Alliance Girls imeendelea kuvuta hisia za mashabiki wa soka nchini kwa mtindo wao wa kipekee wa kuingia uwanjani wakiwa wamevalia mavazi ya asili kama vitenge, madera na mavazi mengine yanayoakisi urembo wa mwanamke wa Kitanzania.
Mbinu hiyo imeonekana kubadili mtazamo wa wengi kuhusu soka la wanawake, ambalo kwa muda mrefu baadhi ya watu linawaharibia taswira yao na ni mchezo wa wanaume.
Kwa sasa soka limekuwa na ushawishi mkubwa kwa watu wa jinsia zote na kwa upande wa wanawake limezidi kukua huku kwa Alliance wakionyesha pamoja na kuvutia wanawake wengi, lakini hauwezi kubadili taswira yao.
Msemaji wa Alliance Girls, Jackson Luca aliliambia Mwanaspoti wazo hilo lilianzia kwa wachezaji wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wa timu, wakilenga kuonyesha mwanamke anaweza kucheza soka na wakati huo huo kubaki nadhifu, mwenye mvuto na kujiamini.
“Lile wazo lilitoka kwa wachezaji na viongozi tukawa tunajadiliana. Mara ya kwanza tulipoona watu wamependa, tukafikiria tufanye nini tofauti kwenye mechi inayofuata. Tunashukuru mwitiko umekuwa mkubwa.”
Amesema wachezaji wa timu hiyo pia hufuatilia maoni ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii na wengi wamekuwa wakitoa pongezi kwa ubunifu huo unaoonyesha upande mwingine wa maisha ya wanasoka wa kike.
Kwa mujibu wa Luca, hatua hiyo inalenga kuondoa dhana iliyojengeka katika jamii, wanawake wanaocheza soka lazima waige maisha na muonekano wa kiume.
“Hata wachezaji wenyewe husoma maoni ya mashabiki. Tumekuwa tukiwahimiza, hata kama kila mmoja ana maisha yake nje ya uwanja, wanapokuwa timu moja waonekane wanapendeza kama wanawake wa kawaida,” amesema.
Hatua hiyo ya Alliance Girls imeanza kubadili taswira zilizojengwa dhidi ya wanawake wana9ocheza soka kwa kuonyesha linaweza kuwa jukwaa la vipaji, nidhamu na mvuto wa kipekee unaoweza kuvutia mashabiki, wadhamini na jamii kwa jumla.
Luca anaamini ongezeko la mashabiki na mijadala inayoendelea inaweza kufungua milango ya fursa mpya za kibiashara.
“Tumegundua si mashabiki hawataki kufuatilia soka la wanawake, na si kwamba hakuna wadhamini, tatizo ni namna mchezo wenyewe unavyoonekana. Mapokeo yamekuwa makubwa sana na tunaamini tukiendelea hivi tutapata matokeo mazuri zaidi,” amesema.
