Fursa mpya uwekezaji kupitia hatifungani yazinduliwaFursa mpya uwekezaji kupitia hatifungani yazinduliwa

Dar es Salaam. Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua hatifungani yake ya kwanza ya Sh100 bilioni kwa lengo la kuongeza uwezo wa utoaji mikopo, kuimarisha mtaji wa uendeshaji na kuwekeza katika majukwaa ya kisasa ya kidijitali huku ikipanua ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji nchini.

Hilo limelenga kufikiwa kupitia uzinduzi rasmi wa programu ya hatifungani ya muda wa kati ambayo ni ya kwanza nchini kutolewa na kampuni wakala wa soko la hisa pamoja na msimamizi wa mifuko ya uwekezaji.

Mpango huo umeanza kwa awamu ya kwanza inayolenga kukusanya Sh15 bilioni ikiwa na nyongeza ya Sh5 bilioni kupitia chaguo la ziada.

Kupitia hatifungani hiyo inayojulikana kama iTrust Bond, wawekezaji watapata riba ya asilimia 13 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka minne huku malipo ya riba yakifanyika kila baada ya miezi mitatu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance Limited, Faiz Arab amesema muundo wa hatifungani hiyo umeandaliwa kwa namna inayowavutia wawekezaji wa aina mbalimbali, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa ni Sh500,000.

Kiwango hicho kimewekwa ili kutanua wigo wa ushiriki wa watu wengi ambao wana uchumi wa hali zote.

“Kampuni hiyo ilibainisha kuwa pamoja na kutoa riba shindani yenye kiwango kisichobadilika, iTrust Bond pia inalenga kuongeza fursa za uwekezaji kupitia dhamana za mapato yasiyobadilika,” amesema.

Amesema muda wa ukomavu wa miaka minne pamoja na mfumo wa malipo ya kila robo mwaka utaifanya hatifungani hiyo kuwa mbadala ikilinganishwa na dhamana za kawaida za Serikali.

“Fedha zitakazopatikana kupitia mpango huu zitatumika kutekeleza mipango mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kuongeza uwezo wa utoaji mikopo, kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kidijitali pamoja na kuimarisha mtaji wa uendeshaji wa kampuni,” amesema.

Mbali na faida hiyo, iTrust imeeleza kuwa riba ya hatifungani hiyo haitakatwa kodi ya zuio hatua inayolenga kuwapa wawekezaji mapato ya uhakika na yanayotabirika.

“Hatifungani hiyo imeidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), na mauzo yamefunguliwa rasmi Mei 18, 2026 na yanatarajiwa kufungwa Juni 12, 2026,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Sera, Utafiti na Mipango kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Alfred Mkombo amesema kuzinduliwa kwa hatifungani hiyo unaonyesha kupiga hatua muhimu katika ustawi wa sekta ya fedha hususani masoko ya mitaji hapa nchini.

“Umoja huu utawezesha kufikia malengo ya Tanzania ya kuwa na soko imara na jumuishi linalotoa bidhaa bunifu na kuvutia uwekezaji wa ndani na kimataifa ambao utachochea ukuaji wa uchumi nchini,” amesema.

Amesema hatifungani hii ni sehemu ya mpango mkuu wa utekelezaji wa maendeleo ya sekta ya fedha wenye lengo la kuwezesha upatikanaji fedha za maendeleo zitakazoinufaisha sekta ya umma na binafsi.

“Bidhaa hii inaweza kutumika kama dhamana kupata mkopo wa dharura pia inampa mtu uhuru wa kuwekeza fedha ambayo itakuwa inamzalishia wakati yeye akiendelea na shughuli nyingine,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *