Mwili wa mtoto aliyepotea wakutwa na majeraha usoniMwili wa mtoto aliyepotea wakutwa na majeraha usoni

Njombe. Baada ya kutoweka kwa takriban siku sita, Alfa Nyalusi (7), mkazi wa Mtaa wa Kibena mkoani Njombe, amekutwa amefariki dunia shambani eneo la Howard na mwili wake ukiwa na majeraha usoni.

Mtoto Nyalusi, alipotea Mei 12, 2026, lakini mwili wake umekutwa kwenye tabaka la maji ukiwa umefunikwa na miti huko Kibena Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Wakizungumza wakati wa mazishi ya mtoto huyo, leo Jumatatu Mei 18, 2026, baadhi ya wananchi wamesema taarifa walizopewa ni kuwa mtoto huyo alikuwa anatoka shule, lakini hakufika nyumbani.

Wamesema baada ya hapo mzazi wake alitoa taarifa kwa wenzake na wananchi wakaungana kwa pamoja kumsaidia kumtafuta mtoto bila mafanikio.

Siwatu Lutumo, mkazi wa eneo hilo amesema tangu siku hiyo ilishindikana kumpata mtoto huyo kabla ya mwili wake kuonekana Mei 16, 2026 maeneo ya Howard huku ukiwa amewekewa miti juu.

Baadhi ya waombolezaji wakishiriki mazishi ya mtoto huyo katika eneo la Kibena, Halmashauri ya Mji wa Njombe, mkoani Njombe.

Amesema tukio hilo limewagusa na wanaomba vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi ili kuwabaini wahusika na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Tukio hili limetugusa tunaomba vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi ili muhusika aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibena Hospitali, Winfred Kayombo amesema baada ya kupata taarifa ya kupotea kwa mtoto huyo waliendelea kumtafuta bila mafanikio hadi walipofahamishwa kuonekana kwa mwili wake.

“Tulipokea taarifa kuna mtoto alikwenda shuleni lakini hajarudi nyumbani tuliwaomba majirani waendelee kumtafuta lakini kwa usiku ule hatukumpata,” amesema.

Amesema siku iliyofuata walikwenda kituo cha polisi kutoa taarifa huku wakiendelea kumtafuta bila mafanikio.

Diwani wa eneo hilo, Erasto Ngole ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuonesha ushirikiano ili waliohusika na tukio hilo wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amesema bado chanzo cha kifo cha mtoto huyo hakijafahamika lakini jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.

Amesema uchunguzi wa awali unaonesha kulikuwa na kutoelewana kati ya baba wa marehemu na mama.

“Pamoja na hayo bado chanzo cha kifo cha huyu mtoto hakijajulikana lakini tunaendelea na uchunguzi ili kubaini,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *