
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikionya matumizi ya mabaunsa katika shughuli za ulinzi, Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA) kimelaani matumizi ya mabaunsa kwa shughuli hizo, kufanya fujo na kuleta madhara kwa watu na mali zao.
Kwa mujibu wa TSIA, mabaunsa hawapaswi kutumika kwa shughuli hizo na kwamba kuna kampuni zinazotoa mafunzo kwa baadhi yao, na wanaofuzu ndiyo wanaotakiwa kutumika kwa ajili ya ulinzi wa mali za watu.
Kauli ya chama hicho inakuja siku chache baada ya Gazeti la Mwananchi kuchapisha habari kuhusu matumizi ya mabaunsa kama walinzi na athari zinazosababishwa.
Katika habari hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohamed Mahmoud, aliliambia Mwananchi kuwa hakuna sheria inayowatambua mabaunsa nchini, na kutumika kama walinzi ni kinyume cha sheria.
Mei 15, 2026, TSIA kupitia mwenyekiti wake, Felix Kagisa, ilitoa taarifa ikirejea habari iliyochapwa katika gazeti la Mwananchi, toleo namba 9405 la Mei 14 mwaka huu.
“Taarifa hii inatolewa na TSIA baada ya taarifa iliyoachapishwa kwenye gazeti la Mwananchi, toleo namba 9405 la tarehe 14 Mei 2026,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chama hicho kinaungana na Serikali kulaani matumizi ya mabaunsa kwa shughuli za ulinzi, kufanya fujo na kuleta madhara kwa watu na mali zao.
Sambamba na hilo, TSIA kupitia taarifa hiyo imefafanua kuhusu kazi za mabaunsa, kikisema kitaalamu hutumika kwenye milango ya kuingilia matamasha au sherehe maalumu.
“Hawa huwa ni kama maofisa wa usalama wenye jukumu la kudhibiti uingiaji wa wageni au waalikwa kwenye sherehe au matamasha, kuhakikisha usalama na kudumisha utulivu, hasa kwa kuangalia vitambulisho,” imeeleza.
Katika milango hiyo, imesema mabaunsa hudhibiti idadi ya watu ukumbini au kwenye eneo la sherehe, kupunguza migogoro na kuondoa wateja wasiotii kama ni eneo la kibiashara.
“Wanafanya kama safu ya kwanza ya ulinzi kuwaweka wageni salama wanaoshiriki au waalikwa kwenye tamasha,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa mabaunsa hawawezi kutumika kama walinzi wa mali za watu.
Imeeleza kuwa kampuni za ulinzi zilizosajiliwa na kuwa wanachama wa TSIA hutoa mafunzo maalumu kwa walinzi wake na kuhakikisha wanaotumika kwenye malindo ni wale waliofuzu mafunzo hayo.
“Tunahakikisha kuwa wanaotumika kwenye malindo ni wale waliofuzu mafunzo na wanafanya kazi kwa weledi, uaminifu na kuzingatia sheria za nchi,” imeeleza taarifa hiyo.
Chama hicho kimewasihi Watanzania wote na wale wanaohitaji huduma ya ulinzi wa watu na mali zao kuhakikisha wanatumia walinzi wa kampuni zilizosajiliwa kisheria na wanachama wa TSIA.
Mbali na TSIA, Mwenyekiti wa Chama cha Mabaunsa na Bodyguard Tanzania, Faraji Robert maarufu Dax, amesema mabaunsa waliandaliwa mahsusi kwa ajili ya kushiriki michezo mbalimbali ya nguvu kama kuvuta magari na kubeba mizigo mizito.
Amesema kumekuwa na mkanganyiko kati ya makundi hayo mawili, jambo linalochangia baadhi ya vikundi vya watu kujifanya mabaunsa na kufanya vitendo visivyo halali kwa kutumia jina la ubaunsa.
“Wakati mwingine tunasikia baunsa amempiga mtu, amemkamata mwanamke na kumpeleka gesti, amevunja nyumba au kuharibu makazi ya watu. Hayo siyo malengo ya kazi tuliyoianzisha,” amesema Dax.
Amesema kupitia utafiti wao walioufanya wamebaini kuwepo kwa kikundi fulani kinachofanya shughuli hizo kinyume cha sheria za nchi.
“Watu wanaofanya matukio hayo si mabaunsa halisi, bali ni watu waliovamia tasnia hiyo kwa kuvaa mavazi ya ubaunsa na hivyo kuharibu taswira yetu,” amesema Dax alipozungumza na Kituo cha Radio cha Wasafi FM.
Dax ametolea mfano tukio la mwaka 2014 eneo la Madale, Dar es Salaam, ambapo kulikuwa na mgogoro wa viwanja uliosababisha vifo vya mabaunsa zaidi ya 20.
“Baadaye ilibainika kuwa kazi ile ilifanyika kiholela na mabaunsa waliitwa bila kufuata utaratibu,” amesema.
Amesema kuna wakati baadhi ya mabaunsa hudanganywa na watu wanaojiita madalali wa mahakama kwa kuonyeshwa nyaraka za kughushi zinazodaiwa kusainiwa na viongozi mbalimbali. Kutokana na changamoto za kiuchumi na elimu ndogo kwa baadhi yao, hujikuta wakiingia kwenye mtego huo.
“Baunsa anaoneshwa karatasi iliyosainiwa na jaji fulani, kumbe ni ya kughushi. Watu wasiokuwa waaminifu wanafanya hivyo na wengine wanaingia kwa sababu ya kutafuta fedha,” amesema.
Dax amesema chama hicho kimekuwa kikifanya vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kutoa elimu kwa mabaunsa kuhusu watu wanaovamia kazi hiyo bila kuwa na weledi wala mifumo rasmi ya utendaji.
“Tulisisitiza kuwa anayehitaji kufanya kazi hiyo anapaswa kuchukuliwa alama za vidole polisi, atambulike anatoka wapi na awe kwenye mfumo rasmi ili kudhibiti uhalifu,” amesema.
Amesema kuwa asilimia kubwa ya wanaojihusisha na ubaunsa ni watu waliokosa ajira nyingine na kuingia kwenye shughuli hiyo bila kufuata utaratibu uliowekwa.
Kuhusu suluhisho
Dax amesema chama hicho kinatarajia kufanya mkutano mkubwa Dar es Salaam utakaowakutanisha viongozi kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Mwanza, Dodoma, Lindi na Arusha, pamoja na Jeshi la Polisi.
“Tunalenga kueleza ukweli kuhusu tasnia hii na kuweka wazi vikundi vilivyovamia shughuli zetu na kufanya kazi ambazo hatuzitambui,” amesema.
Pia, ameiomba Serikali kuwapa nafasi ya kusikilizwa, kama ilivyokuwa awali hadi walipofanikiwa kuanzisha chama hicho mwaka 2019.
“Tunaomba Serikali pamoja na kampuni za ulinzi tushirikiane kuweka mfumo mzuri wa utambuzi wa watu hawa kuanzia wanakozaliwa, wanakoishi hadi kuandaa kanzidata maalumu ili iwe rahisi kutambua wahusika pale matukio yanapotokea,” amesema.
Amesema lengo lao ni kuwa kundi rasmi la kusaidia shughuli za ulinzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, huku wakitarajia kutambuliwa rasmi na kupewa vitambulisho vya kazi.
Historia ya mabaunsa
Asili ya jina baunsa ni neno la Kiingereza ‘bouncer’ linalomaanisha kupiga kwa nguvu au kusukuma.
Lilianza kutumika rasmi Marekani katika miaka ya 1860 kumaanisha mtu mwenye kazi ya kumrusha au kumtupa nje kwa nguvu mtu anayefanya fujo.
Mwaka 1875, neno hilo lilichapishwa rasmi kwenye kitabu cha The Young Outlaw, kikielezea mteja aliyetupwa nje ya mgahawa baada ya kukataa kulipia chakula, na hapo ndipo jina hilo lilipopata umaarufu.
Peter Sharkey anatajwa kuwa baunsa wa kwanza kupata umaarufu nchini Marekani katika miaka ya 1880. Alikuwa akilinda ukumbi maarufu wa Harry Hill’s, New York.
Sharkey alikuwa na mwili mkubwa na alikuwa bondia wa zamani aliyeweza kuwatoa nje watu watatu wakorofi kwa mara moja bila shida.
Kuanzia miaka ya 1970, kumbi za muziki wa disko zilivuta maelfu ya watu, hivyo hitaji la mabaunsa likawa kubwa kuliko kipindi chochote.
Wamiliki wa baa walianza kuwatafuta makusudi wacheza mieleka, wanyanyua vyuma na mabondia kuwa mabaunsa wao ili sura na miili yao tu itishe wafanya fujo kabla hawajaanzisha vurugu.
