
Canada. Mke na mume wote wanapaswa kuwa vichwa vya ndoa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ndoa huundwa na watu wawili wenye haki na wajibu unaolingana.
Bila mmoja wao, hakuna ndoa. Ndiyo maana katika vyeti vya ndoa, wanaowajibika kisheria ni watu wawili pekee yaani mume na mke.
Wengine wanaohusika ni wafungishaji ndoa na mashahidi. Zaidi ya hapo, watoto ni matokeo ya ndoa, lakini hawana mamlaka ya kuamua au kuendesha taasisi hiyo kisheria.
Kutokana na hali hiyo, dhana ya baadhi ya mila na imani zinazomtangaza mume kuwa kichwa pekee cha familia inaweza kutazamwa kama mtazamo unaochochea ubaguzi wa kijinsia. Makala hii inalenga kujadili kwa mtazamo mpana kwamba ndoa ni taasisi inayopaswa kuongozwa kwa ushirikiano na usawa kati ya mke na mume.
Kwa muda mrefu, baadhi ya mifumo ya kijamii na kidini imekuwa ikimpa mwanaume nafasi ya juu zaidi kuliko mwanamke ndani ya ndoa.
Hali hii imejenga dhana kwamba mwanamke ni mtu wa kutawaliwa au kutumika kulingana na matakwa ya mwanaume.
Mfano wa hoja zinazotumiwa kuhalalisha mtazamo huo ni simulizi zinazodai mwanamke aliumbwa kutoka kwenye ubavu wa mwanaume.
Hata hivyo, hoja hizo zimeendelea kuibua mijadala kuhusu mantiki, usawa na nafasi halisi ya mwanamke katika jamii.
Wapo wanaojiuliza kama simulizi hizo zililenga kuhalalisha mfumo dume uliotumika kuwanyima wanawake haki na usawa.
Aidha, baadhi ya maandishi ya kale humwelezea mwanamke kama “msaidizi” wa mwanaume, jambo ambalo wengine hulitafsiri kama kupunguza thamani na mchango wa mwanamke katika ndoa na jamii kwa ujumla.
Mtazamo wetu
Katika mjadala huu, tunajaribu kuangalia ndoa kwa mtazamo wa kijamii zaidi kuliko wa kidini.
Sababu ni kwamba ndoa huathiriwa kwa kiasi kikubwa na tamaduni za jamii husika. Tamaduni nyingi zimejengwa juu ya mila, desturi na mitazamo ya wale walioziunda, hali ambayo wakati mwingine imechangia kuendeleza mfumo wa unyonyaji na ubaguzi wa kijinsia.
Kwanza, tunatenganisha mjadala huu na simulizi za kidini kuhusu Adamu na Eva, kwa kuwa lengo letu si kuchambua dini bali kujadili nafasi ya mke na mume ndani ya ndoa ya kisasa.
Pili, tunaangazia namna ubaguzi, unyanyasaji na unyonyaji wa kijinsia ulivyogeuka changamoto kubwa katika ndoa na jamii kwa ujumla.
Katika mazingira hayo, mwanamke mara nyingi amewekwa katika nafasi ya chini kiasi cha kunyimwa hata utambulisho na mamlaka ndani ya familia.
Tatu, tunaangalia umuhimu wa kichwa katika maisha ya viumbe, hasa binadamu.
Kichwa hubeba ubongo, ambao ni kitovu cha uamuzi, fikra na utambuzi. Kisayansi, viungo muhimu kama moyo, ini, mapafu na ubongo ndivyo huwezesha uhai wa mwanadamu.
Hata hivyo, ubongo ndio kiungo kikuu kinachosimamia utendaji wa mwili mzima.
Binadamu anaweza kuishi bila baadhi ya viungo kama mikono au miguu, lakini hawezi kuishi bila kichwa.
Nne, kichwa ndiyo alama kuu ya utambulisho wa binadamu. Sura ya mtu hubebwa na kichwa, na ndiyo sehemu inayotumika katika vitambulisho rasmi kama pasipoti au kadi za benki.
Katika utambuzi wa mtu, kinachotambulika kwanza ni uso na kichwa chake, si viungo vingine vya mwili.
Tano, hata katika matumizi ya kawaida ya lugha, neno “kichwa” huashiria heshima, akili na uwezo wa kuongoza. Mtu akiitwa “kichwa” mara nyingi huonekana mwenye thamani na uwezo mkubwa.
Hali hii inaonesha namna jamii inavyokipa kichwa umuhimu wa kipekee.
Kwa msingi huo, tunaamini kuwa mume na mke wote ni vichwa vya familia.
Pale ambapo ushirikiano, kuheshimiana na usawa vinapopewa nafasi katika ndoa, hujenga mazingira ya kuaminiana, kusaidiana na kuondoa hofu ya kudhalilishwa, kunyanyaswa au kunyonywa.
Ndoa yenye mafanikio si ile inayotawaliwa na upande mmoja, bali ile inayojengwa katika msingi wa ushirikiano na kuheshimiana kati ya wawili wanaounda taasisi hiyo.
