Dk Mwigulu aagiza mfanyabiashara arudishiwe vitu vyakeDk Mwigulu aagiza mfanyabiashara arudishiwe vitu vyake

Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza mkazi wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kurejeshewa mara moja bidhaa zake za dukani, vifaa vya nyumbani pamoja na mashine ya kusaga zilizokuwa zinashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Mwigulu ametoa agizo hilo leo Jumamosi Mei 16, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mnenia wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Akisikiliza kero za wananchi, Waziri Mkuu alipokea malalamiko ya Mohamed Hassan aliyesema polisi walichukua bidhaa zake za dukani, mashine ya kusaga na vifaa vya nyumbani tangu Januari 24, 2026 na hadi sasa hajarejeshewa.

“Polisi walinifunga kwa miezi miwili, lakini baada ya kutoka wameendelea kunizungusha bila kunirudishia vifaa vyangu. Bidhaa wanataka wanipe nusu, nikakataa kwa sababu siyo haki,” amesema Hassan mbele ya mkutano huo.

Kutokana na malalamiko hayo, Dk Mwigulu alimwelekeza OCD wa eneo hilo kuhakikisha vifaa hivyo vinarejeshwa mara moja ili mhusika aweze kuendelea na shughuli zake za kujipatia kipato.

“OCD mrudishieni bidhaa zake, vifaa vya nyumbani pamoja na mashine yake ya kusaga. Mmeshamfahamu, mwacheni afanye kazi,” amesema.

Waziri Mkuu pia aliwataka watendaji wa Serikali kuacha tabia ya kukamata vitendea kazi vya wananchi bila sababu za msingi, akisema hatua hiyo inaweza kuwaathiri kiuchumi wananchi wanaotegemea shughuli hizo.

“Tusichukue vitendea kazi vya wananchi, kwani hizo ni ofisi za wenzetu. Kama pikipiki au gari limetumika katika uhalifu au mauaji au dawa za kulevya au ubakaji hapo tuna kila sababu ya kukamata hivyo vitu kama vidhibiti,” amesema.

“Sasa, niambieni bidhaa za dukani, mashine ya kusaga au godoro tunavichukua vya nini? Vinahusika vipi na kesi yake? Mhusika mwenyewe yupo na nanyi mnamjua. Hata kama upelelezi bado unaendelea, ndiyo mnachukua mpaka godoro? Rudisheni vifaa vyake vyote na RPC unipatie taarifa zake,” amesema.

Amesema hivyo ni vitega uchumi vya watu na wasipoangalia wanaweza kujikuta wanatengeneza wezi kwa kuwaondolea wananchi mitaji yao.

“Huyu mmeua mtaji wake na yeye ana wategemezi. Lazima tuheshimu mitaji ya watu,” amesema.

Amesema mali zinazotakiwa kushikiliwa ni zile zinazohusishwa moja kwa moja na uhalifu mkubwa kama dawa za kulevya, mauaji au ubakaji, lakini si bidhaa za biashara au vifaa vya kawaida vya nyumbani.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kondoa ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema wilaya hiyo imeendelea kunufaika na maboresho ya sekta ya afya tangu mwaka 2015.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa imepata vituo saba vipya vya afya, huku sita kati yake tayari vikiwa na magari ya wagonjwa.

Dk Kijaji pia aliomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kolo hadi Mnenia ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kwa wakazi wa eneo hilo na vijiji jirani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *