
Dar es Salaam. Benki ya NMB imependekeza gawio la Sh610.15 kwa kila hisa kwa mwaka wa fedha 2025, sawa na Sh305.08 bilioni kufuatia mafanikio ya kifedha yaliyoifanya kuendelea kuimarisha nafasi yake sokoni.
Gawio hilo linajumuisha gawio la kawaida la Sh504.26 kwa kila hisa lenye thamani ya Sh252 bilioni pamoja na gawio maalumu la Sh105.89 kwa kila hisa lenye thamani ya Sh52.95 bilioni.
Iwapo litapitishwa na wanahisa, gawio hilo maalumu litakuwa la kwanza katika historia ya NMB na miongoni mwa malipo makubwa zaidi kuwahi kutolewa katika sekta ya benki nchini.
Akizungumza leo Jumatano, Mei 20, 2026 jijini Dar es Salaam kuelekea mkutano mkuu wa 26 wa Wanahisa wa NMB utakaofanyika Juni 10, 2026 ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, David Nchimbi amesema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa wanahisa kwa ajili ya kuidhinishwa.
Amesema mwaka 2025 ulikuwa wa kihistoria kwa benki hiyo kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa 2021-2025 ulioiwezesha NMB kuimarisha nafasi yake katika ukuaji na faida.
“Bodi inapendekeza gawio la kawaida pamoja na gawio maalumu ili yaidhinishwe na wanahisa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka. Hii inafanya jumla ya gawio lililopendekezwa kwa mwaka 2025 kuwa kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika sekta ya benki nchini,” amesema Nchimbi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa mkakati wa benki, uwekezaji katika teknolojia na maendeleo ya wafanyakazi pamoja na kuimarika kwa huduma za kifedha kidijitali.
Amesema benki hiyo imefikia faida kabla ya kodi ya Sh1.1 trilioni, hatua iliyoiwezesha kuwa kampuni ya kwanza nchini Tanzania kufikia kiwango hicho.
Baada ya ukaguzi wa mwisho wa hesabu, amesema faida baada ya kodi kwa mwaka 2025 iliongezeka kutoka Sh750 bilioni zilizotangazwa awali hadi kufikia Sh756 bilioni.
Zaipuna amesema thamani kwa wanahisa imeendelea kuongezeka ndani ya kipindi cha miaka mitano, jumla ya gawio imepanda kutoka Sh48 bilioni mwaka 2020 hadi zaidi ya Sh305 bilioni mwaka 2025.
Katika kipindi hicho, amesema bei ya hisa ya NMB katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka kutoka Sh2,340 mwaka 2020 hadi Sh13,130, huku thamani ya soko ya benki hiyo ikifikia Dola 2.7 bilioni za. Marekani
Mkurugenzi wa Uhusiano na Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano wa NMB, Innocent Yonazi amesema mafanikio ya mpango mkakati wa miaka mitano yanaonesha dhamira ya benki hiyo katika kujenga thamani endelevu kwa wanahisa na jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkutano Mkuu wa Mwaka, wanahisa pia watajadili masuala mengine ya kimkakati ikiwamo kuidhinisha malipo ya wakurugenzi, uteuzi wa wakaguzi wa nje na maboresho ya muundo wa uendeshaji wa benki hiyo.
