LEO Jumapili Mei 17, 2026, inapigwa Dabi ya Mjini itakayokamilisha mzunguko wa 25 wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kati ya Malindi dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Mlandege, kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, saa 10:00 jioni.
Dabi hiyo itakuwa na mambo matatu, kwanza imeshikilia hatma ya Malindi kujinusuru kushuka daraja ambapo sasa ipo katika mstari mwekundu ikishika nafasi ya 14 ikikusanya pointi 25. Malindi inahitaji kushinda michezo mitano kati ya sita iliyobaki ili kujinusuru isishuke daraja.
Pili, Mlandege iliyo nafasi ya sita na pointi 40, inahitaji kushinda michezo mitatu mfululizo ili kuingia nafasi ya nne bora, hivyo ushindi dhidi ya Malindi ni muhimu.
Tatu, Malindi inahitaji kukataa unyonge baada ya kupoteza mechi ya kwanza ilipofungwa 3-0, huku Mlandege ikitaka kuendeleza ubabe wake kwa kubeba pointi sita za dabi hiyo msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Malindi, Ramadhan Sanga, amesisitiza kuwa hawawezi kushuka daraja na wataonesha maajabu kati mchezo huo kwa kuipiga Mlandege.
“Malindi inaenda kukataa unyonge mbele ya Mlandege na kujinusuru kushuka daraja, tupo imara na tutawashangaza watu katika mchezo huu,” amesema.
Wakati Malindi ikicheza na Mlandege, Fufuni itaikaribisha KVZ kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba kuanzia saa 10:00 jioni ikiwa ni mechi ya raundi ya 26.
Mechi hii inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwani KVZ inaongoza msimamo na pointi 52, wakati Fufuni ni ya tatu na pointi 48.
