Wakili aliyepinga uchaguzi, mkutano mkuu TLS akwaa kisiki mahakamaniWakili aliyepinga uchaguzi, mkutano mkuu TLS akwaa kisiki mahakamani

Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imetupilia mbali rufaa ya Wakili Steven Cleophace aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupilia mbali shauri lake la mapitio ya kimahakama kupinga mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika  (TLS).

Mahakama hiyo imetupilia mbali rufaa hiyo baada ya kujiridhisha kuwa Mahakama Kuu ilikuwa sahihi katika uamuzi wake wa kutupilia mbali shauri hilo licha ya kwamba wajibu maombi walikubaliana na mwombaji katika shauri hilo la msingi.

Hukumu hiyo imetolewa Mei 12, 2026 na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo, Lugano Mwandambo (mwenyekiti wa jopo), Panterine Kente na Leila Mgonya

Chanzo cha mgogoro

Historia ya rufaa hiyo inaanzia kwenye maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa TLS na uchaguzi yaliyofanywa na Sekretarieti ya TLS mwaka 2024.

Kufuatia maandalizi hayo ya AGM na uchaguzi, Wakili Kitale ambaye ni mwanachama wa TLS aliyewahi kuwa mwakilishi wa Kanda ya Ziwa katika Baraza la Uongozi la chama hicho aliibua hoja mbili alizokuwa akizilalamikia.

Kwanza alidai kuwa uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ulifanyika bila kuzingatia masharti ya kisheria yanayosimamia suala hilo.

Hoja ya pili alidai kuwa kulikuwa na ongezeko lisilo la kawaida na lisilofuata utaratibu la ada ya usajili wa AGM kutoka Sh118,767 hadi Sh200,000 kuhudhuria mkutano ana kwa ana, akidai hatua hiyo ilifanyika bila idhini ya Baraza la Uongozi.

Maombi ya kibali

Kwa kuzingatia hoja hizo Wakili Kitale pamoja na wajumbe wengine wa Baraza la Uongozi waliomba kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TLS kupatiwa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali zinazohusu maamuzi hayo, lakini hawakupata majibu.

Badala yake alishauriwa kuwasilisha suala hilo kwa rais wa TLS ambako hata hivyo pia hakupata majibu.

Kutokana na mwenendo huo wa viongozi hao wa TLS kuhusu malalamiko yao hayo, Wakili Kitale alifungua shauri Mahakama Kuu akiomba ruhusa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama.

Katika shauri hilo la maombi namba 16018 la mwaka 2024  Wakili Kitale aliomba ridhaa kufungua shauri la mapitio ya mahakama kuiomba mahakama hiyo, itoe amri ya kutengua uamuzi wa TLS na kuilazimisha kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Pamoja na shauri hilo la maombi ya kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kimahakama, pia aliwasilisha maombi ya zuio la muda kusimamisha mkutano mkuu, uchaguzi na shughuli za kamati za uchaguzi hadi shauri hilo litakaposikilizwa na kuamuliwa.

Shauri la msingi

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Athuman Matuma ilimkatalia Wakili Kitale katika maombi yake ya kutoa amri ya zuio la muda kusimamisha mkutano huo mkuu, uchaguzi na shughuli za kamati za uchaguzi na kamati ya rufaa.

Hata hivyo, iliridhia wakili Kitale kufungua shauri hilo mapitio ya mahakama na Wakili Kitale akafungua shauri hilo la mapitio ya kimahakama, shauri la maombi namba 17558 la mwaka 2024, dhidi ya TLS, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo lililosikilizwa na Jaji Wilbert Chuma, mawakili wa wajibu maombi walikubaliana na maombi hayo ya wakili Kitale katika nafuu alizoziomba isipokuwa tu suala la gharama za shauri.

Hata hivyo, licha ya mawakili wa wajibu maombi kukubaliana na maombi ya mwombaji, Jaji Chuma katika uamuzi wake alioutoa Aprili 3, 2025,  alitupilia mbali shauri hilo pamoja na mambo mengine akisema kuwa hapakuwa na uamuzi ambao ulipaswa kufanyiwa mapito.

Pia, Jaji Chuma alisema kuwa shauri hilo lilikuwa limewasilishwa kabla ya wakati wake, na masharti ya awali yanayotakiwa kwa ajili ya kutolewa kwa amri hizo zilizokuwa zinaombwa hayakuwa yametimizwa.

Wakili Kitale hakuridhika na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, ndipo akakata rufaa hii Mahakama ya Rufani akiwasilisha sababu mbili za kupinga uamuzi huo.

Mosi, alidai kuwa Jaji (Chuma) alikosea kisheria kwa kumnyima haki ya kusikilizwa kwa usawa kinyume na haki ya msingi ya pande zote kusikilizwa kwa usawa.

Sababu ya pili ya rufaa alidai kuwa Jaji alitenda kinyume na sheria kwa kuendelea kuamua kustahili kwa shauri hilo bila kujali kuwa wajibu maombi walikuwa wameyakubali na hivyo alikiuka kanuni zinazosimamia mashauri ya mambo yanayobishaniwa.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, wajibu rufaa waliipinga rufaa hiyo wakiiomba mahakama iitupilie mbali.

Pamoja na mambo mengine wakidai kuwa jaji wa Mahakama Kuu alikuwa na wajibu wa kuhakikisha maombi yaliyopo mbele yake yana msingi wa kisheria hata kama yalikuwa yamekubaliwa na pande zote.

Uamuzi Mahakama

Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Rufani baada ya kuzingatia hoja za pande zote katika hukumu yake imesema kuwa mahakama haiwezi kutoa amri kwa sababu tu pande zimekubaliana.

Majaji hao wameeleza kuwa hata kama upande mmoja utakubali maombi ya upande kinzani, mahakama bado ina wajibu wa kuchunguza kama amri zinazoombwa zinaendana na sheria, haki na masilahi ya umma.

“Ridhaa ya wadaawa haiwezi kuondoa wajibu wa jaji kutumia mamlaka yake ya kimahakama kufanya uchambuzi wa sheria kabla ya kutoa uamuzi,” walisema majaji hao katika hukumu hiyo.

Katika uchambuzi wake, Mahakama hiyo ilikataa hoja kwamba mrufani hakusikilizwa, ikisema pande zote zilipewa nafasi ya kuwasilisha viapo, hoja na maelezo yao mbele ya mahakama.

Majaji walionya kuwa kuruhusu maombi yote kwa sababu tu hayakupingwa kunaweza kudhoofisha mfumo wa utoaji haki na kufungua mianya ya matumizi mabaya ya mahakama.

“Kwa kuzingatia sababu tulizozitoa hapo juu, mahakama hii inaona kuwa rufaa hii  haina msingi wa kisheria, hivyo inatupiliwa mbali bila kutoa amri yoyote kuhusu gharama za kesi,” wamesema majaji hao wakihitimisha hukumu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *