Ujenzi jengo la MSD Chato wafikia asilimia 57, kukamilika OktobaUjenzi jengo la MSD Chato wafikia asilimia 57, kukamilika Oktoba

Geita. Mradi wa ujenzi wa ghala la kisasa la kuhifadhia dawa na vifaa tiba la Bohari ya Dawa (MSD) unaojengwa Chato mkoani Geita umefikia asilimia 57, huku Serikali ikisema ukikamilika utarahisisha upatikanaji wa dawa na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh19 bilioni unatarajiwa kukamilika Oktoba 2026, ukiwa sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya katika mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma na Shinyanga.

Akizungumza Mei 20, 2026 wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema ujenzi huo ni muhimu katika kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na Magharibi mwa Tanzania.

Ghala jipya la Bohari kuu ya dawa(MSD) linalojengwa Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, litakaloongeza uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba kwa mikoa ya Geita, Shinyanga, Kagera na Kigoma pindi ujenzi utakapokamilika.

Mbali na ghala kubwa la kisasa lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800, mradi huo pia unahusisha ujenzi wa majengo ya utawala, ukuta wa uzio, jengo la ulinzi, jengo la jenereta, banda la taka pamoja na kisima cha maji.

Shigela amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati sambamba na kuimarisha usalama wa vifaa vya ujenzi ili kuzuia ucheleweshaji wa mradi.

“Mradi huu una umuhimu mkubwa kwa wananchi wetu, hivyo ni lazima utekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa na ndani ya muda uliopangwa,” amesema Shigella.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi wa Chato kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa kujenga nyumba bora na za kisasa zitakazoweza kuhudumia wafanyakazi na wageni watakaokuwa wakifika katika eneo hilo.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela akizungumza wakati wa ukaguzi wa jengo la ghala la Bohari kuu ya dawa(MSD) linalojengwa Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.

“Kadri huduma zinavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya makazi na huduma nyingine yatakavyoongezeka. Wafanyakazi watakaokuja hapa watahitaji sehemu za kuishi na huduma mbalimbali za kijamii,” amesema.

Ameongeza kuwa uwepo wa mradi huo karibu na Hospitali ya Rufaa ya Kanda unatarajiwa kuongeza idadi ya watu wanaofika Chato kwa ajili ya matibabu na kuuguza ndugu zao, hali itakayoongeza uhitaji wa nyumba za kulala wageni, biashara za chakula na huduma nyingine.

Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Hainan International inayotekeleza mradi huo, Mhandisi Patrick Laibo amesema hadi sasa ujenzi wa ghala umefikia asilimia 48 huku majengo ya ofisi yakifikia asilimia 60.

Amesema kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na MSD kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya muda uliowekwa kwenye mkataba wa Oktoba 19, 2026.

“Kwa sasa maendeleo yanaendelea vizuri na sisi kama mkandarasi tunalenga kukamilisha mradi huu kabla ya muda wa mkataba,” amesema Laibo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chato, Mange Ludomya ameishukuru Serikali kwa kuendelea kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Amesema uwekezaji huo utaongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi kupitia biashara mbalimbali zitakazozaliwa kutokana na ongezeko la shughuli za kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *