
Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh482 milioni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kisasa katika Bonde la Uyole, mkoani Mbeya, mradi unaolenga kufungua mawasiliano ya barabara ya mchepuko kutoka Uyole kuelekea Kasumulu na Songwe pamoja na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Mradi huo wa barabara wenye urefu wa kilomita 17, unahusisha ujenzi wa daraja katika Mtaa wa Utukuyu, Bonde la Uyole, eneo ambalo muda mrefu limekuwa changamoto kwa wananchi na magari kupita hasa kipindi cha mvua kubwa.
Daraja hilo linajengwa kwenye barabara ya mchepuko kutoka Mlima Nyoka, Uyole kuelekea Kasumulu wilayani Kyela mpakani mwa Tanzania na Malawi hadi Songwe.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 20, 2026, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad),Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Justine Mrope amesema awali eneo hilo lilikuwa halipitiki kwa urahisi kutokana na uwepo wa bonde kubwa pamoja na daraja dogo lililokuwa halina uwezo wa kupitisha magari makubwa.
“Awali magari makubwa yalishindwa kupita katika eneo hilo kutokana na miundombinu kuwa hafifu, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na wafanyabiashara,” amesema Mrope.
Amesema Serikali imeamua kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara ya mchepuko ili kufungua fursa za kiuchumi pamoja na kurahisisha wakulima kusafirisha mazao kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Baada ya kukamilika kwa daraja hili, barabara hiyo itaunganisha Uyole kuelekea Kasumulu wilayani Kyela mpakani mwa Tanzania na Malawi na kuwa lango muhimu la shughuli za kiuchumi,” amesema.
Mrope amesema kwa sasa ujenzi wa daraja umefikia hatua ya nzuri ya maandalizi ya kumwaga zege pamoja na kazi nyingine za msingi, huku akieleza kuwa baadhi ya maeneo kutoka Mlima Nyoka hadi Uyole Kati tayari yanaendelea kupitika.
Faida za mradi
Amesema mradi huo pia utasaidia kupunguza msongamano wa magari katika Barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam), hasa panapotokea ajali au dharura.
“Daraja hili likikamilika litakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi na madereva kwa kuwa magari yatakuwa na njia mbadala ya kupita kuelekea Kasumulu bila kukumbwa na changamoto za foleni katika barabara kuu ya Tanzam,” amesema.
Kauli za wananchi
Mkazi wa Mtaa wa Unyakyusa, Bonde la Uyole, Japhel Ndemwa amesema mradi huo utasaidia kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikumbwa na changamoto ya usafiri na usafirishaji wa mazao.
“Changamoto hii ya kuvuka eneo hilo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 50. Wakati wa mvua wananchi tulikuwa tunashindwa kuvuka na shughuli za kiuchumi kusimama kabisa,” amesema.
