
YANGA inatembea na kifungo cha Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ikizuiwa kusajili lakini kama unadhani ni kwamba klabu hiyo inadaiwa unakosea, ishu ni tofauti ikimuhusisha kiungo wao wa zamani, Stephanie Aziz KI.
Iko hivi; Yanga imefungiwa na FIFA baada ya kuchelewa kutoa taarifa ilizotakiwa kuwasilisha juu ya fedha za mauzo ya wachezaji wake waliouzwa msimu uliopita, ikitakiwa kufanya hivyo ndani ya muda maalum ambao ilipewa awali.
Kushindwa kufanya hivyo, FIFA ikaishushia adhabu hiyo ya kutakiwa kutosajili mchezaji yoyote ndani ya vipindi vitatu, adhabu ambayo imeanza mara moja.
Mchezaji wa mwisho ambaye Yanga ilimuuza ni Aziz KI kwenda Wydad Juni 2025, lakini pia mashtaka hayo yanawahusisha wachezaji ambao walitolewa kwa mkopo ambao nao taarifa zao za malipo ya mkopo zinatakiwa kuwasilishwa.
“Yanga sio kwamba wanadaiwa au labda walishindwa kumlipa mchezaji kama ambavyo wengi wanadhani, adhabu yao ni tofauti, unajua FIFA ina utaratibu wake kwamba kila taarifa ya mauzo ya mchezaji pamoja na wale unaowatoa kwa mkopo wanataka kujua fedha zilizotumika,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya TFF.
“Yanga hawajawasilisha taarifa hiyo, kawaida FIFA wanakupa muda maalumu kama siku 14 uwasilishe lakini ukishindwa ndio adhabu kama hii wanakushushia ili ukamilishe na ukikamilisha ndani ya muda huo wanakufungulia.
“Ninachofahamu mimi ni kwamba adhabu hii Yanga wamepewa kwa kuwa kwenye nyaraka hawakutuma wamemuuza Aziz KI kwa bei gani kwa kuwa ndiye mchezaji wa mwisho kuuzwa kwa bei ghali,” kilisema chanzo.
Aidha bosi huyo aliongeza kuwa, endapo Yanga itashindwa kuwasilisha taarifa hiyo ndani ya vipindi hivyo vitatu vya usajili, shauri hilo litapelekwa kamati ya nidhamu ambapo huko ndio adhabu kali inaweza kuikumba klabu hiyo.
“Ukipelekwa kamati ya nidhamu huko sasa ndio inatoka adhabu kali zaidi maana FIFA inaona umeendelea kuwa mkaidi lakini kama wakiwasilisha taarifa hiyo hata sasa wakijiridhisha itaondolewa adhabu.
Wachezaji ambao Yanga imewatoa kwa mkopo msimu huu ni pamoja na viungo Moussa Bala Conte (Raja Athletic), Celestin Ecua (JS Kabylie), Mohamed Doumbia (Marumo Gallants), Denis Nkane (TRA United) na Offen Chikola (Singida Black Stars).
