Chadema, Magereza watofautiana afya ya Lissu mahabusuChadema, Magereza watofautiana afya ya Lissu mahabusu

Dar es Salaam. Wakati Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikidai mwenyekiti wake, Tundu Lissu ana hali mbaya kiafya akiwa mahabusu Ukonga, uongozi wa Magereza umekanusha madai hayo ukisema kiongozi huyo yuko salama na afya yake ni njema.

Mjadala huo umeibuka kufuatia kauli za Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, aliyedai katika mikutano tofauti kuwa hali ya Lissu si nzuri, akiweka msimamo kuwa chama hicho hakitakuwa tayari kumpokea kiongozi huyo akiwa katika hali mbaya kiafya.

Lissu, ambaye amekuwa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, akikabiliwa na kesi ya uhaini, ameendelea kuwa kiini cha mjadala ndani na nje ya chama hicho ambacho kinazidi kushinikiza Serikali imwachie huru bila masharti, kwa madai kuwa kesi inayomkabili ni ya kisiasa isiyo na na masilahi kwa umma.

Juzi, akiwa mjini Geita katika mwendelezo wa mikutano ya Operesheni Katiba Mpya na “Free Tundu Lissu”, Heche alidai amepokea taarifa kutoka kwa mdogo wa Lissu, Vicent, kuwa mwenyekiti huyo alikuwa vibaya kiafya, na viongozi wa chama hicho wamezuiliwa wasiende kumuona gerezani.

“Wanaoruhusiwa kwenda kumwona ni ndugu zake, ameniambia tangu jana jioni (Mei 17) mwenyekiti wetu anaumwa tumbo linamkata na anaharisha, pia ana aumivu makali sana, mtu ambaye hana hatia.

“Hatutakubali kiongozi wetu alichukuliwa mzima, tunamtaka atoke akiwa mzima. Ni muhimu likaeleweka na mambo ya kufikiri Watanzania ni wajinga yameshapitwa na wakati,” alisema Heche.

Jana, pia akiwa Kahama Mjini, Mkoa wa Shinyanga, Heche alidai amezungumza na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, baada ya kumuona Lissu gerezani.

Kwa mujibu wa Heche, Lissu alipewa matunda mbalimbali ikiwemo chungwa, papai, embe na kipande cha nanasi kabla ya kuanza kusumbuliwa na maumivu makali ya tumbo.

“Alisema maumivu aliyoyapata ni makubwa kuliko aliyowahi kuyasikia maishani mwake licha ya kufanyiwa operesheni zaidi ya 36,” alisema Heche.

Alidai baada ya saa moja ya maumivu akiwa mahabusu, Lissu alifanikiwa kupata msaada kutoka kwa askari aliyekuwa akipita, ndipo akapelekwa kupata matibabu na baadaye kubainika kuwa alikuwa na amoeba.

Heche pia amesisitiza msimamo kuwa Chadema inamtaka Lissu atoke gerezani akiwa salama, akiongeza chama hicho kitahitaji uchunguzi wa kina wa afya yake mara atakapoachiwa.

Leo Jumanne, Mei 19, 2026, Mwananchi limemtafuta Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi ambaye amesema taarifa zinazozungumzwa kuhusu hali ya Lissu si za kweli kwa kuwa Lissu yuko imara na anaendelea vizuri kiafya.

“Anaendelea vizuri na afya yake ni njema. Hayo ni maneno yao ambayo wamekuwa wakiyazungumza kwa lengo la kuleta taharuki katika jamii,” amesema Mbezi.

Alipoulizwa kuhusu madai kwamba Lissu alipimwa na kubainika kuwa na amoeba, Mbezi amesema ugonjwa huo ni wa kawaida na unaweza kumpata mtu yeyote.

“Magonjwa mengine ni ya kawaida. Hata wewe ukiwa nyumbani unaweza kuugua amoeba, hivyo si jambo la ajabu,” amesema.

Mbezi amekanusha madai Lissu alipewa chungwa na baadaye akajisikia vibaya, akisema hali yake inaendelea kuwa nzuri.

“Kusema kwamba alipewa chungwa na akajisikia vibaya, hilo tunalikataa. Lissu anaendelea vizuri na afya yake ni njema kabisa,” amesema Mbezi.

Mwananchi limezungumza na Vicent Lissu ambaye amekiri ni kweli hali ya afya ya kaka yake ilikuwa mbaya siku ya Jumamosi, akidai alikula chakula kilichosababisha afya yake kuwa tete.

“Bahati nzuri alipata uchunguzi kutoka kwa madaktari siku hiyohiyo. Tunamshukuru Mungu kwa kuwa anaendelea vizuri,” amesema.

Baada ya ufafanuzi huo wa Jeshi la Magereza, Mwananchi ilimrejea Heche, ambaye amedai wao wana uhakika na wanachokisema kwa sababu watu waliowapa taarifa hizo ndiyo wanaosimamia chakula anachokula Lissu kila siku.

“Tuna uhakika na taarifa tulizonazo. Afya yake si nzuri na tutaomba jumuiya za kimataifa na tutaandika barua rasmi kuomba Lissu afanyiwe uchunguzi wa kina wa kibingwa akiwa gerezani, na Serikali iruhusu tufahamu hali yake ya afya,” amesema.

Heche amesema wanataka kiongozi huyo afanyiwe vipimo kwa sababu kadhaa. Kwanza, alisema Lissu alikuwa akihudhuria kliniki mara kwa mara kutokana na hali yake ya afya, lakini hadi sasa hajaruhusiwa kufanya uchunguzi huo maalumu.

“Mahabusu tunazijua, na mimi mwenyewe nimewahi kuwa mahabusu. Hakuna gereza nchini lenye vifaa vya uchunguzi wa kina wa afya zaidi ya zahanati za kawaida,” amesema.

Alipoelezwa kwamba Magereza wamesema afya ya Lissu ni njema, Heche amesema kauli ya Magereza taarifa hiyo ingekuwa na uzito kama ingetolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na weledi wake.

“Magereza wana zahanati za kupima malaria, ameoba na magonjwa mengine ya kawaida, lakini hatuwezi kujua hali ya ndani ya mwili wake kama hajapelekwa kwenye vipimo vikubwa,” amesema.

Amesema chama hicho kinaona ni muhimu kwa Lissu kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi wa kina kuliko uwezo wa huduma zinazopatikana magerezani.

“Pili, tunawaomba na kuwasihi Magereza wafanye kazi zao kwa weledi na waache siasa katika masuala muhimu kama haya. Kwa sababu kama jambo lolote baya likimtokea Lissu, watalazimika kuwajibika kwa Watanzania,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *