanze kuupanga upya mradi huu. Kusudio letu kubwa ni kuona uwanja unakamilika kabla ya AFCON, kwa sababu ukikamilika baadaye hautakuwa na maana sawa na kukamilika kwa wakati,” amesema Kidumo.

Mkandarasi wa mradi huo, Joseph Mrema, ameahidi kukamilisha kazi ndani ya muda wa mkataba huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wadau wote.

“Sisi ni watu wa vitendo, tutahakikisha tunakamilisha kazi kwa wakati na ubora unaotakiwa,” amesema.

Ofisa Habari wa timu ya Polisi Tanzania, Mkaguzi wa Polisi, Frank Lukwaro amesema kukamilika kwa uwanja wa Majengo kutakuwa mkombozi mkubwa kwa timu hiyo.

“Kwanza ni fursa kubwa. Tunapongeza hatua hii ya kuboresha uwanja wa Majengo, utakuwa na manufaa makubwa kwa soka la Kilimanjaro,” amesema Lukwaro.

Amesema mara kadhaa timu hiyo imekuwa ikikosa uwanja wa uhakika wa mechi na mazoezi, hasa pale Uwanja wa Ushirika unapokuwa na matumizi mengine, hivyo uwanja mpya utatoa suluhisho la kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *