Hivi ndivyo muda wa mapumziko ulivyo muhimu kwa wanafunzi shuleniHivi ndivyo muda wa mapumziko ulivyo muhimu kwa wanafunzi shuleni

Dar es Salaam. Mwelekeo wa shule nyingi kuongeza muda wa vipindi vya masomo na kupunguza muda wa mapumziko umeanza kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wataalamu wa afya na elimu duniani, wakionya kuwa hali hiyo inaweza kuathiri maendeleo ya watoto kiakili, kimwili na kijamii.

Onyo hilo limekuja baada ya Jumuiya ya Madaktari Bingwa wa Watoto Marekani (AAP) kutoa mwongozo mpya unaosisitiza kuwa mapumziko shuleni si muda wa starehe pekee, bali ni sehemu muhimu inayochangia afya bora, ustawi wa akili na hata ufaulu wa wanafunzi.

Mwongozo huo, ambao umetolewa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 13, umebainisha kuwa watoto wanaohudhuria vipindi vya masomo kwa muda mrefu bila kupumzika hupoteza uwezo wa kuzingatia wanachofundishwa na kushindwa kuhifadhi vizuri taarifa wanazojifunza.

Kwa mujibu wa AAP, watoto wanapaswa kupata angalau dakika 20 za mapumziko kila siku, pamoja na vipindi vya kupumzika kati ya masomo ili kuwasaidia kurejesha nguvu za akili na mwili.

Akizungumzia na Mwananchi, mtaalamu wa saikolojia ya watoto wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Anna Mrema, anasema ubongo wa mtoto hauwezi kufanya kazi kwa ufanisi kwa muda mrefu bila kupata nafasi ya kupumzika.

“Watoto wanahitaji muda wa kucheza na kuondoa mawazo ya darasani ili waweze kurejea kwenye masomo wakiwa na umakini zaidi. Bila kufanya hivyo, hata uwezo wa kuelewa hupungua,” anasema Anna.

Anasema watoto wengi wanaochoshwa na ratiba ndefu za masomo huonesha dalili za kukata tamaa, hasira na kushindwa kushirikiana vizuri na wenzao.

Kwa upande wake, mtaalamu wa elimu, Elinaza Msuya, anasema shule nyingi zimeweka mkazo mkubwa kwenye matokeo ya mitihani huku zikisahau umuhimu wa maendeleo ya jumla ya mtoto.

“Mtoto hawezi kuendelezwa kwa vitabu pekee. Michezo na mapumziko humjengea uwezo wa kuwasiliana, kujiamini na kufikiri kwa ubunifu,” anasema.

Kwa mujibu wa Msuya, watoto wanaopata muda wa kushirikiana na wenzao wakati wa mapumziko hujifunza pia namna ya kutatua migogoro na kufanya kazi kwa pamoja.

Akizungumzia mchango wa mapumziko kiafya, daktari bingwa wa watoto, Neema Chuwa, anasema mapumziko yana mchango mkubwa katika kuzuia tatizo la unene kupita kiasi ambalo limeendelea kuongezeka miongoni mwa watoto duniani.

Anasema watoto wengi wa sasa hutumia muda mwingi kwenye simu na vifaa vya kidijitali, hali inayopunguza shughuli za mwili.

“Mapumziko ya shule yanakuwa nafasi muhimu kwa watoto kufanya mazoezi na kuimarisha afya zao. Mtoto anayekimbia, kucheza na kushiriki michezo hupata afya bora zaidi,” anasema Dk Chuwa.

Takwimu za AAP zinaonesha mtoto mmoja kati ya watano nchini Marekani anakabiliwa na tatizo la unene uliopitiliza.

Dk Chuwa anasema hali kama hiyo inaanza kuonekana hata katika nchi nyingi zinazoendelea kutokana na watoto kutumia muda mwingi ndani ya nyumba na kupungua kwa michezo ya nje.

Anasema watoto wanaoshiriki michezo wakati wa mapumziko hupata afya bora ya moyo, mifupa imara na usingizi mzuri.

Akizungumzia upande wa malezi, mtaalamu wa malezi ya watoto, Rehema Mwakalinga, anasema muda wa mapumziko husaidia watoto kujifunza mambo mengi ya kijamii ambayo hayawezi kufundishwa darasani.

Anasema wakati wa kucheza watoto hujifunza kushirikiana, kutatua migogoro, kuheshimu wenzao na kufanya maamuzi.

Mtaalamu huyo anafafanua kuwa hata uwezo wa kuongoza huanza kujengwa kupitia michezo na mawasiliano ya kawaida ya watoto wakiwa mapumzikoni.

“Watoto hujifunza kushirikiana, kuheshimu wenzao, kuomba msamaha na hata kuongoza kupitia michezo ya kawaida wanapokuwa mapumzikoni.

“Hata uwezo wa kuongoza huanza kujengwa kupitia michezo na mawasiliano ya kawaida ya watoto wakiwa mapumzikoni,” anasema Rehema.

Anaongeza kuwa watoto wanaokosa nafasi za kucheza na kuwasiliana na wenzao huweza kuwa na changamoto za kujiamini wanapokuwa wakubwa.

Wasemavyo walimu

Baadhi ya walimu waliozungumza na Mwananchi wanaeleza kuwa wanafunzi wanaopata muda wa kutosha wa kupumzika huwa watulivu zaidi darasani na wenye uwezo mkubwa wa kushiriki masomo.

Stella Mallya, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, anasema watoto wanaokaa muda mrefu darasani bila mapumziko huanza kuchoka na kupoteza hamasa ya kujifunza.

“Unaweza kuona kabisa tofauti. Wanafunzi wakitoka mapumzikoni huwa wachangamfu na tayari kushiriki vipindi. Wakikosa muda huo, wengi huanza kulala au kukosa umakini,” anasema Mallya.

Kwa upande wake, mwalimu wa sekondari, Joseph Mwakipesile, anasema baadhi ya shule zimekuwa zikiona mapumziko kama muda wa kupoteza, jambo ambalo si sahihi.

“Mapumziko si adui wa elimu. Ni sehemu ya elimu yenyewe kwa sababu yanamsaidia mwanafunzi kuwa tayari kujifunza vizuri zaidi,” anasema.

Naye mwalimu wa michezo, Asha Hamisi, anasema michezo ya wakati wa mapumziko huwasaidia wanafunzi kujenga afya na nidhamu.

“Watoto wanapocheza pamoja hujifunza kufuata sheria, kushindana kwa haki na kuheshimiana. Hayo yote ni mafunzo muhimu katika maisha yao,” anasema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Mtoto Dignity, Loyce Mhando, anasema shule zinapaswa kuweka mazingira yanayolinda muda wa mapumziko kwa wanafunzi kwa kuwa watoto wana haki ya kucheza na kupumzika kama sehemu ya ukuaji wao.

“Tunapaswa kuelewa kuwa mtoto anayefurahia mazingira ya shule huwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi kitaaluma na kijamii,” anasema Mhando.

Adhabu ya kunyimwa mapumziko

Katika baadhi ya shule, wanafunzi wanaochelewa kazi, kufanya makosa au kuwa na utovu wa nidhamu huadhibiwa kwa kunyimwa muda wa mapumziko.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza matatizo badala ya kuyatatua.

Akizungumzia hilo, mshauri wa afya ya akili kwa vijana, Hassan Mbise, anasema wanafunzi wenye changamoto za kitabia ndiyo wanaohitaji zaidi muda wa kupumzika.

“Ukimnyima mtoto mapumziko kwa sababu ana fujo au hana utulivu, unakuwa umeondoa nafasi yake ya kupunguza msongo na kurejesha utulivu wa akili,” anasema.

Mbise anasema watoto wengi wenye matatizo ya kitabia huwa wanahitaji shughuli za mwili ili kupunguza nguvu nyingi walizonazo.

Anasema kuwafanya wakae muda mrefu darasani bila mapumziko kunaweza kuongeza uchovu wa akili na kuwafanya wawe wakorofi zaidi.

“Wanafunzi wenye changamoto za kitabia ndiyo wanaohitaji zaidi muda wa kucheza na kupunguza msongo wa akili. Kuwazuia mapumziko kunaweza kuongeza matatizo yao,” anasema.

Anasema watoto wengi hupunguza msongo na uchovu wa akili kupitia michezo na shughuli za mwili, hivyo kuwafanya wakae muda mrefu darasani bila kupumzika kunaweza kuathiri afya zao za akili.

Nchi za Japan, Denmark na Uingereza zimeendelea kuweka mfumo wa wanafunzi kupata mapumziko kila dakika 45 hadi 50 za vipindi vya masomo.

Wataalamu wanaamini mfumo huo huwasaidia wanafunzi kurejesha umakini, kupunguza uchovu na kuongeza uwezo wa kujifunza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *