Kumalizika enzi za kutekeleza kwa lazima amri za kimabavu za madola ya MagharibiKumalizika enzi za kutekeleza kwa lazima amri za kimabavu za madola ya Magharibi

Pars Today – Majid Nili Ahmadabadi, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ujerumani amejibu kauli za kansela wa nchi hiyo alizotoa baada ya mazungumzo ya simu na rais wa Marekani Donald Trump, akisema kwa maandishi kwamba: “Enzi ya kutekeleza kwa lazima amri za kimabavu na za upande mmoja za madola ya Magharibi, zimekwisha.

Baada ya mazungumzo ya simu na Donald Trump aliporejea Marekani kutokea China, kansela wa Ujerumani Friedrich Mertz amedai katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Iran lazima irudi kwenye meza ya mazungumzo, Lango Bahari la Hormuz lazima lifunguliwe, na Tehran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia.” Akijibu kauli hizo za kansela wa Ujerumani, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo naye amejibu kwa maandishi akisema kuwa, enzi za kutoa amri za lazima kwa mataifa mengine hazipo tena. Aidha Balozi Majid Nili amepinga madai yasiyo na msingi ya Friedrich Mertz, akisisitiza kwamba Iran haijawahi kuwa na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia na kansela huyoi wa Ujerumani analijua vizuri jambo hilo. Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ujerumani ameongeza kwamba, kama lengo la viongozi wa Magharibi ni kuiwekea mashinikizo Iran kwa kutia chumvi kama hivyo, wanapaswa pia wasisahau uzoefu wa kushindwa Marekani na Israel mbele ya taifa shujaa la Iran.

Sehemu muhimu ya majibu ya Balozi wa Iran kwa kauli za Kansela wa Ujerumani ni ile iliyofichua mgongano wa wazi katika matamshi na vitendo vya Mertz na viongozi wengine wa Ulaya wanaodai kupigania amani na ubinadamu. Balozi Nili amewakhutubu viongozi wa Ujerumani akiwaambia, ikiwa wasiwasi wenu ni amani kweli, mlipaswa kwanza kutekeleza jukumu la kibinadamu la kulaani jinai iliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni ya kushambulia na kuua kwa umati na kikatili wanafunzi wa Skuli ya Kimsingi ya Minab nchini Iran. Siku ya kwanza ya uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran yaani tarehe 28 Februari 2026, Marekani iliishambulia kikatili skuli ya wasichana wadogo ya Shajare Tayyebe katika mji wa Minab wa kusini mwa Iran kwa kutumia makombora kadhaa ya Tomahawk. Katika uhalifu na jinai hiyo mbaya sana, wanafunzi 168 wadogo wa kike waliraruliwa vipande vipande na makombora hayo ya Marekani. Watoto hao wa Iran walichomwa moto hai na wazimawazima katika ukatili huo wa kupitiliza wa Marekani. Viongozi wa Marekani wanatamba kwa kufanya uhalifu huo mkubwa. Lakini hakuna hata serikali moja ya Ulaya iliyonyanyua ulimi kulaani jinai hiyo; halafu viongozi wa madola ya Magharibi akiwemo kansela wa Ujerumani wanajipa uthubutu wa kujitokeza hadharani na kudai kuwa eti wanatetea amani na ubinadamu.

Picha za kuhuzunisha za watoto hao waliokatika viungo zilienea kote ulimwenguni, lakini kutoka Berlin hadi Paris na kutoka London hadi Roma, hakuna serikali ya Ulaya iliyotoa hata taarifa nyepesi tu ya kulaani jinai hiyo ya kutisha mno. Si Friedrich Mertz wala mwenzake yeyote wa Ulaya waliokuwa tayari kunyanyua ulimi kusema kwamba mauaji ya watoto 168 walio chini ya umri wa miaka kumi yaliyofanywa na Marekani na Israel yalikuwa ni jinai. Hizo ni tawala zile zile zinazotoa maazimio ya haraka na kuchukua hatua kubwa za kidiplomasia kwa kila tukio nchini Ukraine au nchi inayowaunga mkono lakini kuhusu Malaika hao wa Iran wameamua kukaa kimya kabisa kama hakuna chochote kilichotokea. Lakini ukimya wao huo umewafedhehesha mbele ya macho ya walimwengu.

Kitendo cha Mertz cha kutumia cheo chake cha kansela wa Ujerumani kushirikiana na Trump kuipangia Iran nini cha kufanya na wakati huo huo anashindwa kusema hata neno moja la kulaani jinai walizofanyiwa watoto 168 wa Iran, kinamfanya kansela huyo wa Ujerumani kuwa mshirika wa moja kwa moja wa jinai za Trump na Wazayuni wenzake katika uhalifu huo wa wazi na mkubwa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajua vyema kwamba madola ya Magharibi yanataka kuinyima Iran haki zake zisizoweza kukanushika, kama vile kutumia vizuri nafasi yake ya kijiografia katika Ghuba ya Uajemi na Lango-Bahari la Hormuz. Iran inajua vyema kwamba siasa za nchi za Ulaya na Marekani ni kunyamazia kimya jinai yoyote inayofanywa na kila mwenye misimamo kama yao hata kama jinai hiyo itakuwa kubwa kupindukia kama ya kuuliwa kidhulma na kwa umati watoto wadogo wa kike 168 wa Iran wasio na hatia yoyote.

Matamshi ya Balozi wa Iran nchini Ujerumani ya kwamba zama za “hewallah bwana” zimekwisha na madola ya Magharibi hayana uwezo tena wa kuyatwisha mataifa huru amri zao za kiimla na kibeberu. Iran ya leo ni Iran ya baada ya kusimama imara kukabiliana na vikwazo, mauaji na vita vikubwa. Ni nchi ambayo imeonesha kivitendo kwamba hakuna shinikizo linaloweza kuipigisha magoti. Maadamu tawala za Ulaya zinaendelea kukataa kuwalaani waziwazi wauaji wa watoto wa Iran, hazina haki ya kuipa Iran ushauri wa kimaadili. Kama alivyosisitiza Balozi wa Iran, upatanishi wa kweli utaanza kwa kulaani jinai hiyo kubwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni na sio kukariri kibubusa matamshi yale yale ya kikoloni na kushirikiana na Ikulu ya White House katika jinai zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *