Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3
Taarifa za kifo cha mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, Felicien Kabuga zimepokelewa nchini humo na kote duniani huku wengi wakijuliza maswali kuhusu haki ambayo waathiriwa wa vitendo vyake walikuwa wanaitafuta kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.
Kisheria, kifo chake kinatamatisha kesi dhidi yake iliyokuwa ikiendelea katika mahakama maalum ya kimataifa inayosikiliza kesi za jinai – IRMCT– iliyopo mjini The Hague nchini Uholanzi.
Kwa sasa mawakili wanapojiandaa kupokea taarifa za ni wapi kesi hiyo inakwenda baada ya sasa.
Kwa jamaa za waliouawa kikatili katika mauaji hayo yaliyoanza Aprili 7 mwaka 1994 na kudumu kwa mwezi mzima, taarifa hii inafunga ukurasa muhimu katika historia ngumu sana ya taifa hilo la Afrika Mashariki ambapo takribani watu laki nane waliuawa baada ya kushambuliwa na Kundi la jamii ya WaHutu iliyofahamika kama INTERAHAMWE ambao ilichochewa kumaliza INYENZI {mende kwa lugha ya Kinyanrwanda.}
Kabla ya kujipatia umaarufu kwa kufadhili mauaji hayo dhidi ya jamii ya waTustsi nchini Rwanda, Kabuga alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda aliyekuwa na ushawishi mkubwa vilevile katika ulingo wa siasa za taifa hilo.
Haya hapa ni mambo Matano kumhusu mzee huyo aliyefariki akiwa mwenye umri wa miaka 93, jijini The Hague ambapo alikuwa ana zuiliwa na mamlaka za usalama na ambapo pia kesi yake ilikuwa imeanza kusikilizwa lakini ikasimamishwa kwa muda usiojulikana katika mahakama ya umoja wa mataifa ya International Residual Mechanism for Criminal Tribunals (IRMCT)
1: Alikuwa Tajiri na ushawishi mkubwa
Kabla ya mauaji ya kimbari ya 1994, Kabuga alikuwa akitambuliwa kama mtu mwenye utajiri mkubwa zaidi nchini Rwanda. Mali yake ilitokana na biashara ya kahawa na majani chai. Pia alikuwa mwendani wa karibu wa kisiasa na shemeji wa Rais wa zamani Juvenal Habyarimana.
2: Alitumia mali yake kufadhili mauaji
Upande wa mashtaka ulimfungulia kesi Kabuga katika mahakama ya ICC, akituhumiwa kwa mauaji ya kimbari na vile vile mashtaka ya ukiukaji wa haki za kibinadamu. Kabuga anashutumiwa kwa kutumia mali yake kufadhili na kununua silaha zilizotumiwa na Kundi la Interahamwe na kuchangia kubuniwa kwa hazina iliyofahamika kama NATIONAL DEFENCE FUND kwa ajili ya kunua silaha.
3: Alitumia kituo chake redio kusambaza chuki
Kabuga alimiliki kituo cha redio na televisheni cha RADIO TELEVISION LIBRE DES MILLE COLLINES (RTLM). Kituo hicho kilikuwa na umuhimu mkubwa katika kampeni ya kuwamaliza WaHutu nchini Rwanda kwa muda huo ambapo mauaji yalipangwa na kutekelezwa. Watangazaji wake walitakiwa kutangaza taarifa za uchochezi na propaganda ya chuki dhidi ya jamii ya WaTutsi kutoka kwa jamii ya WaHutu.
4: Alikwepa kukamatwa kwa miaka 26
Kwa wakati mmoja vyombo vya habari nchini Kenya viliripoti kwamba Kabuga alikuwa anaishi mafichoni nchini Kenya n ahata baadhi yao yakafanya uchunguzi kutafuta ukweli kuhusu madai hayo.
Kenya ilikanusha madai hayo mara kwa mara ikisema kwamba Kabuga hayupo nchini humo na wala serikali haiwezi kushirikiana na mtu ambaye alikuwa ni mshukiwa wa uhalifu na aliyekuwa akitafutwa na mamlaka za usalama za kimataifa.
Kutokana na uwezo wake mkubwa kifedha, mfanyabiashara huyo alitumia fedha na kushirkiana na marafiki wake na washirika wake katika mataifa mbali mbali duniani kujificha kwa takriban miaka 26, kabla ya kukamatwa.
Marekani ilikuwa imetoa Zawadi ya Dola Milioni 5 kwa yeyote atakaye toa taarifa muhimu kumhusu Kabuga. Lakini ujanja wake ulifikia ukingoni mnamo May 2020 alipokamatwa na maafisa wa usalama Jijini Paris , Ufaransa.
5: Kesi yake ilisimamishwa kwa sababu ya hali mbaya ya afya yake
Baada ya kukamatwa nchini Ufaransa, ilichukuwa muda kabla shughuli rasmi za mahakama ya kimataifa ya jinai ICC kuanza. Alipelekwa mbele ya mahakama maalum ya kimataifa ya Umoja wa mataifa ya {International Residual mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) iliyopo mjini The Hague, mnamo 2022.
Hata hivyo miezi michache baadaye mwaka wa 2023, Majajji waliosimamia kesi hiyo walitangaza kwamba Kabuga hangeweza tena na kesi hiyo kutokana na afya yake ya akili kwani alithibitishwa na daktari kwamba anauguwa ugonjwa wa DEMENTIA ambao huathiri uwezo wa ubongo kuhifadhi kumbukumbu muhimu.
Kutokana na hali hiyo, kesi ilisimama kwa muda huo wote, mahakama ikisubiri kupata taarifa muhimu kutoka kwa Kundi la wataalamu waliokuwa wakimpa huduma ya matibabu.
Kabuga amefariki kabla ya kesi hiyo kurejelewa, huku wengi wakihofia kwamba huenda haki walioitamani itazikwa naye kaburini.
Serikali ya Rwanda haijatoa taarifa kuhusu kifo chake Kabuga.
