Pointi 21… Pasua kichwa Simba, YangaPointi 21… Pasua kichwa Simba, Yanga

VITA ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2025/26 imeingia katika hatua ya lala salama yenye presha na lawama huku tofauti ya pointi mbili pekee kati ya Yanga na Simba ikinogesha mbio hizo, makocha watia neno.

Yanga wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 54 huku Simba wakifuatia kwa karibu katika nafasi ya  pili na pointi 52 huku zilisalia mechi saba ambazo zina pointi 21 za kuamua, hali inayofanya kila mchezo kuanzia sasa kuwa kama fainali.

Katika mazingira ya sasa, sio ubora wa kikosi pekee unaotajwa kuamua ubingwa, bali pia rekodi za nyuma, uimara wa vikosi, uwezo wa kutumia nafasi na namna timu zinavyoweza kucheza kwenye presha ya matokeo.

Kwa upande wa Yanga, ratiba yao iliyobaki inaonyesha watakutana na Singida Black Stars (nyumbani), Namungo (nyumbani), Mashujaa (ugenini), Fountain Gate (ugenini), Azam FC (nyumbani), TRA United (nyumbani) pamoja na JKT Tanzania (ugenini).

Katika mechi dhidi ya Singida BS ambayo itachezwa Mei 22 kwenye Uwanja wa KMC, Yanga wataingia wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi katika michezo mitatu iliyopita.

Machi 5, 2026  Yanga walicheza ugenini dhidi ya Singida Black Stars na kushinda mabao 3-0  katika mechi ya mzunguko wa kwanza huku Februari 17, 2025 ambapo ilikuwa ni mechi ya pili ya msimu uliopita wakishinda nyumbani kwa mabao 2-1 na Oktoba 30, 2024 wakishinda ugenini kwa bao 1-0, jambo linaloonyesha wananchi wamekuwa na ubora mkubwa wanapokutana na wapinzani hao.

Dhidi ya Namungo, Yanga pia wana rekodi nzuri inayowapa matumaini makubwa kuelekea mchezo huo muhimu wa mwisho wa msimu. Februari 22, 2026 walishinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Namungo, kabla ya kushinda mabao 3-0 nyumbani Mei 13, 2025.

Novemba 30, 2024 walishinda tena ugenini kwa mabao 2-0 huku safu yao ya ulinzi ikionekana kuwa imara zaidi katika michezo hiyo.

Dhidi ya Mashujaa ndipo Yanga wameonyesha ukatili mkubwa zaidi katika rekodi zao za hivi karibuni. Januari 19, 2026 waliifunga Mashujaa mabao 6-0 wakiwa nyumbani, kabla ya kushinda mabao 5-0 ugenini Februari 23, 2025. Desemba 19, 2024 walishinda nyumbani kwa mabao 3-2.

Fountain Gate nao wamekuwa wakipata wakati mgumu mbele ya Yanga, Desemba 4, 2025 Yanga walishinda mabao 2-0 nyumbani, Aprili 21, 2025 wakashinda ugenini kwa mabao 4-0 huku Desemba 29, 2024 wakipata ushindi mwingine wa mabao 5-0 wakiwa nyumbani.

Katika michezo hiyo mitatu dhidi ya Fountain Gate, Yanga wamefunga mabao 11 bila kuruhusu bao lolote, jambo linaloonyesha tofauti kubwa ya kiwango kati ya timu hizo.

Hata hivyo, Azam FC wanaonekana kuwa miongoni mwa timu zitalkazotoa ushindani mkubwa zaidi dhidi ya Yanga katika mbio hizi za ubingwa.

Machi 15, 2026 Yanga walitoka sare ya 0-0 ugenini dhidi ya Azam, Aprili 10, 2025 wakashinda ugenini kwa mabao 2-1, huku Novemba 2, 2024 wakipoteza nyumbani kwa bao 1-0.

Mechi dhidi ya TRA United, Yanga itakuwa na mtiani mwingine kutokana na kiwango cha timu hiyo, ambapo katika mzunguko wa kwanza walitoka suluhu ugenini Machi 18, 2026 huku katika mechi mbili za msimu uliopita wakishinda na kuchapwa moja.

Yanga ilishinda kwa mabao 3-0 ugenini Aprili 2, 2025 na kupoteza mabao 3-1 nyumbani Novemba 7, 2024, mechi iliyomtibulia aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi.

Kwa upande wa JKT Tanzania, Yanga wameonekana kuwa na ubora mkubwa zaidi baada ya kushinda mabao 5-0 nyumbani Februari 25, 2026, kutoka sare ya 0-0 ugenini Februari 10, 2025 na kushinda mabao 2-0 nyumbani Oktoba 22, 2024.

Kwa upande wa Simba, wekundu hao wa Msimbazi watakutana na Coastal Union (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), Pamba Jiji (nyumbani), Mbeya City (ugenini), Mtibwa Sugar (ugenini), Singida BS pamoja na KMC zote nyumbani.

Dhidi ya Coastal Union, Simba wana rekodi nzuri baada ya kushinda mabao 2-0 nyumbani Aprili 2, 2026 na kushinda mabao 3-0 ugenini Machi 1, 2025. Hata hivyo, Oktoba 4, 2024 walitoka sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Coastal Union matokeo yaliyotibua hesabu za ubingwa wakiwa chini ya Fadlu Davids.

Dodoma Jiji nao wamekuwa wakitoa changamoto kwa timu kubwa wametoka kuichapa Yanga kwa mabao 3-2 na katika mechi ya mwisho dhidi ya Simba walitoka suluhu kwa upande wa msimu uliopita, Mnyama alishinda mechi zote mbili alianza ugenini Septemba 29, 2024 kwa bao 1-0 kisha wakati wakiwa nyumbani, Machi 14, 2025 ilikuwa kwa mvua ya mabao 6-0.

Dhidi ya Pamba, Simba ilitoa sare ya bao 1-1 Machi 19, 2026 kwenye duru la kwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku msimu uliopita wakishinda kwa mabao mabao 5-1 nyumbani Mei 8, 2025 na kushinda bao 1-0 ugenini Novemba 22, 2024.

Mbeya City wamekuwa wakipata wakati mgumu mbele ya Simba walifungwa

mabao 3-0 nyumbani Desemba 4, 2025 na katika mechi mbili za msimu uliopita walipoteza kwa mabao 3-2 Januari 18, 2023 huku mchezo wa Novemba 23, 2022 ukiisha kwa sare ya mabao 1-1.

Kwa upande wa Mtibwa Sugar, Simba walitoka sare ya 1-1 nyumbani Januari 18, 2026 katika mechi ya mzunguko wa kwanza huku mbili za nyuma wakishinda kwa mabao 2-0 Mei 3, 2024 wakiwa nyumbani na mabao 4-2 ugenini Agosti 17, 2023.

Dhidi ya Singida Black Stars, Simba walishinda kwa mabao mabao 2-1 ugenini Machi 11, 2026 katika mechi za mzunguko wa kwanza huku kwa matokeo ya msimu uliopita wakishinda kwa bao 1-0 ugenini Desemba 28, 2024 na kupata ushindi kama huo nyumbani, Mei 28, 2025.

Mechi ya mwisho ya msimu kwa Simba ni dhidi ya KMC ambao wamekuwa na rekodi mbaya dhidi ya Mnyama, wamechapwa katika mechi tatu zilizopita, walifungwa mabao 2-0 nyumbani Februari 11, 2026 na msimu uliopita walipoteza kwa mabao 2-1 Mei 11, 2025 na 4-0 Novemba 6, 2024.

WASIKIE MAKOCHA

Kufuatia kupoteza mchezo wao uliopita na kuruhusu Simba kupunguza tofauti ya pointi kileleni, kaimu kocha mkuu wa Yanga, Abdihamid Moalin, alisema kilichobaki kwa sasa ni kuangalia mechi zilizopo mbele yao na kuhakikisha timu inarejea kwenye wimbi la ushindi.

Moalin alisema matokeo yaliyopita hayawezi kubadilishwa lakini kikosi chake kina wajibu wa kuonyesha tabia ya timu kubwa katika kipindi hiki muhimu cha mwisho wa msimu.

“Huu ni wakati wa kutazama mbele kwa sababu hakuna ambacho tunaweza kubadilisha kuhusu matokeo yaliyopita, tuna mechi muhimu mbele yetu na tunapaswa kufanya vizuri. Lazima tuonyeshe namna ambavyo timu kubwa inatakiwa kujibu mapigo,” alisema Moalin.

Kwa upande wa Simba, kocha mkuu Steve Barker alisema bado wanaamini wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa iwapo wataendelea kupata matokeo mazuri katika michezo iliyosalia.

“Jambo muhimu kwetu ni kuendelea kufanya vizuri katika mechi zilizobaki. Bado tunaamini tuna uwezo wa kutwaa ubingwa na tunapaswa kubaki na umakini katika kila mchezo,” alisema Barker.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *