Mahakama yashindwa kuamua hatima kesi ya mgawanyo wa rasilimali ChademaMahakama yashindwa kuamua hatima kesi ya mgawanyo wa rasilimali Chadema

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeshindwa kutoa uamuzi wa pingamizi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili, kutokana na kutokamilika.

Uamuzi huo ulipangwa kutolewa leo Jumatano, Mei 20, 2026 na Jaji David Ngunyale aliyesikiliza pingamizi hilo. Hata hivyo, mahakama hiyo haikuweza kutoa uamuzi huo na badala yake itafanya hivyo Mei 28, 2026.

Akiahirisha uamuzi huo mpaka tarehe hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Hussein Mushi amesema kuwa Jaji Ngunyale ana majukumu mengine na   bado hajamaliza kuandika uamuzi huo.

“Kwa hiyo shauri hili linaahirishwa mpaka Mei 28, 2026,” amesema Naibu Msajili Mushi kwa niaba ya Jaji Ngunyale.

‎Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo wadaiwa wameibua pingamizi wakiiomba mahakama iitupilie mbali kwa madai kuwa ni batili.

Hivyo pingamizi hilo lilisikilizwa Mei 13, 2026 na Jaji Ngunyale na baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo akapanga kutoa uamuzi wake leo.

Hoja za pingamizi

Jopo la mawakili wa wadaiwa (watoa pingamizi) linaloongozwa na wakili Mpale Mpoki akishirikiana na mawakili Dk Rugemeleza Nshala, Hekima Mwasipu na Selemani Matauka liliieleza mahakama kuwa kesi haipaswi kuwepo mahakamani.

Walibainisha waombaji hawakukidhi matakwa ya Amri ya VII kanuni ya 1(e) ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC), inayotaka hati ya madai ya kesi ibainishe muda wa chanzo cha madai yao, kwamba mambo wanayoyalalamikia yalitokea lini.

Wanadai kuwa lengo la kutimiza masharti ya kanuni hiyo ni kuipa nafasi mahakama kupima kama kesi hiyo imefunguliwa ndani ya muda unaoelekezwa katika sheria yaani miaka sita.

Kwa mujibu wa mawakili hao, katika hati ya madai ya kesi hiyo hakuna hata aya inayozungumzia kuwa ni lini sababu ya madai ilitokea na kwamba katika aya ya nne ya hati ya madai waombaji wanaeleza kuwa sababu za madai yao bila kueleza zilianza lini.

Huku akiirejesha Mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali zilizokwishaamuliwa na Mahakama Kuu na zingine Mahakama ya Rufani, wakili Mpoki amedai kuwa kesi nyingine zimekuwa zikiondolewa mahakamani kwa kutokukidhi matakwa ya kanuni ya 1(e) ya CPC.

Walidai kuwa katika mashauri hayo Mahakama zimesema kuwa kama muda wa kuanza sababu za madai haujaonesha kunainyima mahakama uwezo wake wa kujua kama ina mamlaka ya kusikiliza kesi husika.

Majibu ya wadai

Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai (wajibu pingamizi), Shabaan Marijani, akisaidiana na mawakili Dido Simfukwe na Alvan Fidelis, walipinga hoja hizo wakidai kuwa hati ya kesi hiyo imeonesha ni lini sababu za madai zilianza.

Katika kuthibitisha hilo aliielekeza Mahakama katika aya ya mbalimbali ikiwemo ya saba mpaka ya 16 akieleza kuwa zimetaja tarehe mwezi na mwaka na nyingine zikionesha kuwa mambo wanayoyalalamikia yanaendelea mpaka sasa.

Hivyo kwa kuzingatia muda huo wa kuanza kwa mambo yanayolalamikiwa alidai kuwa umetajwa kwenye hati ya madai, Wakili Marijani, alisisitiza kuwa kesi  hiyo imefunguliwa ndani ya muda wa ukomo kama inavyotakiwa kisheria.

Hata hivyo wakili Nshala alidai kuwa aya ambazo wajibu pingamizi wamedai kuwa ndizo zinazoonesha muda wa lini mgogoro ulianza akitaja aya ya saba mpaka ya 14 hazielezi ni lini mgogoro ulianza na kwamba zinaeleza tu mambo wanayoyalalamikia.

“Kwa mfano aya ya 20 haisemi kuwa tarehe fulani mahali fulani viongozi fulani walisema maneno ya kuvunja Muungano,” amesisitiza Dk Nshala na kuhitimisha;

‎Katika kesi hiyo wadai wanadai kuwa  kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na katiba ya chama hicho.

‎Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo pamoja na mambo mengine wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *