Waliokuwa wafanyakazi Teku wakwaa kisiki mahakamaniWaliokuwa wafanyakazi Teku wakwaa kisiki mahakamani

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) uliokuwa umewapa ushindi wafanyakazi wanane wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), ikisema walikiuka taratibu za ndani za rufaa kabla ya kufungua shauri lao.

Mahakama ilieleza wafanyakazi hao walikosea kisheria kwa kushindwa kwanza kutumia utaratibu wa ndani wa rufaa kabla ya kupeleka mgogoro wao CMA.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 11, 2026 na jopo la majaji watatu ambao ni Rehema Mkuye, Dk Eliezer Feleshi na Dk Deo Nangela, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo ya madai namba 1459/2024.

Baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote, Mahakama hiyo ilibatilisha kesi yote kuanzia CMA hadi Mahakama Kuu, na kueleza kuwa wafanyakazi hao walipaswa kwanza kutumia Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya Wafanyakazi ya Teku kabla ya kupeleka mgogoro wao CMA.

Maombi hayo ya madai yalifunguliwa na Bodi ya  Wadhamini ya Teku na Makamu Mkuu wa Chuo hicho dhidi ya Hamis Bakari, Nyanjige Mayala, Boany Dahaye, Edson Wikedzi, Ndinhesya Asukenie, Mponjoli Mwandamboi, Ishmail Mwambapa na Amani Simbeye.

Mgogoro huo ulianza baada ya wafanyakazi hao waliokuwa wakifanya kazi kama wakufunzi na wahadhiri kufukuzwa kazi Septemba 6, 2013 kufuatia tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa nidhamu.

Miongoni mwa tuhuma hizo ni kuanzisha kampuni binafsi iitwayo Grow Big Company iliyodaiwa kufanya shughuli zilizokuwa na mgongano wa masilahi na mwajiri wao, kutumia anwani ya Teku kuendesha shughuli hizo pamoja na madai ya kuwafungia viongozi wa chuo ofisini.

Pia, mjibu madai wa nne, sita na nane (Edson, Mponjoli na  Amani) pamoja na wafanyakazi wengine ambao hawakutajwa majina, walishtakiwa kwa kumfungia kinyume cha sheria, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (DVC-finance), Israel Mwaikenda, ofisini kwake kwa muda wa saa nne.

Mmoja wa wafanyakazi hao (Amani) alituhumiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari ndani ya eneo la chuo bila kibali.

Kutokana na makosa hayo, kikao cha nidhamu kiliendeshwa na kamati ya nidhamu Agosti 29 na 30, 2013 na kuwaona washakiwa wana hatia na kupendekeza wafukuzwe kazi, hatua iliyotekelezwa Septemba 6, mwaka huo.

Katika barua zao za kufukuzwa kazi walipewa haki ya kukata rufaa ndani ya siku tano, kwa kamati ya rufaa ya nidhamu ya wafanyakazi lakini badala yake waliamua kufungua shauri CMA wakidai kufukuzwa kwao hakukuwa halali.

Wakiwa CMA, wafanyakazi hao walidai mchakato wa nidhamu ulikuwa na upendeleo kwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Israel ndiye alikuwa pia mlalamikaji katika shauri hilo.

Pia, walidai kamati hiyo haikuwa imeundwa kihalali kwa kuwa mmoja wa wajumbe hakukidhi sifa zilizotakiwa kisheria.

Walieleza pia kuwa sheria walizotuhumiwa kuzikiuka hazikuwepo rasmi na kwamba adhabu waliyopewa ilikuwa ya kibaguzi kwa kuwa wafanyakazi wengine waliotuhumiwa kwa makosa yanayofanana hawakufukuzwa kazi.

Teku ilitetea hatua hiyo ikisema taratibu zote zilifuatwa na wafanyakazi walipewa nafasi ya kujitetea kabla ya uamuzi kufikiwa.

Baada ya kusikiliza pande zote, CMA iliamua kuwa kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao kulikuwa si halali kiutaratibu na kimsingi.

Tume hiyo iliwapa fidia ya mishahara ya miezi 50, fidia ya jumla ya Sh60 milioni kwa kila mfanyakazi pamoja na mafao mengine ya ajira.

Hata hivyo, Teku ilikata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Mahakama Kuu ilikubaliana kwa kiasi kikubwa na CMA kwamba kufukuzwa kazi kulikuwa batili, lakini ikapunguza kiwango cha fidia kutoka mishahara ya miezi 50 hadi miezi 15 na kufuta malipo ya Sh60 milioni yaliyotolewa kama fidia ya jumla.

Bado Teku haikuridhika na ikaamua kukata rufaa Mahakama ya Rufaa.

Uamuzi majaji

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Mahakama ya Rufaa iliibua masuala mawili muhimu ya kisheria, likiwamo suala la wafanyakazi hao kushindwa kutumia utaratibu wa ndani wa rufaa kabla ya kwenda CMA.

Jaji Nangela amesema suala hilo lilikuwa la msingi kwa sababu taasisi ilikuwa tayari imeweka mfumo rasmi wa kushughulikia rufaa za kinidhamu.

Mahakama ilieleza kuwa matumizi ya mifumo ya ndani ya utatuzi wa migogoro si jambo la hiari bali ni takwa muhimu la kisheria.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, matumizi ya utaratibu wa ndani humpa mwajiri nafasi ya kurekebisha makosa bila kupeleka mgogoro nje ya taasisi, huku yakisaidia kujenga rekodi muhimu zinazoweza kutumika baadaye mahakamani.

Mahakama ya Rufani ilinukuu uamuzi wake wa awali katika kesi ya Bayport Financial Services dhidi ya Cresense Mwandele pamoja na kesi ya Isaya Joseph Chawinga dhidi ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ikisisitiza kuwa muhusika lazima amalize kwanza taratibu zote za ndani kabla ya kwenda kwenye vyombo vya nje kama CMA.

Majaji walibaini kuwa wafanyakazi hao walikuwa wanafahamu uwepo wa Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya Wafanyakazi ya Teku lakini waliamua kutoiwasilisha rufaa yao huko.

“Kuachwa huku kulikuwa na madhara makubwa na kuliharibu kesi zilizowasilishwa mbele ya CMA, ambazo zilianzishwa mapema,” ilieleza hukumu hiyo.

Kutokana na hitimisho hilo, Mahakama ya Rufaa ilieleza kesi yote iliyofunguliwa CMA ilikuwa batili tangu mwanzo, hali iliyofanya pia uamuzi wa Mahakama Kuu kukosa msingi wa kisheria.

Kwa kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Mahakama ilibatilisha kesi zote zilizokuwa zimefunguliwa mbele ya CMA pamoja na hukumu ya Mahakama Kuu katika Marekebisho ya Kazi Na. 36 ya mwaka 2018.

“Uamuzi, amri na maagizo yote yaliyotokana na kesi hizo yameondolewa.”

Hata hivyo, Mahakama ilieleza kuwa wafanyakazi hao bado wanaweza kufuatilia madai yao ya ajira mbele ya Mahakama au katika chombo chenye mamlaka.

Mahakama ilieleza kila upande utabeba gharama zake yenyewe bila kuamriwa kulipa gharama za upande mwingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *