
Njombe. Wauguzi wilayani Ludewa mkoani Njombe wamehimizwa kufanya kazi kwa kujitolea na kudumu katika vituo vyao vya kazi, badala ya kuomba uhamisho mara kwa mara, hali inayodaiwa kuathiri utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Wito huo umetolewa leo, Mei 16, 2026 na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Oscar Simtengu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi yaliyofanyika wilayani humo.
Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu “Wauguzi wetu, mustakabali wetu; wauguzi waliowezeshwa huokoa maisha.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Simtengu amesema Wilaya ya Ludewa imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya watumishi kuhama mara kwa mara, hasa katika kada ya afya, jambo linalochangia upungufu wa watumishi na kuathiri huduma kwa wananchi.
“Wilaya ya Ludewa inakabiliwa na changamoto ya watumishi kuhama mara kwa mara, hasa kada ya afya, hali inayosababisha ugumu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” amesema Simtengu.
Amesema pamoja na changamoto hizo, wauguzi wanapaswa kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa upendo, huruma na uvumilivu, kwa kuwa huduma ya afya inahitaji utu na moyo wa kujitolea.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Wise Mgina, amesema taaluma ya uuguzi ni miongoni mwa kazi zenye heshima kubwa kutokana na nafasi yake katika kuokoa maisha ya watu.
Amesema ni muhimu wauguzi kuendelea kuthaminiwa na kupewa motisha ili kuongeza ari ya kazi na kuwafanya waendelee kutoa huduma kwa kujituma.
“Uuguzi si kazi rahisi, ni taaluma inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hivyo ni lazima wauguzi wawezeshwe na kuthaminiwa,” amesema Mgina.
Naye Katibu wa Afya Wilaya ya Ludewa, Emmanuel Mushi, aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Twilumba Lihweuli, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya afya wilayani humo.
Amesema maboresho hayo yanahusisha ujenzi wa majengo mapya ya hospitali pamoja na wodi za kulaza wagonjwa, hatua inayosaidia kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuajiri watumishi wapya wa afya na kuboresha mazingira ya utoaji huduma,” amesema Mushi.
Awali akisoma risala ya wauguzi, Katibu wa Tanzania National Nurses Association Wilaya ya Ludewa, Gift Hingi, amesema ajira mpya za wauguzi zilizotolewa na Serikali zimepunguza changamoto ya upungufu wa watumishi katika vituo vya afya.
Amesema hatua hiyo imeongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kusaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa wauguzi.
Hata hivyo, mmoja wa wauguzi wilayani humo, Rita Msigwa, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapatia vifaa vya kisasa pamoja na kuhakikisha stahiki zao zinalipwa kwa wakati.
“Tunaomba mazingira bora ya kazi pamoja na vifaa vya kisasa vya kutolea huduma ili tuweze kuwahudumia wagonjwa kwa ufanisi zaidi,” amesema Msigwa.
