Kibaha. Wakati kukiwa na hofu kwa wananchi wa mtaa wa Kumba Shule Kibaha kwa Mfipa mkoani Pwani kwamba kuna simba ameonekana katika eneo hilo, serikali ya mtaa imeeleza kuwa aliyeonekana ni mnyama mwingine wa porini na si simba kama inavyoelezwa.
Taharuki hiyo imeibuka katika eneo la Kumba Shule ambapo ilidaiwa kuonekana kwa simba dume na jike katika makazi ya watu.
Taharuki hiyo ilisababisha wakazi wa eneo hilo kukumbwa na hofu na wengi wao kutotoka nje wakihofia usalama wao.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 17, 2026, Diwani wa Msangani ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa Kumba, Frank Msimbe amesema baada ya kuwepo kwa taarifa hizo aliwapigia simu polisi kata kuomba msaada.
Askari wa wanyamapori akifuatilia nyayo ambazo zilidaiwa kuwa ni za Simba
“Polisi kata iliwasiliana na askari wa wanyamapori ambao walifika haraka eneo la tukio na kubaini nyayo za mnyama aliyekuwa akidaiwa ni simba si za simba,” amesema.
Amesema uchunguzi wa askari hao wa wanyamapori ulibaini nyayo hizo ni za mnyama mwingine na si simba akiwataka wananchi kuondoa hofu na taharuki iliyokuwepo.
Akizungumzia namna alivyopata taarifa hizo, Mwenyekiti wa mtaa huo amesema alipigiwa simu saa 11 alfajiri na mmoja wa wananchi akidai kwamba amemuona simba ambaye kakimbia eneo la Kumba Shule
“Nilimwambia nenda kaangalie nyayo zake, lakini kwa kuwa kipindi hiki ni cha mvua, nilimshauri azifunike nyayo kadhaa ili zisifutike wakati tukiwasubiri askari wa wanyamapori, akazifunika na sufuria bovu,” amesema.
Amesema aliwapigia simu polisi kata ambao nao wakawasiliana na askari wa wanyamapori ambao walifika kwa haraka eneo la tukio.
Askari wa wanyamapori akifuatilia nyayo ambazo zilidaiwa kuwa ni za Simba
“Walizichunguza zile nyayo na kubaini sio simba ni mnyama tu mwingine wa porini lakini sio za simba,” amesema Msimbe bila kutaja ni nyayo za mnyama gani huku akieleza kuna watu wakimuona hata mbwa wa porini wanasema ni simba.
Msimbe amewasihi wakazi wa eneo hilo kuondoa taharuki na hofu akisisitiza askari wa wanyamapori wamewahakikishia eneo hilo halina simba baada ya kufanya uchunguzi katika maeneo yote yaliyodhaniwa mnyama huyo amepita.
Baadhi ya wananchi wa Kumba waliozungumza na Mwananchi wamesema walipata taarifa kwamba eneo hilo ameonekana simba dume na jike.
“Binafsi nilipata hofu, kusikia mtaani kuna simba, sikutoka nje hadi niliposikia taarifa kwamba mnyama aliyeonekana si simba,” amesema Aisha Juma.
Mkazi mwingine, Mwajuma Mafuru amesema, “Tunashukuru serikali ya mtaa ilichukua hatua za haraka hadi kuja askari wa wanyamapori na kufanya uchunguzi na kubaini sio kweli huku Kumba kuna simba.
