Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha na kupitisha Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kiasi cha shilingi Bilioni 334.34 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambayo itatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele tisa vya Wizara hiyo.
Akizungumza Bungeni Jijini Dodoma kabla wakati akijibu hoja za Wabunge kabla ya kuoitishwa kwa bajeti hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema Serikali imejipanga kufanya utafiti wa kina kwa lengo la kubaini sababu za migongano baina ya binadamu na wanyamapori na njia za kisayansi ya kuzitatua.
Dkt. Kijaji amesema serikali itafanya utafiti huo ili kusaidia kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto ya migongano baina ya binadamu na Wanyamapori hususani Tembo.
Kuhusu malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi, Dkt. Kijaji amesema serikali kupitia mfumo wa PAIS inaendelea kuboresha huduma hiyo na kuongeza kuwa awali kulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa kifuta jasho na kifuta macho I kutokana na sababu mbalimbali ambapo ilichukua takribani miezi sita hadi 12 kwa mwathirika kupokea fedha hizo tofauti na sasa ambapo takribani siku sita hadi 14 baada ya kutolewa taarifa mwathirika anapokea fedha hizo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akijibu baadhi ya hoja zilizohusiana na masuala ya nidhamu katika utumishi amesema Serikali haitamvumilia wala kumfumbia macho Mtumishi yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kWa kuzingatia nidhamu, weledi na utu katika kulinda rasilimali na kuendeleza uhifadhi.
Aidha, Mhe. Chande ametoa wito kwa watalaam wa Wizara na Taasisi zake kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu, Kanuni na Sheria pamoja na kuzingatia utu na kuwataka Wananchi nao kutovunja Sheria kwa kuwa uhifadhi na Maliasili zinazolindwa ni kwa manufaa ya Taifa zima.
Bajeti hiyo ya Bilioni 334. 34 imepitishwa na Bunge na kutoa fursa kwa Wizara hiyo kuanza utekelezaji wa mikakati yake katika kuendeleza uhifadhi na Utalii kwa mwaka wa fedha ujao 2026/2027.

(Feed generated with FetchRSS)
