
Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya, yametoa muda wa siku 40 kwa serikali kushughulikia ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake na vitendo vingine vya Ukatili wa Kijinsia, yakisema iwapo haitafanya hivyo wataitisha maandamano.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika taarifa yao ya hapo jana, mashirika hayo yanataka ukatili dhidi ya wanawake na dhulma za kijinsia kutangazwa janga la kitaifa, yakitaka kuundwa kwa mfuko wa kuwasaidia waathiriwa wa dhulma za kijinsia, polisi kuajibishwa na kampeni ya kitaifa ya kupambana na dhulma hizo.
Wito huu umerejelewa tena na chama cha wanasheria nchini Kenya, LSK, baada ya kufanya hivyo mwezi Machi mwaka huu, LSK ikisema ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia linatishia maisha, utu, usalama na haki za kikatiba za wanawake na wasichana nchi nzima.
Kwa mujibu wa shirikisho la mawakili wanaoshughulikia maswala ya wanawake, FIDA, visa 35 kati ya 70 vilivyoripotiwa mwaka huu vilikuwa vya kujeruhiwa au kudhalilishwa kingono na watu wa karibu.
Tukio la hivi karibuni ni la mwanamziki wa nyimbo za injili Rachel Wandeto, aliyeshambuliwa kwa tindi kali na baadaye kufariki akiwa hospital ya rufaa ya Kenyatta.
