Mama asimulia alivyouza mashamba, atoa figo kumwokoa bintiyeMama asimulia alivyouza mashamba, atoa figo kumwokoa bintiye

Dar es Salaam. Katika Kijiji cha Nyarikungu, Kitongoji cha Nyagunge wilayani Magu, mkoani Mwanza, maisha ya Rosemary Mtiro (63) yalikuwa ya kawaida ya mwanamke anayejitafutia riziki kupitia kilimo.

Lakini ndani ya miaka michache, maisha yake yalibadilika kabisa baada ya mwanawe, Olivia Fabian Rweganwa (26) kuanza kuugua ghafla akiwa chuoni.

Rosemary anasema mwaka 2022 alipokea simu ambayo hakuwahi kutarajia kutoka kwa Olivia aliyekuwa akisoma kozi ya uhazili (katibu muhtasi) ngazi ya cheti mkoani Tabora.

“Alinipigia simu akaniambia anakojoa damu. Nilimwambia aende hospitali, wakaambiwa ana UTI sugu. Akapewa dawa, akameza dozi na akaendelea na masomo,” anasimulia Rosemary kwa sauti ya utulivu iliyobeba uchungu wa miaka mingi.

Rosemary Mtiro akimwangalia binti yake Olivia Rweganwa siku chache baada ya kumchangia figo. Olivia alipandikizwa figo hiyo Mei 9, 2026 katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Baada ya kumaliza mwaka wake wa masomo, Olivia aliondoka Tabora na kwenda kwa dada yake Karagwe, mkoani Kagera. Hata hivyo, hali yake iliendelea kudhorota.

“Kila alipokwenda hospitali aliambiwa ni UTI. Lakini mwili ukaanza kuvimba, tumbo kujaa maji na hali ikawa mbaya zaidi. Walimpeleka hospitali ya Karagwe, baadaye Bukoba mjini, lakini bado hali yake haikuwa inaeleweka,” anasema mama huyo.

Anasema ilifika wakati Olivia alipoteza nguvu kabisa hadi wakalazimika kuomba rufaa ya haraka kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza.

“Tulipofika Bugando hali yake ilikuwa mbaya sana. Macho yalikuwa yamemtoka, alikuwa hoi. Madaktari walimpokea haraka na hapo ndipo walipogundua figo zote zimefeli.”

Olivia aliingizwa kwenye matibabu ya dialisisi mara moja na kwa muda mrefu maisha yake yalitegemea mashine za kusafisha damu.

“Mwaka wa kwanza mpaka wa tatu alikuwa anasafishwa damu mara tatu kwa wiki. Alikuwa mahututi sana lakini Mungu akamsaidia akatoka chumba cha wagonjwa mahututi,” anasema Rosemary.

Gharama za matibabu

Lakini pamoja na matumaini ya kuendelea kuishi, gharama za matibabu zilianza kuisukuma familia ukingoni mwa maisha.

Rosemary anasema aliuza kila kitu alichokuwa nacho ili kugharamia matibabu ya mwanawe.

“Niliuza mashamba yote. Nilikuwa na ekari tatu na nusu pamoja na majaluba. Tiba ilikuwa ghali sana. Kwa sasa sina tena mashamba,” anasema.

Rosemary akizungumza na wataalamu wa afya wodini.

Anasema wakati mwingine walibaki bila fedha kabisa hadi akaamua kwenda Wizara ya Afya, mkoani Dodoma kuomba msamaha wa matibabu.

“Walinisikiliza na kunipa msaada wa matibabu bure kwa sera ya afya. Hilo lilitusaidia sana maana gharama zilikuwa kubwa mno.”

Hata hivyo, baada ya miaka ya dialisisi, Rosemary alianza kufikiria njia ya kudumu zaidi ya kumuokoa mwanawe.

“Nikajiambia, mwanangu bado mdogo. Alianza kuugua akiwa na miaka 22, sasa ana miaka 26. Bado hajatimiza ndoto zake. Nikasema lazima nimsaidie.”

Uamuzi huo ulimfikisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam ambako yeye na mwanawe walifanyiwa vipimo vya upandikizaji wa figo.

Awali familia ilikaa kikao, pacha wa Olivia ndiye alisema angeweza kutoa figo, lakini madaktari waliona bado alikuwa mdogo.

“Madaktari waliniambia hata mimi ninaweza kumsaidia. Nikasema sawa, bora mwanangu aendelee kuishi.”

Rosemary, ambaye ni mjane tangu mume wake afariki dunia Januari 20, 2024, anasema hakusita hata kidogo kufanya uamuzi huo.

“Nina watoto saba, hawa mapacha ndiyo wa mwisho. Tayari nilishampoteza mtoto mmoja. Sikuwaza mara mbili.”

Rosemary aliruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) siku tatu tu baada ya kumchangia mwanawe figo kupitia teknolojia ya upasuaji wa tundu dogo (laparoscopic surgery), tofauti na upasuaji wa kawaida ambao humlazimu mgonjwa kukaa hospitalini kwa muda mrefu zaidi kutokana na maumivu na muda wa kupona.

Rosemary anasema hali yake inaendelea vizuri na kwamba huduma aliyopata kutoka kwa madaktari bingwa wa Muhimbili imempa imani kubwa juu ya uwezo wa wataalamu wa afya nchini.

Anasema tangu alipofika Muhimbili Oktoba mwaka jana alikuwa akiendelea kufanyiwa vipimo mbalimbali hadi Mei 9, 2026 mwanawe alipofanyiwa upandikizaji wa figo kwa mafanikio.

Rosemary anaeleza kuwa upasuaji huo wa tundu dogo haukuacha kovu kubwa mwilini kama ilivyo katika upasuaji wa kawaida.

Hii ni mara ya kwanza, Muhimbili kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wanne kwa kutumia teknolojia hiyo ya kisasa inayorahisisha uponaji wa haraka kwa wagonjwa na wachangiaji wa figo.

Jopo la madaktari Watanzania kutoka ndani na nje ya nchi, wakifanya upasuaji wa kuvuna figo kwa Rosemary Mtiro (63) kwa njia ya matundu ‘Laparascopy’ kabla ya kuipandikiza kwa Olivia. Kabla ya teknolojia hiyo, upandikizaji umekuwa ukifanyika kwa kufungua tumbo.

Lakini pamoja na mafanikio ya upandikizaji, changamoto bado ipo. Rosemary anasema dawa za baada ya upasuaji ni ghali mno.

“Dawa za kila siku zinagharimu zaidi ya Sh1.045 milioni kwa mwezi. Mimi sihitaji dawa nyingi, lakini mwanangu anahitaji dawa hizi maisha yake yote.”

Kwa sauti ya matumaini, mama huyo anatoa ombi lake la mwisho; “Namuomba Rais Samia atusaidie kupata dawa hizi ili mwanangu aendelee kuishi vizuri.”

Sindano ya ‘Powersafe’ yatajwa chanzo

Leo hii, baada ya upandikizaji kufanyika kwa mafanikio, Olivia anaendelea vizuri na matumaini ya kuanza maisha mapya yanaonekana kurejea tena.

“Najisikia vizuri sana. Mungu ni mwema,” anasema Olivia akiwa wodini.

Anasema kuugua kulimkatisha ndoto zake muda mfupi baada ya kuhitimu masomo ya uhazili.

“Nilikuwa nimehitimu tu nikaanza kuugua. Ndoto yangu ilikuwa kufanya kazi, kujitegemea na kuendelea kusoma zaidi,” anasema.

Olivia anasema madaktari walimweleza kuwa huenda figo zake ziliharibiwa na dawa za sindano alizokuwa akitumia miaka ya nyuma.

Rosemary Mtiro.

“Walisema kuna dawa za sindano zinaitwa ‘Powersafe’ nilizotumia ambazo zinaweza kuwa zilichangia kuharibu figo. Dalili zilianza taratibu tangu mwaka 2019 baada tu ya kuchoma hizo sindano lakini tatizo lilikuja kugundulika vibaya mwaka 2022.”

Licha ya mateso yote aliyopitia, Olivia anasema jambo kubwa lililompa nguvu ni kuona mama yake akijitoa kwa ajili yake.

“Nilijisikia faraja sana kuona ameonesha upendo mkubwa kiasi hiki kuokoa maisha yangu. Nampenda sana na namuombea maisha marefu.”

Anasema sasa matumaini yake ni kupata nafuu ya kutosha ili aanze tena kutafuta kazi na kujenga maisha yake.

“Baadaye nikitoka hapa nitaomba kazi sehemu yoyote. Ninaamini nitapata. Pia, natamani kuwa na familia yangu,” anasema Olivia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *